Sunday, 27 September 2015

TANZANIA KUNUFAIKA NA MABILIONI YA MCC



RAIS Jakaya Kikwete, akIzungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), Dana Hyde, mjini New York, Marekani, jana. (Picha na Freddy Maro).

NA MWANDISHI WETU
HATIMAYE serikali imefanikiwa kuingia kwenye mpango wa awamu ya pili wa kupatiwa fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia la Millennium Challenge Corporation (MCC), zitakazoanza kutolewa mwakani.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Tanzania kutimiza masharti ya kuingizwa kwenye mpango huo ambapo, wajumbe wa Bodi ya MCC walipiga kura na kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.
Kuidhinishwa kwa fedha hizo kulitangazwa juzi na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana Hyde, katika mkutano wake na Rais Jakaya Kikwete, uliofanyika kwenye Hoteli ya JW Marriot Essex House, jijini New York, Marekani.
Hyde alisema Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu, chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, imeafiki namna ambavyo Tanzania inakabiliana ipasavyo dhidi ya rushwa na kuchukua hatua stahiki kwa watuhumiwa wa vitendo hivyo.
“Hongera mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC-2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” alisisitiza Hyde.
Tofauti na fedha zingine zinazotolewa na wafadhili duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inataka igharamiwe.
Hyde alibainisha kuwa baada ya kuidhinishwa, serikali inatakiwa kupeleka muhtasari kwenye bodi ya MCC, kuidhinisha fedha hizo ambazo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC–2, zitakwenda kuboresha huduma za umeme vijijini.
Kupitia mradi huo, asilimia 46 ya Watanzania wanapata huduma ya umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005, na sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa fedha za MCC-1.
Chini ya mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa  Dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na sh. bilioni 992.80).
Kiasi cha Dola milioni 698 (sawa na sh. trilioni 1.46) zilitolewa chini ya MCC-1, hivyo Tanzania itakuwa imepata jumla ya Dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Tanzania itakuwa nchi iliyopata kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.
Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro, na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Fedha hizo pia zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar na kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.

No comments:

Post a Comment