Tuesday 27 October 2015

CCM YAPINGA MATOKEO LONGIDO




NA SHAABAN MDOE, LONGIDO

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Longido, kimepinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo yaliyompa ushindi mgombea wa CHADEMA, Onesmo Nangole, kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi zima la upigaji kura, kuhesa na kutangaza matokeo.

Akizungumza na vyombo vya habari jana, katika ofisi za CCM mkoa wa Arusha, Katibu wa wilaya hiyo, Esupatu Naikara, alisema zoezi la uchaguzi tangu upigajikura, halikuwa la haki na amani kutokana na vurugu mbalimbali zilizokinzana na sheria za uchaguzi walizotia saini.

Aliitaja moja ya kasoro hizo kuwa ni ukiukwaji wa sheria ya mawakala, ambayo inakitaka kila chama kuweka wakala mmoja katika kila kituo, ambapo CHADEMA kiliweka mawakala zaidi ya 15 hadi 20 katika kituo kimoja hali iliyozua vurugu vituoni.

Alisema hali hiyo ilionekana zaidi katika maeneo ya nje ya mji, ambapo mawakala hao walikuwa wakifanya fujo vituoni wakati wote wa upigaji kura, kuhesabu pamoja na utangazaji matokeo.

Katibu huyo alisema polisi na msimamizi mkuu wa jimbo walipoelezwa kuhusu hali hiyo, hakukua na hatua zozote zilizochukuliwa.

Naikara alisema kutokana na hali hiyo, Chama kilijaribu kuongeza idadi ya mawakala ili kukabiliana na vurugu zilizokuwa zikisababishwa na mawakala hao, lakini askari wa jeshi la polisi waliwazuia, hali iliyoonyesha wazi kuwa kulikuwa na njama kati ya polisi na CHADEMA.

Alisema mapema jana asubuhi walipofika katika ofisi za halmashauri ili kusikiliza matokeo, walimkuta mgombea wa CHADEMA ndani ya chumba cha kujumlishia matokeo, lakini walipotaka kuingia, walizuiliwa hali iliyosababisha watumie nguvu.

Naikara alisema baada ya kuingia kwenye chumba hicho kwa nguvu, mgombea huyo wa CHADEMA alianzisha fujo, ikiwa ni pamoja na kuzimwagia maji karatasi za kura.

Kutokana na hali hiyo, msimamizi mkuu wa uchaguzi, ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri, aliwataka wote kutoka nje, ambapo walikubali, lakini walipokuwa wanaelekea nje ya eneo hilo, mgombea huyo wa CHADEMA alibaki nyuma.

Katibu huyo alisema baadaye walimpigia simu mkurugenzi huyo kutaka kujua hali inaendeleaje, lakini aliwajibu kuwa watume wakala mmoja kwa ajili ya kujua kinachoendelea.

“Tulipojibiwa hivyo, tukaamua kwenda pamoja na tulipofika tulimkuta mkurugenzi huyo mlangoni, ambapo alimkabidhi mgombea wa CCM karatasi ya matokeo aliyoyatangaza bila sisi kuwepo,”alisema.

Alisema alishangazwa na kitendo hicho na walipotaka kumuuliza sababu za kutangaza matokeo bila wao kuwepo, alitokea mlango wa nyuma na kutokomea kusikojulikana.

Kufuatia hali hiyo, Naikara alisema Chama pamoja na mgombea wake, wamegomea matokeo hayo na kuamua kukata rufani kuyapinga kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya taratibu muhimu.

Akizungumzia matokeo hayo, mgombea wa CCM alisema hakubaliani nayo kutokana na ukweli kwamba ni ya kupikwa kwa vile hayakuwa na saini yake.

Aliitaja sababu nyingine iliyomfanya kuyakataa matokeo hayo kuwa ni idadi ya kura walizopata wagombea wote na zile zilizoharibika zinazidi idadi ya wapiga kura halali.

Alitaja idadi ya wapigakura halali kuwa ni 40,606, kura halali zilikuwa 39,988 na zilizoharibika 767, wakati mgombea wa CCM alipata kura 19,352, CHADEMA kura 20,076, CUF 307 na ACT kura 253, ambazo zikijumlishwa zinazidi wapigakura halali.

Mapungufu mengine ni kuchelewa kwa masunduku ya kura hata kwa maeneo ya jirani, ambayo yalifika jana saa tano usiku juzi na saa moja asubuhi jana pasipo kuwepo na ulinzi wowote wa polisi.

Alisema masanduku hayo yalionekana yakibebwa na magari ya watu binafsi, ambao ni wafuasi wa CHADEMA na kwamba walitoa taarifa kwa mkurugenzi wa halmashauri, ambaye alipuuzia malalamiko hayo hali iliyoonyesha kuwepo kwa dalili za rushwa.

No comments:

Post a Comment