Friday, 30 October 2015

KINANA: TUNAKWENDAUFANYA KAZI

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye muda wote alionekana mwenye furaha, alisema kazi iliyobaki ni kuunda serikali na kutekeleza ahadi zilizotolewa na wagombea kwa wananchi na zile zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisema ushindi ni mzuri na  imeonyesha dhahiri wananchi wana mapenzi na CCM na pia walivutiwa na ahadi zilizotolewa na Dk. Magufuli.

Akizungumzia kuhusu wapinzani kukataa matokeo, Kinana alisema kazi ya wapinzani ni kupinga maendeleo pamoja na matokeo, hivyo aliwataka kubadilika, kuyakubali matokeo na kumpongeza mshindi.

Kinana alisema CCM iko tayari kupokea na kuchukua mawazo ya wapinzani na kuyafanyia kazi na aliwataka  wana-CCM kujiandaa kufanya kazi.

DUNI AGONGA MWAMBA

Katika hatua nyingine, mgombea mwenza wa CHADEMA, Juma Duni Haji, aliwasili kwenye kituo hicho cha kutangazia matokeo na kuishia nje ya ukumbi, baada ya kuzuiwa na walinzi kwa kuwa hakuwa na kitambulisho maalumu kinachoruhusu watu kuingia ndani.

Akiwa na bahasha iliyofungwa, Duni aliishia kwenye kiti ambapo aliwaambia maofisa kuwa alikuwa anataka kuonana na Jaji Lubuva.

Hata hivyo, alipotakiwa kueleza shida yake ama aeleze ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na kitu gani, alidai ni siri hivyo  alitakiwa kupeleka mzigo huo makao makuu ya NEC, ambapo alitekeleza agizo hilo.

Duni aliondoka katika ukumbi huo kwa gari namba T 754 DDY, ambapo wawakilishi wa CHADEMA waliokuwa wakijumlisha matokeo waliondoka kabla ya kufanya majumuisho ya jumla, baada ya kula nao chakula cha mchana.

Mbali na Duni, mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Lawrence Masha, ambao walikuwa wameambatana na mgombea mwenza huyo,  nao  hawakuruhusiwa kuingia ndani.

VIONGOZI WA DINI WAMPASHA LOWASSA

Wakati ushindi wa Dk. Magufuli ukiamsha shangwe kila kona ya nchi, viongozi wa dini wamemshauri Lowassa kukubali matokeo yaliyotangazwa na NEC.

Ushauri huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Makanisa ya Pentekoste, Askofu Pius Ikongo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya KNCU mjini Moshi.

Alisema amemsikiliza Lowassa katika taarifa yake kwenye vyombo vya habari kuwa hakubaliani na matokeo ya NEC, jambo ambalo si sahihi.

“Atapigana hadi tone la mwisho, hii ina maana asipotangazwa mshindi nchi inaweza kuingia katika machafuko na ndio hivyo sasa Dk. Magufuli ameshatangazwa mshindi,” alisema Askofu.

Alisema kauli hiyo imemshitua na kwamba hakutarajia kutolewa na kiongozi makini kama Lowassa na kuwaasa Watanzania kupuuzia kauli zenye mwelekeo wa kuhatarisha amani.

Naye Askofu Isaya Sizya wa Kanisa la Fire Altar Ministry la jijini Arusha, alisema kila mtu ana utashi wake, lakini kubwa zaidi ni amani ya nchi ambayo ndio bora kuliko kitu kingine.

Tarime yalipuka kwa furaha

Wakazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, wamempongeza Dk. Magufuli kwa kushinda kwa kishindo kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kada na mkereketwa wa CCM wilayani Tarime, Peter Zakaria alitoa mabasi na magari yake kuwabeba wakazi wa mji huo wakizunguka kusherehekea ushindi katika maeneo mbalimbali mjini hapa.

Wakizungumza na gazeti hili  katika viunga vya mji wa  Tarime, Sirari na Nyamongo baada ya kutangazwa kwake na NEC, wakazi hao walisema wamefurahia Dk. Magufuli kushinda mbio za urais na kwamba wakao tayari kwa kazi.

“Magufuli ni mchapa kazi na mwadilifu. Ushindi wake umetufariji sana, tuko tayari kufanya kazi na yeye bega kwa bega,” alisema Zakaria.

No comments:

Post a Comment