Friday, 30 October 2015

HONGERA DK JOHN MAGUFULI KWA USHINDI WA KISHINDO




HATIMAYE Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza matokeo rasmi ya kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25,mwaka huu.

Akitangaza matokeo hayo kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alimtangaza mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Dk. Magufuli ameibuka mshindi baada ya kupata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46, akifuatiliwa na mgombea wa CHADEMA, Edward Lowassa, aliyepata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.93

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Anna Elisha Mghwila ameshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 98,763, sawa na asilimia 0.65, akifuatiwa na Chifu Lutalosa Yemba wa ADC, aliyepata kura 66,049, sawa na asilimia 0.43 na Hashim Rungwe Spunda wa CHAUMA, aliyepata kura 49,256 sawa na asilimia 0.32.

Wagombea wengine walikuwa Lyimo Macmillan Elifati wa TLP aliyepata kura 8, 198, sawa na asilimia 0.05, Kasambala Janken Malik wa NRA, aliyepata kura 8,028, sawa na asilimia 0.05 na Dovutwa Fahmi Nassoro wa UPDP, aliyepata kura 7,785 sawa na asilimia 0.05.

Kutokana na matokeo hayo na kwa mujibu wa madaraka aliyonayo kikatiba, Jaji Lubuva, alimtangaza rasmi Dk.Magufuli kuwa ndiye Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2015/2020. Dk. Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5, mwaka huu.

Mbali na mgombea wa CCM kushinda kiti cha urais, pia Chama kimeshinda majimbo 217 ya uchaguzi kati ya majimbo 264 na hivyo kuwa na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikilinganishwa na wapinzani.

Kwa mujibu wa NEC, uchaguzi wa wabunge katika majimbo mengine saba haukufanyika, sita kutokana na vifo vya wagombea wa vyama vya CCM na CHADEMA vilivyotokea wakati wa kampeni na pia kujitokeza kwa baadhi ya kasoro chache.

Ushindi wa Dk. Magufuli umepokelewa kwa furaha kubwa na viongozi, wanachama na wafuasi wa CCM, hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na upinzani mkali na pia kuwepo kwa changamoto nyingi.

Tunapenda kumpongeza Dk. Magufuli kwa ushindi wake huo, ambao bila shaka umewapa matumaini makubwa wananchi wa Tanzania kutokana na rais huyo mteule kuinadi vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM wakati wote wa mikutano yake ya kampeni.

Kingine kinachowapa Watanzania matumaini hayo ni sera binafsi za rais huyo mteule, mikakati yake katika kufufua viwanda vilivyokufa, kutoa ajira kwa vijana, kupambana na wala rushwa na mafisadi na pia kauli mbiu yake ya ‘Hapa kazi tu’.

Tunatoa mwito kwa viongozi na wafuasi wa vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi huo, kukubaliana na matokeo hayo yaliyotangazwa na NEC, hasa ikizingatiwa kuwa katika mashindano yoyote, kuna kushinda na kushindwa.

Ikumbukwe kuwa uchaguzi ni njia mojawapo ya kuonyesha kukomaa kwa demokrasia katika nchi yoyote na kwamba kinachofuata ni waliochaguliwa kushirikiana katika kuwaletea wananchi maendeleo wanayoyataka.

Wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, ambao wametamka wazi kuwa hawakubaliani na matokeo hayo na walijaribu kuyapinga kwa kuitaka NEC isiendelee kutangaza matokeo ya majimbo yaliyokuwa yamesalia. Hiyo si siasa, ni dalili za viongozi hao kutokubali kushindwa na kutaka kuzusha vurugu zinazoweza kuhatarisha amani.

Kama walivyonukuliwa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Jumuia ya Madola, Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Kamati ya Bunge la Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuia ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), uchaguzi huo ulifanyika mwa amani, utulivu na ulikuwa huru na wa haki.

Nasi tunaungana na waangalizi hao kusema kuwa uchaguzi huo ulikwenda vizuri kuanzia mchakato wa kampeni zake, upigaji kura na hatua ya kuhesabu na kutangaza matokeo, hivyo hakuna sababu za kuutilia shaka.

Kama ni kasoro ama dosari ndogo ndogo zilikuwa za kawaida na zinaweza kurekebishwa katika uchaguzi mkuu ujao, kwa vile hazikuwa na madhara yoyote makubwa yanayoweza kuyafanya matokeo yatiliwe shaka ama kufutwa.

Kwa kuwa uchaguzi umeshamalizika, tunatoa mwito kwa Watanzania kuungana na kuwa kitu kimoja, bila kujali itikadi za kisiasa ili kila mmoja apiganie maendeleo ya mahali alipo. Hii itasaidia kuisukuma serikali kuharakisha maendeleo kwa wananchi na pia kutatua kero zinazowakabili.

Aidha, tunatoa mwito kwa rais mteule kuhakikisha kuwa baada ya kuapishwa, anatekeleza kwa vitendo ahadi zote alizozitoa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali wakati wa kampeni. Bila kufanya hivyo, wananchi watapoteza imani kwake na wanaweza kukiadhibu Chama wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020.

Hongera Dk. Magufuli. Watanzania wana hamu kubwa ya kukuona ukitekeleza kwa vitendo kauli mbiu yako ya ‘Hapa kazi tu’ na pia kupambana na wala rushwa, wabadhirifu wa mali za umma, mafisadi na watendaji wabovu serikalini.

Pia tunaipongeza CCM kwa kuonyesha ukomavu wake wakati wote wa kampeni, ikiwa ni pamoja na kuwanadi wagombea wake kwa kutumia nguvu ya hoja.

Tunaamini kuwa wagombea wote wa CCM waliochaguliwa katika uchaguzi huo, watatekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuzidisha imani ya wananchi kwa Chama. Mungu ibariki  Tanzania.

No comments:

Post a Comment