Saturday 31 October 2015
DK. MAGUFULI: SIKU ZA WANAFIKI ZINAHESABIKA
NA WAANDISHI WETU
RAIS Mteule Dk.John Magufuli, amefunguka na kusema hakuomba nafasi ya urais kwa majaribio na atahakikisha waliokigharimu Chama Cha Mapinduzi, CCM, na serikali kwa ujumla wanaondoka mchana kweupe.
Aidha, amesema wanafiki siku zao zinahesabika kwa kuwa ni bora kukaa na mchawi kuliko mnafi anayekuumiza ukiwa nae ndani.
Dk. Magufuli alishindwa kuficha hisia zake na kueleza duku duku lake kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa aliwakumbatia wanafiki na ndio waliomwangusha.
Aliyasema hayo jana alipozungumza na mamia ya wanachama wa CCM na wananchi waliojitokeza kumpokea katika Ofisi Ndogo za CCM jijini Dar es Salaam mara baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi wa urais na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema ushindi wake ni wa Watanzania wote wenye kuhitaji mabadiliko ya kweli na atahakikisha anatimiza deni kubwa la kuwafanyia wananchi kazi ili watimize matamanio yao ya kupata maendeleo.
“Nina changamoto kubwa ya kufanya kazi ili kutimiza ahadi….mniombee na makamu wangu mama Samia Suluhu Hassan, tutekeleze wajibu wetu kwa kuwa kuna kero nyingi katika jamii kwenye kupata huduma ipasavyo,”alisema.
Aliongeza kuwa ili kufikia malengo, ushirikiano wa wananchi ni muhimu kutoka vyama vyote na maandamano katui hayapaswi kupewa nafasi ili kutoa nafasi ya kufanya kazi.
Dk. Magufuli alimshukuru Rais Kikwete kwa kuiacha nchi kwente mikono salama na kuwa na moyo wa pekee kwani wapo marais wanaong’ang’ania madaraka na kufikia hata hatua ya kubadilisha katiba ili waendelee kuongoza.
Alisema CCM imepata kazi kubwa kwa kuwa wapo vigogo ndani ya chama wanakiumiza.
“Msema kweli ni mpenzi wa Mungu, nisipolisema hili litaniumiza na kupata kiungulia…Chama kimepata wakati mgumu na waliotuumiza wamo ndani ya Chama kuna maadui wengi, wajisafishe wenyewe wafanye kazi heri mchawi kuliko mnafki,”alisema.
Alisema tiba ya mnafiki ukimgundua leo mtimue kesho.
Dk. Magufuli alisema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana ni mkweli na ametumia nguvu zake kujenga CCM na kupambana na maadui wa ndani na nje.
Dk. Magufuli alisema ana kazi kubwa na ngumu ya kusafisha Chama na serikali na anatambua kuwa atagusa maslahi ya watu, lakini ili jipu lipone ni lazima damu itoke na sasa uchaguzi umekwisha watu wafanye kazi.
Alisema watendaji wasiotimiza wajibu wao hawatakuwa na msamaha na kuwa wataondoka tu.
Aidha aliahidi wananchi kuwa ataanza kufanya kazi siku hiyo hiyo atakayoapishwa.
Katika hatua nyingine, viunga vya katikati ya jiji la Dar es Salaam, vilizizima kwa furaha, wakati maelfu ya wananchi na wapenzi wa CCM walipofika kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, kumpokea Rais mteule, Dk. John Magufuli, baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Licha ya kunyesha kwa mvua kubwa, wananchi hao hawakusita kuendelea kumsubiri Dk. Magufuli, tangu saa 12 asubuhi, huku wakiwa wamebeba mabango na kuimba nyimbo mbalimbali za Chama.
Wananchi hao walianza kudeki barabara na kupiga “push up” kuashiria kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” ambayo Dk. Magufuli, amekuwa akiisisitiza kwenye mikutano yake ya kampeni, wakati akiwania nafasi hiyo.
Kama ilivyo kawaida ya wanachama na wapenzi wa CCM, licha ya kujawa na furaha isiyokuwa na kifani, wakati wote walimsubiri rais mteule huku wakisherehekea kwa amani na utulivu.
Haikuwa kazi rahisi kwa wananchi hao kuficha hisia zao za furaha, wakati Dk. Magufuli, akitanguliwa kidogo na Rais Jakaya Kikwete, walipowasili kwenye ofisi hizo saa 5: 47 asubuhi.
Wakiongozwa na bendi ya Tanzania One Theater (TOT), waliimba wimbo maalum wa ushindi kumpokea rais mteule, ambaye wakati wote alikuwa mwenye furaha na uso wa bashasha.
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipokuwa akimkaribisha Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kuzungumza na mamia ya wanachama wa CCM, wapenzi, wakereketwa na wananchi, alisema Watanzania wamefanya chaguo sahihi kuiamini CCM kuongoza awamu ya tano ya serikali chini ya Dk. John Magufuli.
Alisema wamefanya kazi kubwa ya kukipa Chama kura nyingi zilizomfanya Dk. Magufuli na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, kuibuka kidedea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu uliokuwa na changamoto nyingi.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete, alisema ni wajibu wa Watanzania kujipongeza kwa ushindi walioupata kumpitisha Dk. Magufuli kuwa Rais mteule wa awamu ya tano wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kazi kubwa imefanyika kupambana na vyama vya upinzani ambavyo kwa wakati huu baadhi yao vinaendelea kutapatapa baada ya kushindwa kisera kwenye mbio za kuelekea Ikulu.
“Tumewashinda kwenye matokeo ndio sababu wanatapatapa, ahsanteni kwa kuipa ridhaa CCM kuiongoza awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sina uhakika na hatima yao baada ya matokeo haya kwa sababu walikuwa wanachonga sana. Mikutano yao imejaa viroba, kwetu hatuna vibora hatuwapi watu viroba, hatujui hata vinauzwa wapi… lakini mwisho wake ndio huo sio riziki; sisi tunazidi kuwaombea kheri,” alisema Rais Kikwete.
Pia aliongeza: “Leo ninatamani kuwashukuru tu Watanzania na wana-CCM kwa umoja wenu tangu kipindi cha uteuzi wa Dk. Magufuli, ambao baada ya kuwaacha baadhi kati ya wale makada 38, wengine walijiengua na kukihama kabisa chama kutokana na kutoridhika.
“Waliamini kabisa kuwa CCM itameguka vipande vipande, lakini tulikuwa imara na niwaeleze wajue kuwa hakuna wakati wana CCM wanakuwa imara na wamoja kama wakati ambao mtu anajaribu kutaka kuharibu uhai wa chama.”
Rais Kikwete alisema wanachama wa CCM ni silaha kubwa ya ushindi ya wakati wote dhidi ya wapinzani kwa sababu wanajua muda upi wa kuungana kujenga Chama na muda upi wa kugeukia shughuli za kiuchumi kujenga taifa.
Alisema amefurahi kuiongoza Tanzania kwa miaka 10 ya mafanikio ambayo hana shaka yataendelezwa kwa kasi zaidi na Rais mteule Dk. Magufuli na msaidizi wake Samia Suluhu Hassan.
Aliongeza kuwa ndani ya siku tano kuanzia jana, atakabidhi madaraka kwa Dk. Magufuli ambaye anatarajiwa kuapishwa Novemba 5, mwaka huu, kisha kuendelea na majukumu mengine.
“Ninashukuru nimepata mrithi wangu, ndani ya siku tano kuanzia leo (jana) nitakabidhi madaraka kwa Rais mteule, Dk. Magufuli, tingatinga, ambaye kasi yake si mchezo na mimi nitaenda Msoga kulima,” alisema.
Katika hotuba yake fupi, Kikwete alisema Katibu Mkuu Abdulrahaman Kinana amekuwa na mchango mkubwa kwenye ushindi wa CCM kwa mwaka huu kutokana na uchapakazi wake uliotukuka kwa chama ili kuhakikisha ushindi.
Alisema Kinana ni kiongozi wa mfano kutokana na uwezo wake wa kubuni vitu vipya kwa wakati husika ili kurejesha heshima ya Chama kwa Watanzania na wana CCM.
“Ni kiongozi wa mfano, alikuwa tayari muda wowote tuliokuwa tukimhitaji, nilikuwa nikimpigia wakati wowote… yeye anapokea simu na kutekeleza wajibu wake kama mtendaji mkuu wa chama chetu, ahsante sana Kinana,” alisema.
Pia, Rais Kikwete alisema Mjumbe wa Kamati ya Ushindi, January Makamba, amefanya kazi kubwa kufanikisha kampeni za mwaka huu kwa uwezo wake wa kuwasiliana na watu mbalimbali, wakiwemo wasanii ambao walihakikisha wanaipigania kampeni CCM bila kuchoka.
Alisema Makamba ndiye aliyekuwa akituma ujumbe mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na simu zenye kueleza mafanikio yaliyofanywa na CCM kwa wakati wote madarakani na kueleza umma kwa nini wanapaswa kukichagua tena Chama kushika dola.
Alitumia fursa hiyo kupongeza vyombo vya habari na hasa kituo cha televisheni cha Star cha jijini Mwanza.
Rais Kikwete alisema kituo hicho kimetoa mchango mkubwa kwenye kampeni zilizositishwa Oktoba 24, mwaka huu, ambapo kupitia matangazo yao ya moja kwa moja ya mikutano ya kampeni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, Watanzania walijua fungu gani walichague.
Alisema wanastahili pongezi kwa mchango huo kwa Chama na Watanzania.
Rais Kikwete alimsisitiza Dk. Magufuli asiusahau mchango wa makada hao kwenye uongozo wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment