Saturday 31 October 2015

NEC YAMKABIDHI CHETI MAGUFULI, NAPE ATAKA MATAIFA YA KIGENI KUACHA SHINIKIZO

MAKAMU wa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, akionyesha cheti walichokabidhiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu. Kushoto ni Rais Mteule, Dk. John Magufuli.
RAIS Jakaya Kikwete akitazama cheti alichokabidhiwa Rais Mteule, Dk. John Magufuli
DK. Magufuli akimuonyesha cheti chake aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwila.
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi akifurahia jambo la Spika wa Bunge, Anne Makinda na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Pius Msekwa

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu, Damian Lubuva, amemkabidhi cheti Rais Mteule wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan.

Jaji Lubuva alikabidhi cheti hicho jana, saa 4.56, asubuhi, katika ukumbi wa Diamond Jubilee mjini Dar es Salaam.

Kabla ya kukabidhi cheti hicho, Jaji Lubuva, alisema uchaguzi mkuu, uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, NEC ilishirikisha mawakala wa vyama vyote ambao walitia saini karatasi za matokeo ya uchaguzi huo.

Alisema vyama sita vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo, vilitia saini na kukubali matokeo hayo ambapo vyama viwili havikutia saini.

Jaji Lubuva alisema kwa mujibu wa sheria, NEC ina mamlaka ya kumtangaza mshindi hata kama mawakala hawakutia saini.

Alisema mwaka 2010, wapiga kura milioni 8.3, walipiga kura na kwamba uchaguzi wa mwaka huu, waliopiga kura walikuwa milioni 15.5.

Jaji Lubuva alivishukuru vyama vya siasa, vilivyoshiriki uchaguazi huo na kwamba vilitoa ushirikiano mkubwa kwa NEC.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, alisema kuna majimbo ya uchaguzi 264, kata 3,957, ambazo zilishiriki uchaguzi.

Hata hivyo, alisema majimbo 256, yalishiriki uchaguzi, manane hayakushiriki, kati ya hayo sita wagombea wake walifariki dunia na mawili uchaguzi uliahirishwa kwa sababu mbalimbali.

Alisema kata 34, hazikufanya uchaguzi ambapo kata nane, wagombea wake walifariki na kwamba 26, hazikufanya uchaguzi kwa sababu mbalimbali.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa mgombea urais wa chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, alisema anakubali matokeo ya uchaguzi  ambao Dk. Magufuli amekuwa rais.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, wagombea wote walikuwa wakizungumzia mabadiliko, hivyo ana amini kuwa Dk. Magufuli, atalisimamia hilo.

Anna ambaye alikuwa mgombea pekee mwanamke, alisema wanataka katiba mpya inayotokana na wananchi na kwamba kuwe na usawa baina ya wanawake na wanaume.

Alisema wanataka kuona fahari ya Watanzania inadumishwa siku zote ambapo alitumia fursa hiyo kumkabidhi Dk. Magufuli, katiba ya chama chao.

Baada ya Dk. Magufuli na Samia, kukabidhiwa hati za kuchaguliwa, walimuonyesha Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na viongozi wengine waliokuwa meza kuu.

Aidha, aliwaonyesha viongozi mbalimbali wa dini, mabalozi, waangalizi wa uchaguzi, wananchi na wana-CCM, waliohudhuria hafla hiyo ambao walikuwa na furaha muda wote.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wagombea urais, akiwemo Dovutwa Fahmi (UPDP), Chief Lutalosa Yembe (ADC), Kasambala Malik (NRA) na Lyimo Elifatio (TLP).

Mbali na hao, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Phillip Mangula, mke wa rais, Mama Salma Kikwete, mke wa rais mteule, Janeth Magufuli na viongozi wengine.

Wananchi na wana-CCM waliohudhuria hafla hiyo, walionekana kuwa na furaha ambapo muda wote walikuwa wakishereheka huku wakitumbuizwa na brass band ya polisi.

CCM kimeyataka mataifa makubwa duniani kujifunza  kuheshimu demokrasia za nchi nyingine ikiwemo Tanzania hata kama yanatoa misaada ya kimaendeleo.

Kauli hiyo inakuja baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi wa Rais na wawakilishi baada ya kutokea dosari mbalimbali.

Miongoni mwa dosari hizo ni kuwepo kwa kura nyingi kwa upande wa Pemba tofauti na idadi ya watu waliojiandikisha katika daraftari, hivyo kusababisha  kufuta uchaguzi huo.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipozungumza na gazeti hili katika hafla ya kukabidhiwa kwa cheti cha ushindi kwa Rais Mteule wa Tanzania, Dk. John Magufuli na Makamu mteule wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Nape alisema mataifa hayo hayapaswi kutoa shinikizo kwa sababu Tanzania ni nchi huru na inaendeshwa kwa mujibu wa katiba na inafanya demokrasia kwa muda mrefu.

Alisema ZEC ndiyo ina mamlaka juu ya uchaguzi wa Zanzibar, hivyo alitaka maamuzi waliyatoa yaheshimiwe na kusiwepo kwa mashinikizo.

“Wasituingilie na nawaomba Watanzania tuendelee kulinda uhuru na tusikubali kushinikizwa kufanya mambo yaliyo nje ya utaratibu wetu,” alisema Nape.

Katika hatua nyingine, Nape alisema uchaguzi umeisha hivyo aliwaomba wananchi kukataa na kuwalaani wote wanaoendeleza mambo ya uchaguzi badala ya kuhamasishana kufanya kazi.

Alisema atakapofika bungeni atashauri itungwe sheria ya kukomesha nongwa za uchaguzi kwa sababu zinakwamisha utendaji wa kazi.

Wakati huo huo, Nape aliwashukuru wananchi wa jimbo la Mtama kwa imani kubwa waliyompa kwa kumchagua kuwa mbunge wao ambapo aliwaahidi kuwatumikia na kwamba atafanya kazi waliyomtuma.

Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi alisema anaishukuru CCM kwa heshima kubwa waliyoitoa kwa wanawake ambapo Samia anakuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke.

Hata hivyo, aliwaomba wananchi kutulia na kutoruhusu uvunjifu wa amani na badala yake wampe ushirikiano Dk. Magufuli na Samia ili waweze kutekeleza majukumu yao.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka  Hamidu Shaka, alisema Watanzania wanatakiwa kuimarisha umoja na mshikamani wao.

Alisema vijana tayari wamepata mkombozi atakayeenda sambamba na kasi ya maendeleo wanayoitaka hivyo wajipange katika vikundi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zilizoandaliwa kwa ajili yao.

Katika hatua nyingine, alitoa rai kwa mashirika ya ndani na nje kuheshimu demokrasia kwa sababu Tanzania ni taifa huru na lina utaratibu na sheria zake.

Waziri wa Katiba na Sheria,  Asha-Rose Migiro alisema amefurahi kwa ushindi wa Dk Magufuli  kwa sababu taifa limepata kiongozi safi na mzalendo wa kweli.

Kuhusu baadhi ya mataifa kutoa shinikizo juu ya uamuzi wa ZEC, alisema Tanzania ina katiba ambayo ndiyo inayoiongoza, hivyo kilichokubaliwa Zanzibar ni kwa mujibu wa katiba.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Asumpter Mshama,  alisema amefurahishwa na maamuzi sahihi yaliyofanywa na Watanzania kwa kumchagua Dk. Magufuli, hivyo aliwaomba wote bila kujali itikadi za vyama waungane na wafanye kazi na waendelee kuboresha amani.

Kwa upande wake, Christopher Ole Sendeka, ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya CCM, alisema ushindi wa Chama umeonyesha namna ambavyo wananchi wanatambua walikotoka.

Pia alisema ushindi huo ni ishara na uthibitisho kuwa Mwenyezi Mungu ana nia njema na Tanzania, hivyo kuaamua kuwaletea kiongozi ambaye atakidhi kiu yao ya maendeleo.

Kuhusu mataifa ambayo yanataka kuingilia uamuzi wa ZEC alisema Tanzania ni taifa huru, hivyo iachwe itekeleze majukumu yake na hakuna mizingwe katika hilo.

No comments:

Post a Comment