Saturday 31 October 2015

UKAWA YAMETIMIA, LOWASSA AJIPANGA KURUDI MONDULI


Na Joseph Kulangwa

HAPANA ubishi tena kwamba Dk. John Magufuli wa CCM ndiye Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania baada ya kumtimulia vumbi mpinzani wake mkuu, Edward Lowassa wa CHADEMA kwa kivuli cha Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA).

Dk. Magufuli ameibuka mshindi kiwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 dhidi ya 6,072,848 za hasimu wake kisiasa, Edward Lowassa sawa na asilimia 39.93 wa Chadema (Ukawa).

Si siri pia, kwamba hivi sasa kuna watu ndani ya vyama vya upinzani wanatafakari ni upi mustakabali wao na wa vyama vyao baada ya kile walichokuwa wakikitafuta kwa muda mrefu hatimaye kuwaponyoka.
Wakati wana CCM nchini na duniani kote wakisherehekea kwa kutoa Rais kwa mara nyingine, wafuasi wa UKAWA wanashika tama na kujiuliza nini kimetokea na upi utakuwa mustakabali wao kisiasa.

Rais Mteule Magufuli, anabungua bongo kuona atakuja na Baraza lipi na la aina gani la mawaziri ili kukidhi kiu ya Watanzania, huku pia akizingatia kuwa ana mzigo wa kuhakikisha anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama chake kwa mujibu wa ahadi alizotoa akikampeni.

Hilo likiendelea, Rais wa Awamu ya Nne anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete ni dhahiri anashusha pumzi na kujipongeza kuwa amekifikisha chombo alichokuwa akikiongoza bandarini salama, licha ya hisia mbalimbali zilizokuwapo kuwa hakitafika salama.

Rais Kikwete anaiacha nchi ikiwa salama na CCM ikiwa imara baada ya misukosuko iliyoikumba kutokabna na kinyang’anyiro cha urais ambapo ilishuhudia hata baadhi ya waasisi wake wakiikimbia kwenda walikodhani kuna asali, maziwa na mana.

Hivi sasa kundi la kina Freeman Mbowe chini ya Lowassa linajitahidi linavyoweza kushawishi wafuasi wake, waamini kuwa ushindi aliopata Dk. Magufuli ni batili na kwamba mshindi alistahili kuwa mgombea wake, Lowassa.
Kukataa kutambua matokeo kama inavyoelekea kuwa kwa kundi hilo, hakuna tija wala siha kwa taifa hili zaidi ya kulitakia mabaya, kwani hakuna njia zaidi ya kufanya fujo na kuliingiza kwenye maafa na hivyo kutoka kwenye njia ya kujiletea maendeleo.

Ni dhahiri sasa UKAWA imechanganyikiwa, Lowassa anajiandaa kurudi Monduli kuchunga mifugo yake kama alivyokwishaahidi kuwa akishindwa atafanya hivyo; Frederick Sumaye ambaye alikuwa akitazamiwa kuwania uspika, pengine anaweza kuendelea na ndoto yake ambayo bila shaka kwa wingi wa wabunge wa CCM hatafanikiwa.

James Mbatia wa NCCR-Mageuzi amebaki jeshi la mtu mmoja ni Mwenyekiti wa Chama anayekumbana na upinzani wa ndani lakini pia ni mbunge pekee wa chama hicho; amekishusha chama chake kilichokuwa na wabunge bungeni.

Baada ya Lowassa kurudi kijijini na kustaafu siasa kwa amani yenye machungu, Mbowe anabaki na chama legelege kisicho na viongozi imara kama alivyokuwa Katibu Mkuu wake, Dk .Willbrod Slaa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe ambaye nuru ya ACT-Wazalendo inamwangazia.

CUF nayo kwa upande wake, inabaki ikijiuliza itafanya nini bila mikono ya Profesa Ibrahim Lipumba aliyejivua wadhifa wa uenyekiti na Juma Duni Haji ambaye alihamia CHADEMA  punde tu baada ya Lowassa kutangazwa mgombea urais wa chama hicho.

Ni kweli kuwa kama si urais, Duni asingehamia CHADEMA na hivyo hapo si mahala pake na hataweza kutoa mchango mkubwa kuijenga CHADEMA ambayo kwa kiasi kikubwa ngome yake iko bara tena katika baadhi ya kanda.

Kwa hakika mambo yalivyo ndani ya UKAWA yanatia ukiwa, kwa sababu kile kilichokuwa kinatarajiwa na jinsi viongozi hawa walivyokuwa wamejipanga, kinyume chake ni sintofahamu inayohitaji mganga bingwa wa kuiondoa kwa sasa.

Kinachobaki ni kwa wabunge wa UKAWA waliobahatika kuchaguliwa na wananchi kusimama wao kama wao kutetea nafsi zao kwa maana ya majimbo yao, wakijiandaa kujitetea katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Tatizo ni kubwa kwa waliokuwa wakitarajia kuishi kwa hisani ya ‘Rais’ Lowassa, hawa ni wale ‘marafiki’ zake waliomchangia lakini pia waliokuwa na mahaba naye waliohama CCM na kumfuata UKAWA akiwemo Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru.

No comments:

Post a Comment