Saturday, 31 October 2015

RAIS MAGUFULI AMEWATANGULIA GALILAYA


NA FREDERICK SANGA

HATIMAYE Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemtangaza Dk. John Magufuli kuwa rais wa tano wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Magufuli amepata ushindi wa asilimia 58.46A akimuacha kwa mbali mpinzani wake mkubwa Edward Lowassa aliyepata asilimia 39.93 huku wagombea wa vyama vingine wakigawana asilimia zilizosalia.

Wakati tunampongeza Rais Mteule Dk. Magufuli kwa ushindi mnono, sina budi kuipongeza Kamati ya Ushindi ya CCM iliyokuwa inaongozwa na Mjumbe wa kamati hiyo, January Makamba.

Kamati hiyo imefanya kazi kubwa ambayo imechangia kupata ushindi huu wa kishindo. Makamba amekuwa msemaji mzuri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati wote wa kampeni na hata wakati wa upigaji kura hadi  kutangazwa kwa matokeo.

Kamati hiyo imedhihirisha pasi na shaka kuwa siasa ni sayansi na sanaa. Kwa kadri mjumbe huyo alivyokuwa akitoa tathmini na maendeleo ya kampeni wananchi walio wengi walipata imani kubwa na CCM na hatimaye kukipigia kura Chama.
Makamba ametumia vizuri vyombo vya habari kutoa taarifa kila ilipohitajika na kwa usahihi mkubwa na ameandika makala mbalimbali zilizoonyesha mikakati ya kisayansi iliyopelekea ushindi.

Wakati tukimpongeza Rais Dk. Magufuli na Kamati ya ushindi, sina budi pia kuwapongeza wananchi wote wa Tanzania kuwa na imani na CCM.

 Watanzania safari hii wameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa kwani wamepiga kura kwa utulivu mkubwa na kwa maamuzi sahihi na yenye tija kwa taifa.

Ni dhahiri Watanzania walizisikiliza vyema sera za vyama vyote na hatimaye wakapekecha na kuona upi ni mchele na zipi ni pumba na Dk. Magufuli alikuwa ni mgombea pekee aliyeweza kunadi sera za Chama kwa umakini wa hali ya juu.

Ametumia taaluma yake ya ualimu kufafanua sera na kueleweka vizuri. Dk.Magufuli alionyesha uwezo mkubwa wa kujenga hoja kwa muda mrefu kati ya dakika 50 hadi dakika 60. Hakuna mgombea yeyote aliyeweza kuvunja rekodi hiyo.

 Waandishi wa habari nao wametoa mchango mkubwa kwa ushindi wa Dk.Magufuli, walikuwa wakiandika makala mbalimbali  za kuelimisha jamii mazuri ya CCM na Magufuli.

Pia walisaidia kufafanua vizuri sera za CCM kupitia magazeti ya Chama ya UHURU na MZALENDO.Lakini pia kwa upekee kabisa natoa shukrani za dhati kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhuru Publications LTD, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo, Uhuru Wikiendi na Burudani, Radhamani Mkoma.

Amekuwa ni kiungo muhimu katika kuhakikisha makala zote zinazowafikia zinapewa nafasi gazetini.Aksanteni kwa kuheshimu mawazo ya wanaCCM kupitia taaluma zao za habari.

Matarajio makubwa ya wananchi ni kuona utekelezwaji wa sera za CCM, ambazo sina shaka na Dk.Magufuli ambaye amejipambanua kama mpambanaji mkubwa wa ufisadi na mafisadi, ameahidi kuyasimamia yale yote aliyoyaahidi kwa nguvu zake zote

Mara nyingi amekuwa akisika katika kampeni zake akisisitiza kwamba yeye ni mkweli na atakuwa mkweli daima hatakubali kupindishwa na mtu yeyote pale anapoona haki haitendeki.

Pamoja na ahadi nyingine alizoahidi DK. Magufuli, wananchi wanasubiri kwa hamu vita dhidi ya ufisadi na mafisadi, pamoja na kutatua tatizo la ajira kwa vijana.

Kama alivyoahidi wakati wa kampeni aliahidi kuanzisha Mahakama Maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi. Ni imani yangu kuwa Dk. Magufuli atalitekeleza hilo kama alivyoahidi kwani mafisadi wamekuwa wakijenga taswira mbaya kwa Chama na serikali kwa ujumla.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu amtie nguvu Dk. Magufuli katika kulisimamia hilo. Hali kadhalika,wananchi wengi hasa vijana wanasubiri kuona tatizo lao la ajira likishughulikiwa kama  alivyoahidi wakati wa kampeni.

Katika kulishughulikia tatizo la ajira kwa vijana aliahidi kujenga viwanda, kuvutia wawekezaji ili wajenge viwanda vikubwa na vidogo, hasa sehemu zile ambazo malighafi inapatikana kwa wingi.

Pia aliwataka wawekezaji ambao wamevinunua viwanda bila kuviendeleza wajiandae kuvirudisha ili wapewe wale wenye uwezo wa kuviendeleza.

Tunatarajia Dk.Magufuli atapewa ushirikiano katika kutekeleza ahadi hizi, wapo waliokuwa wanabeza kampeni za CCM kwa kupitia mgombea wake waliwaahidi Watanzania ushindi.

CCM ilijiamini kushinda kwa sababu ya mikakati mizuri na ya kisayansi ambayo ilishaanza kuonyesha ushindi hata kabla ya kupiga kura.Msomaji wa Makala hii binadamu hatuna utamaduni wa kuaminiana hata pale ukweli unapojidhihirisha.

Tunapenda kupinga kila kitu hata kama hatuna ushahidi, hilo halinipi tabu  kwa sababu Mwana wa Mungu Yesu kristo alikuwa haaminiwi na wanafunzi wake kila alipokuwa anazungumzia kuteswa, kufa na kufufuka kwake.

Kabla Yesu hajakamatwa na wayahudi alisikika akiwaambia wanafunzi wake “Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu, kwa kuwa imeandikwa,nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.

Lakini baada ya kufufuka kwangu,nitawatangulia kwenda Galilaya.”(Math 26; 31-32), maneno hayo hayakueleweka vizuri kwa wanafunzi wa Yesu, kwani ilikuwa ni ajabu kwa mtu ambaye alisema atakufa,halafu mtu huyo aje tena aonekane Galilaya?

Baada ya Yesu kusulibiwa hadi kufa, maandiko yanasema alifufuka siku ya tatu.Tunaambiwa Mariam Magdalena na Mariamu wa pili walikwenda kulitazama kaburi.

Hawakumkuta! Malaika akawaambia hayupo hapa amefufuka kama alivyosema .Nanyi nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake amefufuka na amewatangulia Galilaya ndiko mtakakomwona.

Wanawake wale wakaenda kuwaambia wanafunzi wa Yesu yote waliyoyaona na wakawaambia wanafunzi wakaenda Galilaya.

Wanafunzi wale walipokwenda Galilaya walimkuta Yesu huko ambako aliwaambia “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani,basi enendeni ,mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi , mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi, na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Bila shaka Rais Mteule Magufuli sasa amewatangulia Galilaya, kama Yesu alivyowaambia wanafunzi wake hapo Galilaya kwamba amepewa mamlaka yote duniani na mbinguni.

Ndipo Dk. Magufuli anavyoweza kusema kwani amepewa mamlaka yote bara na visiwani na anawaagiza (kupitia mawaziri wake) mkawafanye Watanzania wote kuwa kitu kimoja mkihubiri amani, upendo na mshikamano, kuwafundisha kuzishika sheria za nchi na Tazama mimi (Magufuli) nipo nanyi siku zote hadi uchaguzi wa 2020.

Wale wanafunzi ambao hawakumuelewa Yesu alipowaambia anatawatangulia Galilaya, walikuja kumwelewa walipomkuta huko na kuwaambia amepewa mamlaka, hali kadhalika watu ambao hawakumuelewa Magufuli alipokuwa akisema atatekeleza sera za CCM akiingia Ikulu.

Hapana shaka sasa  wamemuelewa kwamba amepewa mamlaka yote kisheria bara na visiwani kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. HONGERA MAGUFULI, HONGERA CCM.
 fredysanga@ymail.com 0713218219

No comments:

Post a Comment