Sunday, 1 November 2015

UVCCM YATOA TAMKO KALI


TAARIFA ILIYOTOLEWA NA UMOJA WA VIJANA WA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 31 OKTOBA 2015 MAKAO MAKUU YA UVCCM DAR ES SALAAM


Ndugu Waandishi wa Habari,
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi unachukua nafasi hii kukipongeza kwa dhati Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyekuwa mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais mteule Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea mwenza wake Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kupata ushindi wa kidemokrasia wa kishindo kwa kupata asilimia 58.46%.
Ushindi huo ni alama na kielelezo cha kuendelea kukubalika kwa CCM mbele ya Watanzania walio wengi kutokana na Sera zake, Mipango yake na mikakati ya kuwatumikia wananchi, kulinda amani, utulivu na kuendeleza Umoja wa Kitaifa nchini.
Ndugu waandishi wa habari,
Kwa upande mwingine tumelazimika kuwaita hapa leo kuelezea masuala muhimu kadhaa  yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015.
Kama ilivyotolewa taarifa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha,  kwamba Uchaguzi wa Zanzibar kwa sehemu kubwa ulikumbwa na kasoro nyingi za kimsingi ambazo zimesababisha Tume kufuta matokeo kwa  nafasi za Urais, Wawakilishi na Madiwani.
Ndugu waandishi wa habari,
UVCCM tumefanya tathmini ya haraka na kina ili kujua kiini cha tatizo hilo  ikiwemo  kukusanya taarifa toka vyanzo mbalimbali ambapo tumebaini na kugundua madhaifu kadhaa yaliyojitokeza katika hatua za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa upande wa Zanzibar.
Tumepata wasiwasi wa suala zima la namna zabuni ya karatasi za kupigia kura ilivyotangazwa na kumpata mzabuni ambae alipewa kazi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Ni ukweli usiopingika kwamba ZEC ilizidiwa nguvu na wanasiasa wa Chama cha Upinzani cha CUF ambao kwa kiasi fulani wameshinikiza Tume ya Uchaguzi kwa namna moja au nyingine kuikubali Kampuni ya ya Afrika Kusini ambayo sifa zake zinafahamika kuwa ina matatizo.
UVCCM tuna mashaka na kampuni hiyo iliyopewa kazi ya kuchapisha vifaa vya Uchaguzi ambayo kumbukumbu zinaonyesha  iliwahi kuomba kazi ya kutayarisha vifaa kama hivyo katika uchaguzi mkuu wa  mwaka 2005 na kupewa, lakini SMZ baada ya kugundua kampuni hiyo ina matatizo,  ilivunja mkataba na karatasi za kura zilichapishwa hapa hapa nchini.


Kampuni hii inalalamikiwa kuwa chanzo cha kuvurugika kwa chaguzi mbalimbali katika nchi za Afrika ikiwemo  Cameroon, Benin, Ivory Coast  na baadhi ya nchi za Latini Amerika. UVCCM  tumeshangazwa sana kuona ZEC wakiikubali Kampuni ambayo tayari SMZ mwaka 2005 waliikataa na  kuvunja nayo mkataba.
Kampuni hii inasemekana kwamba imekuwa  inashirikiana na vyama vya upinzani hasa katika nchi za Afrika chini ya mkakati wa kuvisaidia kushinda Uchaguzi.
Pia tumepata  mashaka na watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ama walizembea au walikuwa sehemu ya njama za kutaka kuvuruga uchaguzi. Kwa nini tunasema hivyo? Ni kwa sababu watendaji wa Tume ya Uchaguzi wanaifahamu vyema Kampuni hii, matatizo yake, lakini wameshindwa kuishauri Serikali na matokeo yake kuiingiza nchi katika hasara na mkanganyiko wa kisiasa.
Tunawataka watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kujipima kama wanatosha kuendelea kuwa na sifa ya kuwa Watendaji wa Tume hii sambamba na Makamishna wao ambao nao hawakujituma zaidi kujiridhisha na utendaji kazi wa Kampuni hiyo kwa kuzingatia taarifa za nyuma za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hasa pale ilipovunja Mkataba.
Kwa mwenendo huo na mtazamo halisia  ni wazi kuwa Chama cha CUF kimehusika na njama hizi za wizi wa kura na ndio maana Katibu Mkuu wake  Seif Shariff Hamad akaamua kukiuka taratibu na kajitangazia ushindi kinyume na Katiba na Sheria za nchi wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea katika majimbo ya Pemba na Unguja. Ni kituko na mshangao kuona  vyombo  vya dola vikimtazama macho mgombea huyo aliyefanya kosa la jinai bila ya kumchukulia hatua za kisheria na kumfikisha kwenye mikono ya sheria.
Umoja wa Vijana wa CCM tunaitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Kuunda Tume huru itakayochunguza kwa kina na undani wa kadhia hii ikiwemo suala zima la namna ilivyoendeshwa zabuni hadi kufikia kupatikana mzabuni na taarifa yake itolewe kwa umma.
Ndugu waandishi wa habari,
Tumekuwa tukisema  mara kadhaa Chama cha CUF ni chama ambacho kimezoea kuwahamasisha wafuasi wao kufanya vurugu, ghilba,  ubaguzi na masuala mengine ambayo hayaendani na kanuni za kidemokasia.
Katika kuyathibitisha haya, wakati wa kazi ya kupigakura na kuhesabu kura huko Kisiwani Pemba, wafuasi wa CUF wakiwa na jazba wamevamia vituo vya kupigia kura kinyume cha sheria na kuanza kuwashambulia kwa mapanga Mawakala wa Chama cha Mapinduzi na kuwatoa nje, huku wengi wao wakijeruhiwa vibaya.
Wafuasi hao wa CUF wakiwa katika makundi, wameyafanya hayo katika Vituo vya Majimbo ya Tumbe, Micheweni na Konde katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo Mawakala wa CCM wamewapiga na kuwajeruhi na kusababisha kusimamishwa kwa kazi za kuhesabu kura.
Hadi sasa Mawakala wetu hali zao sio nzuri bado wapo hospitalini wakiendelea kupatiwa matibabu. Tumekuwa tukijiuliza inakuwaje Pemba CUF hawataki vyama vyengine kushiriki Uchaguzi kwa kuwafanyia vitendo vya kuwapiga, kuwabagua, kuwabughudhi wakati wao wanashiriki katika kila uchaguzi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Ndugu waandishi wa habari,
Haikuishia katika Majimbo hayo tu, bali uvunjaji wa sheria uliendelea katika sehemu mbalimbali za huko Pemba ambapo wafuasi wa CUF waliokuwa wamekaa pembezoni mwa barabara karibu na Vituo vya Makangale, Kisiwani kwa binti Abeid, Chonga, Mtambwe, Wete, Kojani, Mchangamdogo wafuasi hao wa CUF waliwazuia wana CCM wasiende kupigakura.
Mbali na kufanya hivyo, pia katika huduma  za usafiri wafanyakazi wa gari za abiria za kutoka Wete kwenda Gando, Konde-Wete, Chake – Wete kupitia njia kongwe waliwashusha wana CCM  na huku katika vituo vyengine vya kupanda abiria wakiwakataa wana CCM wasipande magari yao
Hivi wanataka kutuambia kuwa CCM na vyama vyengine nje ya CUF havina haki ya kushiriki katika Siasa Kisiwani Pemba? Ubaguzi huu haukubaliki na tunawaomba wapenda demokrasia wote na Jumuiya za Kimataifa kuchukia vitendo vya kibaguzi na kihuni vinavyofanywa na wafuasi wa CUF kule Pemba.
Ndugu waandishi wa habari
Tangu siku ya Jumatatu wafuasi wa CUF kule Pemba wanachanganya maji na dawa ya kusafishia chooni au kwenye masinki ya kuoshea vyombo wanawamwagia wafuasi wa CCM ama katika makazi yao au usiku wakiwa wamelala wanawamwagia maji hayo ambayo yanawaletea madhara ya kuwashwa mwilini.
Ni dhahiri kuwa Chama cha CUF hakipati kura nyingi kule Pemba kwa ridhaa ya wapigakura, bali ni kwa kuwashurutisha wapigakura , kutoa vitisho na hata katika baadhi ya Majimbo wanawake wametishiwa na waume zao wasipopiga kura  CUF watapewa talaka.
Hali kama hiyo pia imejitokeza katika Shehia za Kijini na Potoa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo wanaume waliwashurutisha wake zao kwamba watakapofika kituo cha kupigia kura wadai hawajui kusoma na kuandika au wana matatizo ya kutokuona vizuri  ili waume zao wapige kura kwa Chama cha CUF. licha ya sheria kuzuia mikusanyiko ya watu karibu na vituo vya kupigia kura huko Pemba wafuasi wa CUF walikusanyika karibu na vituo vya kupigia kura Katika majimbo ya Ole, kojani, Chonga, Mkanyageni, Mtambwe, Wete, Jadida, na Konde,. Vituo vya shengejuu pujini, kiuyu, Minungw’ini kulikuwa na wafuasi wa CUF waliokusanyika na hata walipotakiwa kuondoka na polisi hawakutii.
Ndugu waandishi wa habari,
Yote hayo yametendeka mbele ya macho ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi  na licha ya mawakala wetu kulalamikia ukiukwaji huo wa demokrasia hakuna aliyewasikiliza. Ni wazi kuwa kuliandaliwa mazingira ya wizi wa kura na ukiukwaji wa taratibu na sheria uliopewa baraka na baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi tunalaani vikali vitendo vya wafausi wa Chama cha CUF  na tunaziomba pia Jumuiya za kimataifa kuungana nasi katika kulaani vitendo hivyo ambavyo havikubaliki hata kidogo.
Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka wale wote wanaohusika na uharamia huu na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria.
Sote tunafahamu kuwa misingi ya uchaguzi huru ni pamoja na masuala mazima ya kutotishwa wapigakura, kutoshurutishwa kupiga kura kwa Chama fulani kwa maana mpigakura awe huru kuchagua Chama anachokitaka , kuwepo kwa mawakala na watazamaji wengine wa Uchaguzi mambo ambayo kwa sehemu kubwa hayazingatiwi  katika Majimbo mengi kule Pemba.
Wakati tukijiandaa kurejea Uchaguzi wa Zanzibar UVCCM. Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuwa makini na watendaji wake hasa wasimamizi wa vituo kule Pemba ambao kwa namna moja au nyingine wanashirikiana na Chama cha CUF kuvihujumu Vyama vingine hasa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu waandishi wa habari,
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na pengine ilijulikana mapema na waangalizi wa Uchaguzi, Makundi ya Waangalizi wa Uchaguzi hasa wale wa Kimataifa  walikipa kisogo Kisiwa cha Pemba. Tujiulizeni kwa nini waangalizi wengi walisalia katika Kisiwa cha Unguja na kukiacha Kisiwa cha Pemba?
Hata hivyo tunazo taarifa za uhakika kuwa baadhi ya waandishi wa habari nao waliondolewa kwa hila na vitisho huko Pemba kwa madai kuwa kungeweza kutokea machafuko ambayo yangehatarisha aidha maisha au usalama wao .
Mpango huo wa  vitisho tumepata ushahidi umeratibiwa na kusimamiwa ipasavyo kwa karibu na waandishi wawili  wa habari wa kike ambao ni wafuasi na mashabiki wa CUF waliokuwa wakipokea maelekezo kutoka kwa Kiongozi mmoja wa Upinzani huko Zanzibar.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU

No comments:

Post a Comment