Waandishi Wetu
MGOMBEA urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, ametenga kiasi
kikubwa cha fedha kununua wapigakura milioni 10 nchi nzima ili kujihakikishia ushindi
katika safari yake ya mabadiliko ya kuelekea Ikulu.
Habari zilizopatikana kutoka vyanzo vya kuaminika,
zinasema mgombea huyo amepanga kufanya ‘biashara’ hiyo ya kununua wapigakura kati
ya Oktoba 23 na 24, ikiwa ni siku moja au mbili kabla ya upigaji kura, biashara
iliyopewa jina la ‘nauli kwa wapigakura’ wake Oktoba 25.
Tayari mgawo wa kwanza wa fedha hizo umeshatolewa kwa vikundi
vya wanawake katika mikoa kadhaa ukiwemo mkoa wa Morogoro.
Mratibu mkuu wa mpango huo wa kununua idadi hiyo ya wapigakura
ametajwa kwa jina la Regina Lowassa, ambaye ni mke wa mgombea huyo.
Kwa karibu wiki ya pili sasa, Regina amekuwa haonekani kwenye
mikutano ya kampeni za mumewe kutokana na kupewa kazi hiyo ya kuorodhesha majina
ya watu milioni 10 nchi nzima.
Kwa mujibu wa habari hizo, ili mtu yeyote aweze kupata mgawo
huo wa fedha za Lowassa, ambazo kiasi halisi hakijaweza kupatikana hadi sasa,
lakini zikitajwa kuwa kati ya Sh 50,000 na 100,000 kulingana na eneo analoishi mtu,
kwa maana ya wanaoishi mijini na nje ya miji.
Mpango huo wa Lowassa, ambao umetajwa na baadhi ya wachambuzi
wa mambo kwamba ni moja ya mbinu chafu ambayo ilikuwa haijawahi kutokea katika historia
ya chaguzi za nchi hii, umetajwa kupata baraka zote kutoka kwa baadhi ya vigogo
wa juu katika Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
ambao wanadaiwa kutoa maelekezo kwa maofisa wao mikoani ‘kufumbia macho mchezo huo.’
Aidha, mpango huo unalenga kumhakikishia Lowassa kupata kura
milioni 14, ambazo mara kadhaa amekuwa akizitaja katika maeneo mbalimbali nchini
aliyokwisha kufanya kampeni zake za kuwaomba kura wananchi.
Ili kujihakikishia idadi hiyo ya kura, Lowassa anadaiwa kutenga
fungu maalumu la fedha kwa ajili ya kununua kura milioni 10 kwa fedha taslimu,
akiwa na matumaini kwamba kura hizo milioni nne zilizobaki ili kufikisha kura milioni
14, ataweza kuzipata kutoka kwa wapigakura wenye mapenzi na yeye, maarufu kwa jina
la wenye ‘mahaba na Lowassa.’
Wananchi wema na wazalendo kwa Taifa hili wanaoishi mjini
Morogoro, wengi wao wakiwa ni wajisiriamali waliojiajiri katika kazi za bodaboda,
mama na baba lishe pamoja na wauza mbogambago katika Soko Kuu la mkoa huo, ndiyo
wamekuwa watu wa kwanza kufichua mpango mzima huo wa Lowassa.
Kwa mujibu wa wananchi wema na wazalendo hao kwa Taifa lao,
Regina Oktoba 2, mwaka huu, alikuwa mjini Morogoro kwa ajili ya mradi huo.
Akiwa mjini Morogoro tarehe hiyo, mama huyo anadaiwa kukutana
na baadhi ya viongozi wa vikundi vya wajasiriamali, wakiwemo madereva hao wa bodaboda,
mama na baba lishe, wauza mbongamboga, makondakta wa daladala na wapigadebe.
Inaelezwa kwamba katika maelekezo yake kwa makundi yote hayo,
Regina aliwataka kuorodhesha majina ya wapigakura 300,000, popote walipo katika
mkoa huo pamoja na namba zao za simu za mkononi, ambazo zitatumika kuingiziwa fedha
hizo siku mbili au siku moja kabla ya kupiga kura, Oktoba 25, mwaka huu.
Orodha hiyo ya wapigakura 300,000, imetajwa kuwa kiwango
cha chini kabisa kinachomhakikishia Lowassa kupata kura 7,500,000 kutoka katika
mikoa yote 25 ya Tanzania, huku kwenye mikoa yenye idadi kubwa ya wapiga kura kama
vile Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Arusha, Tanga na mingineyo, orodha ya chini ya
wapigakura inayotakiwa ikianzia 400,000, hali itakayomhakikishia kupata kura hizo
milioni 10.
Kutoka Morogoro, mke huyo wa Lowassa alikwenda mkoani Tanga
kati ya Oktoba 3 na 4, kwa ajili ya kuendelea na mradi huo ambao kwa mujibu wa vyanzo
hivyo vya uhakika, utafanyika nchi nzima, hasa kwa upande wa Tanzania Bara.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hoseah, hakuweza kupatikana
ili pamoja na mambo mengine, aeleze jinsi ofisi yake ilivyojipanga kukabiliana na
mbinu chafu hiyo ya rushwa ya kuwanunua wapigakura, lakini ofisa mmoja mwandamizi
wa taasisi hiyo aliyezungumzia suala hilo kwa sharti la kutotajwa jina lake,
ameahidi kulifuatilia.
Ili kudhibiti uovu huo wa Lowassa katika uchaguzi wa mwaka
huu, ofisa huyo wa TAKUKURU ameomba ushirikiano kutoka kwa vyombo vya habari na
mwananchi mmoja mmoja kupata walau namba 10 za watu walioko kwenye orodha ya wapigakura
hao wa mgombea urais huyo ili iwe rahisi kwa maofisa wa taasisi hiyo kufuatilia
vyema na kwa ufanisi.
“Jambo hilo linawezekana kutokana na jinsi jamaa alivyopania
kuupata urais wa nchi hii, tuachie tutalifanyia kazi. Kikubwa ninachokiomba kwenu
(waandishi), ili kuturahisishia kazi hii vyema na kwa ufanisi, ni kutoa ushirikiano
kwetu tupate namba za simu hata 10 tu kutoka mkoa wowote za wapigakura walioko kwenye
orodha ya kupata mgawo wao huo ili tuweze kuzifuatilia,” alisema ofisa huyo.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, kupatikana kwa namba hizo za simu,
hata kama ni tano tu, zinaweza kusaidia kukamatwa kwa mtu atakayekuwa anatuma fedha,
kama itatokea namba ya mtumaji huyo kwa watu hao mbalimbali itakuwa ni moja,
lakini pia kama viwango vya fedha vinavyotumwa vitakuwa vinafanana.
Taarifa hizi za mpango huu wa Lowassa wa kutaka urais wa
kuununua kwa fedha, umefichuka huku habari kutoka katika Makao Makuu ya CHADEMA,
yaliyoko Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam, zikibainisha mpango mwingine unaofanana
na huo.
Mpango mwingine huo, kwa mujibu wa taarifa hizo za makao
makuu ya CHADEMA, ni maelekezo ya Lowassa kwa viongozi wakuu wote wa vyama vinavyounda
UKAWA, kuelekeza nguvu zao kwenye kusaka wabunge wa majimboni, huku akiwataka kazi
ya mkakati wa kuingia Ikulu, kumwachia yeye na wapambe wake.
“Lowassa ametoa maelekezo kwa viongozi wetu na viongozi wengine
wote wa UKAWA, wao wahangaike na kutafuta wabunge tu majimboni, kazi ya namna atakavyoshinda
na kuingia Ikulu baada ya tarehe 25, wamwachie yeye,” anasema ofisa huyo wa CHADEMA,
ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za wazi kabisa.
No comments:
Post a Comment