Wednesday, 7 October 2015

UKAWA WAVURUGWA



Na Waandishi Wetu, Arusha
MTIKISIKO mkubwa umevikumba vyama vinavyounda UKAWA, mkoani hapa baada ya ujio wa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kutikisa jijini hapa na kusababisha mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, kubadilishiwa ratiba.
Pamoja na kuahirisha mikutano hiyo, pia umoja huo kwa sasa umejikita kuandaa hujuma dhidi ya CCM, wilaya ya Arusha na mkoa kwa ujumla ikiwemo ya kukusanya kadi, bendera na kununua fulana za Chama ili kuwavalisha vijana ambao baadaye wajitokeze kuwa wamejiunga na CHADEMA.
Tayari, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi nchini,  wametakiwa kufuatilia na kuchukua hatua kali dhidi ya wanasiasa wanaokula njama za kutaka kuvuruga mikutano ya kampeni ya vyama vingine vya siasa.
Vijana hao wanaandaliwa kwa ajili ya kuzichoma moto fulana na kadi hizo feki za CCM katika mikutano ya Lowassa, hususan utakaofanyika leo katika Kata ya Sinoni, Arusha.
Kwa mujibu wa ratiba ya awali ya mgombea huyo, kabla ya kuwasili kwa Dk. Magufuli, ilikuwa ikionyesha angefanya mkutano wa hadhara katika viwanja hivyo katika Kata ya Sinoni, jana, ikiwa na lengo la kuzima yale yaliyozungumzwa na Dk. Magufuli, lakini ghafla ilibadilika.
Ratiba ya Lowassa inaonyesha kuwa leo angefanya mikutano katika eneo la Ngaramtoni jimbo la Arumeru Magharibi, asubuhi na saa tano angefanya mkutano katika jimbo la Arumeru Mashariki, eneo la Usa-River na jioni jimbo la Arusha Mjini eneo la Sinoni.
Kufuatia hofu ya kukosa watu iliyowakumba viongozi wa UKAWA, walilazimika kubadilisha ratiba hiyo kama ilivyothibitishwa na Katibu wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Kalist Lazaro na kwamba, mgombea huyo atakuwa na mikutano miwili tu katika jimbo la Karatu na jioni Sinoni jijini Arusha.
Aidha, alisema kutokana na mabadiliko hayo, leo Lowassa atafanya mikutano miwili katika jimbo la Longido, eneo la Longido Mjini na Namanga huku akipita eneo la Ngaramtoni na si mkutano wa hadhara kama ilivyokuwa imepangwa.

HUJUMA ZA UKAWA
Katibu wa CCM wilaya ya Arusha, Feruz Banno, alisema kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia, zimeeleza kuwa viongozi wa UKAWA wamekuwa wakiwapa fedha vijana kwa ajili ya kununua fulana, kadi na bendera za CCM watakazozionyesha wakizirejesha kwenye mkutano huo.
Alisema hilo walishalibaini na kwamba haliwezi kuwa na madhara kwa kuwa anaamini hakuna mwana-CCM yeyote wa kweli anayeweza kufanya hivyo bali watakaokubali ni wale mamluki waliotengenezwa kwa kazi hiyo.
“Kadi watakazokua nazo vijana hao si za kweli kwa kuwa kwa sasa sisi hatutoi kadi za wanachama wapya bali ni zile zilizorejeshwa mwaka 2010, ndizo watakazozitumia kwa hujuma hizo, lakini tunasema hiyo haitawasaidia kwa kuwa wanachama wetu wako makini,” alisema.
Hata hivyo, alisema kuhusu fulana na bendera walizoziandaa kuzichoma siku hiyo ya mkutano ni jambo rahisi kulifahamu kwa kuwa Chama kimekuwa kikigawa sare hizo bure na zingine zikiuzwa kama sehemu ya hamasa, jambo ambalo limewezesha hujuma hizo kufanyika kwa urahisi.
Alisema jambo lililosababisha mafuriko hayo ya watu ni kutokana na kuhamasika na sera nzuri na zinazotekelezeka zinazotolewa na Dk.Magufuli, hali iliyowajengea imani na kuhamasika kuja kumsikiliza.
“Watu wamehamasika sana, kwa kweli wanampenda Dk. Magufuli, hana kashfa wala makandokando kama wagombea wengine na ni mchapakazi, sasa wataachaje kuja… mkutano wao utajaa watu wa mikoa ya jirani ambao watakesha uwanjani wakinywa viroba na hoteli na gesti zitajaa,” alisema.
WATWANGANA MAKONDE
Wakati Arusha wakijipanga kwa siasa chafu, Jimbo la Mwanga hali ni tete kutokana na kushindwa kukubaliana nani asimame kugombea nafasi ya ubunge baina ya Henry Kileo wa CHADEMA na Yangsevia Msuya, ambaye anatoka NCCR-Mageuzi.
Wagombea hao ambao wote kwa pamoja walikuwa katika uwanja wa Cleopa Msuya, wakimsuburi Lowassa, ambaye hata hivyo hakutokea, walianza kurushiana maneno na majigambo hali iliyosababisha wafuasi wa vyama hivyo kuanza kuchapana makonde.
Hali hiyo ya sintofaham ilisababisha vurugu kubwa kati ya wafuasi wa vyama hivyo viwili, ambapo mpaka sasa wingu zito limetanda.

No comments:

Post a Comment