Friday, 2 October 2015
NEC: HAKUNA WIZI WA KURA
NA WAANDISHI WETU
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema madai yanayotolewa na wanasiasa kuwa kuna uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi, hayana ukweli.
Pia, imewataka wanasiasa ama vyama vyenye ushahidi wa uchakachuaji wa matokeo kuwasilisha kwa NEC ili udhibitiwe badala ya kutoa lugha zenye kuhatarisha amani.
Amesema baadhi ya vyama vimekuwa vikitoa malalamiko ya uchakachuaji wa matokeo, lakini havijawahi kuwasilisha ushahidi kuhusiana na wizi huo, jambo ambalo amesema si sahihi.
Aidha, imevionya vyama kuacha kauli za kudai kuwa vitasusia uchaguzi mkuu kwani, ni za hatari ambazo zinaweza kuliingiza taifa mahali pabaya na kuwakatisha wananchi tamaa.
Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, ambapo alisema tume hiyo daima inasimamia haki na usawa.
Amesisitiza kuwa NEC ndio yenye jukumu la kutangaza matokeo ya urais na kwamba, licha ya matokeo kubandikwa kwenye vituo vya kupigia kura bado mshindi halali atatangazwa na chombo hicho na si vinginevyo.
Jaji Lubuva alitumia fursa hiyo kuvitoa hofu vyama vya siasa kuwa hakuna wizi wa kura wala uchakachuaji kama inavyodaiwa na baadhi ya vyama.
“Kuna vyama vinadai kuna wizi wa kura unafanyika ni vyema wakasema zinaibiwaje…zinapitia dirisha gani ili kuanzia sasa tulizibe kabisa au watuletee ushahidi namna kura zinavyoibiwa.
“Tunawatoa hofu wananchi na vyama vya siasa kwa ujumla kuwa hakuna wizi wa kura hayo ni maneno ya mitaani ambayo hayana ukweli wala ushahidi wowote. Mwenye ushahidi alete hapa,” alisema Jaji Lubuva.
Alivitaka vyama vya siasa kujenga imani na NEC na kwamba, haijawahi kumbeba wala kumpendelea mgombea yoyote.
Aidha, Jaji Lubuva alieleza kushangazwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya vyama vya siasa pamoja na wagombea kuwa watasusia uchaguzi mkuu, ambao utafanyika baadaye mwezi huu.
Alisema kauli za aina hiyo ni za hatari na kwamba zinakatisha tamaa wapigakura hivyo aliwataka wanaotoa kauli za aina hiyo kuacha mara moja.
“Wapo baadhi ya watu wanasema watagomea uchaguzi… sasa ukijiuliza watagomea kwa sababu gani hawasemi. Kauli za aina hiyo si nzuri kutolewa na wanasiasa,” alisema.
Hata hivyo, alisema pamoja na matokeo ya urais, kupandikwa vituoni bado mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya rais kwa mujibu wa sheria ni NEC na sio mtu mwengine yoyote.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, karatasi za kupigia kura, hazijawasili nchini na zimechelewa kwa sababu ni hati ambazo zinawasili mwishoni kutokana na umuhimu wake.
Aliwataka wahariri wa vyombo vya habari kujiepusha na kutangaza matokeo bali wanachopaswa kufanya ni kutangaza idadi ya kura alizopata mgombea husika kwenye vituo.
Jaji Lubuva alisema vyombo vya habari ni muhimu katika jamii hivyo vinatakiwa kutoa kipaumbele kwa habari zenye maslahi ya taifa badala ya zile zinaoweza kuchochea vurugu miongoni mwa jamii.
Aliwataka wahariri kuepuka kutoa habari zinazotoka kwenye vyanzo visivyo rasmi ili kudumisha amani, umoja na usalama wakati wa uchaguzi mkuu.
KAULI ZA VIONGOZI
Jaji Lubuva aliwaasa wahariri kuwa wanapaswa kuwa makini na kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na kwamba mambo mengine wanayotamkwa hayafai kuripotiwa kwa jamii.
Alisisitiza kuwa wahariri wana jukumu la kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kura zao kwa mustakabali wa taifa.
Jaji Lubuva alisema NEC, inawataka viongozi hao kuacha kulalamika bali pale wanapoona hawaridhishwi na kauli au mwenendo wa chama kingine cha siasa, sheria za maadili zipo, wanapaswa kuzitumia.
KUTANGAZA MSHINDI
Mwenyekiti huyo alisema vyombo vya habari havina mamlaka ya kutangaza mshindi, bali wanachoruhusiwa ni kutangaza idadi ya kura alizopata mgombea husika na kwamba mamlaka ya kutangaza mshindi ni ya NEC.
“Si jukumu lenu kutangaza mshindi ni nani, isipokuwa kubainisha idadi ya kura aizopata mgombea, kinyume cha hapo ni kuingilia kazi ya tume,” alisisitiza.
WAGOMBEA WAHESHIMU MATOKEO
Aliwataka wagombea wote kuwa tayari kupokea matokeo yatakayotolewa na tume badala kupinga kwa kuwa walitia saini wakati wanateuliwa na tume kugombea nafasi zao.
“Hilo lilikuwa ni sharti moja wapo la mtu kikidhi kuteuliwa kuwa mgombea, ambapo ni pamoja na kukubaliana na matokeo yatakayotangazwa na tume, awe ameshinda ama kushindwa,” alisema.
Hivyo, washiriki katika uchaguzi wawe tayari kukubali matokeo yatakayotangazwa na tume kama walivyotia saini.
KAILIMA
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, aliwaasa wahariri ambao wakati huu wa kampeni wameonyesha mwelekeo wa kuligawa taifa kikabila, kikanda kuacha mara moja.
“Kalamu zinaua kuliko risasi, nawataka kuacha mara moja kumwaga mbegu ya kuligawa taifa, si kipindi hiki cha uchaguzi tu, bali siku zote mtumie kalamu zenu kujenga umoja, uzalendo na mshikamano kwa jamii,” alisema.
VIFAA VYA KUPIGIA KURA VITUONI
Kailima alisema hadi kufikia Oktoba 15, mwezi huu, vifaa vyote vitakuwa vimeshawasili katika majimboni kote nchini ambapo, mwishoni mwa wiki ujayo tume itatoa takwimu kamili za watakaopiga kura.
Alisema tayari watendaji wa uchaguzi wameshateuliwa, 30 katika ngazi ya mkoa, 972 majimboni na kwenye kata watendaji 7914 na waliashaanza kupatiwa mafunzo tangu Septemba 23, mwaka huu, ili kumudu majukumu yao kikamilifu.
Alisema mbali na waangalizi wa uchaguzi, wapo watazamaji wa uchaguzi 12 wa kimataifa na 75 wa hapa nchini.
VITUO
Mwaka huu kutakuwa na vituo vya kupigia kura 72,000, ambapo kila kituo kitakuwa na wapigakura 450.
NEC, iliwataka wapiga kura kufika kwenye vituo walivyojiandikishia siku nane kabla ya uchaguzi kuangalia majina yao pamoja na utaratibu wa vituo vya kupigia kura utakavyokuwa.
Ilisema watu milioni 23.7, wameandikishwa kupiga kura hapa nchini, ambapo majimbo ya uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani ni 264, kata 3,957 za Tanzania Bara, ambapo wagombea ubunge ni 1,218 na wagombea udiwani ni 10,879.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment