Friday, 2 October 2015

DK. SHEIN: MSIDANGANYIKE



VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamewataka wananchi wa Kiwani kutodanganyika na kutofanya makosa ya kuwachagua wapinzani upinzani, ambao wamekuwa wakitoa ahadi zisizoweza kutekelezeka.

Viongozi hao waliyazungumza hayo kwa nyakati tofauti katika Mkutano wa CCM wa Kampeni za uchaguzi huko Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba uliohudhuriwa na maelfu ya wanaCCM pamoja na wananchi ambapo, mgeni rasmi alikuwa mgombea Urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Katika maelezo yao viongozi hao wa CCM walieleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za maendeleo ya uchumi na huduma za jamii ni utekelezaji wa ahadi za CCM na mgombea wake katika uchaguzi uliopita.

Dk. Maua Daftari, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa alikipongeza chama cha CCM kwa kuwajali wanawake kwa kuwaingiza katika maamuzi kutokana na kuwajali.

Alisema kuwa km 7.5 za barabara kutoka Mgagadu hadi Kiwani itatengenezwa mara tu baada ya kuingia madarakani Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Dk. Shein.

Dk. Daftari alisema kuwa amani, utulivu, umoja na mshikamano ni Sera ya CCM, na kuwasihi wafuasi wa CUF kutofanya mambo ya ajabu kwani tayari wameshaanza mikutano ya siri ya kutaka kuwadhuru wanaCCM lakini Serikali iko macho na hilo na kuwataka wananchi na wanaCCM kutobabaik.

Pamoja na hayo, Dk. Daftari aliwaeleza vijana na wananchi wa Kiwani kuwa Serikali imo katika mikakati ya kutafuta ufumbuzi wa suala la ajira kwani hatua za uchimbaji mafuta na gesi zitasaidia kutatua suala hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai alisema kuwa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM imetekelezwa kwa asilimi 90 ambapo Dk. Shein ameweza kuisimamia Serikali vizuri bila ya kuyumba na amekuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha Wazanzibari wa Unguja na Pemba kuwa wamoja na kuwaunganisha Wazanzibari katika kusimaimia Mapinduzi  na Muungano.

Alisema kuwa Dk. Shein ameweza kutatua matatizo kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa agizo kwa kumuagiza Waziri wa Fedha kununua meli ili kutatua tatizo la usafiri wa bahari kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema kuwa CCM itapata ushindi wa zaidi ya asilimia 60 na kuwataka wananchi kumchagua Dk. Shein ili aendelee kuyalinda Mapinduzi pamoja na Muungano uliopo.

Naye Balozi Amina Salum Ali aliwataka wananchi wa Jimbo la Kiwani kuwarudisha Muwakilishi na Mbunge wa Jimbo hilo  kwa tiketi ya CCM pamoja na kumchagua Dk. Shein na viongozi wengine wote wa CCM.

Balozi Amina aliwataka vijana wa Zanzibar wasibabaishwe na lugha za wapinzani huku akiwataka kuangalia vijana wa Libya walivyokua hapo kabla na hivi sasa walivyo na kuwaeleza kuwa mabadiliko wanayoambiwa kuwa sio kweli.

Alisema kuwa hadithi ya mafuta ni ndefu kwani wakoloni walijua na hawakuchukua jitihada zozote kwa kudhani kuwa Wazanzibari watafaidika huku akisema kwa hivi sasa suala la mafuta limeshafanyiwa kazi na Serikali chini ya uomgozi wa CCM.

Alisikitishwa na kauli za Maalim Seif anaepita mitaani na kujisifu kuhusiana na suala la mafuta.

Aliwataka wananchi wa Kiwani kueleza haja ya viongozi katika chama cha CUF kuwekewa muda maalum wa kugombania nafasi za uongozi kwani Maalim Seif amekuwa akisimama yeye peke yake katika nafasi ya urais wa Zanzibar tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Naye Balozi Ali Karume aliwataka wananchi na wanaCCM kumuamini na kuwataka waombe kwa Mwenyezi Mungu kumpata kiongozi bora na kusema kuwa kwa Zanzibar hakuna kiongozi bora na anaeweza kuendesha nchi bali ni Dk. Ali Mohamed Shein na tayari miaka mitano aliyoyafanya yameonekana.

Alimuombea kura Dk. Shein, Magufuli, Samia, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wote wa CCM huku akiwaeleza wananchi kuwa viongozi wa CUF wameshindwa kuwatetea wananchi waliowachagua katika kuimarisha miradi yao ya maendeleo ikiwemo barabara na kusema kuwa ndani ya uongozi wa CCM miaka mitano ijayo barabara yao itakuwa imeshatiwa lami.

Mohamed Aboud ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais  aliwaomba na kuwanasihi wananchi na wanaCCM wa Kiwani kutosikiliza maneno ya wapinzani na badala yake waichague CCM kutokana na kuatekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Chini ya Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema kuwa juhudi kubwa zimechukuliwa na CCM chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, maji, umeme na mengineyo huku akishangazwa na vingozi waliopita wa CUF wa jImbo hilo nini wamekifanya na kuwafanyia wananchi ndani ya miaka mitano.

Alisema kuwa Dk. Shein, amefanya mambo mengi katika uongozi wake wa miaka mitano iliyopita na tayari amejenga misingi imara ya kuleta maendeleo katika miaka mitano ijayo.

Waziri Aboud alisema kuwa nana anasima mia mafuta, zao la karafuu liimarike na liwe na bei, ujenzi wa jengi la uwanja wa ndege na miradi mengine ya maendeleo.

"Hawa rafiki zetu wapenda kupandia gari letu wakati lishajaa...lakini milango yetu iko wazi waje wajiunge na CCM ili tuijenge nchi yetu na sisi tuko tayari kuwakaribisha wale wote wanaotaka umoja na mshikamano",alisema Aboud.

Aliwataka CUF kutopoteza muda na badala yake kuiunga mkono CCM "watu hawakitaki maana chama hicho kwani wameshakiuza," alisema Mohamed Aboud.

Aboud alisema kuwa CCM ni Chama imara, kina msimamo na hakiyumbi na kimekuwa kikitetea wananchi na kuwataka wananchi, wanaCCM pamoja na wafuasi wote wa CUF kuwatilia kura wagombea wa CCM.

No comments:

Post a Comment