RAIS Jakaya Kikwete akiwa na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dinna
Hyde, walipokutana nchini Marekani hivi karibuni.
Na Mayage S Mayage
TANZANIA, chini ya uongozi mahiri wa Rais Jakaya
Kikwete, imefuzu masharti yote yaliyotakiwa na Shirika la Maendeleo la Melenia
(MCC) la Marekani, baada ya watendaji wakuu wa shirika hilo kujiridhisha na
hatua zinazochukuliwa na serikali katika utendaji wake, hasa katika eneo la
utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Kutokana na kuridhishwa huko, Mtendaji Mkuu wa MCC,
Dinna Hyde, amemhakikishia Rais Kikwete kwamba, nchi yake imeingizwa katika
mpango wa pili wa MCC, kwa maana ya MCC-2, ambao unaihakikishia Tanzania
kupatiwa msaada wa bure wa Dola za Marekani milioni 472.8, sawa na karibu sh.
bilioni 992.8.
MCC ni taasisi inayomilikiwa na Serikali ya Marekani kwa
asilimia mia moja. Moja ya jukumu kuu la taasisi hiyo, ni kutoa misaada kwenye
miradi muhimu ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa nchi
zinazoendelea.
Aidha, majukumu ya MCC yanajengwa katika msingi kwamba
msaada wowote utakaotolewa na Serikali ya Marekani kupitia shirika hilo,
utaleta tija na ufanisi wenye matokeo mkubwa zaidi kwa serikali husika katika
nyanja za utawala bora, uchumi huria na uwekezaji wa moja kwa moja kwa
mwananchi mmoja mmoja kwa lengo la kupunguza, kama si kuondoa kabisa umasikini.
Kwa hiyo, ili nchi yoyote ile duniani ifanikiwe kupata
misaada hiyo ya mabilioni ya shilingi kutoka Shirika hilo la MCC la Wananchi wa
Marekani, msingi wa kwanza ni kwa nchi husika kukidhi vigezo na masharti yao
yanayojengwa kwenye misingi ya utawala bora, hasa katika eneo la rushwa na aina
nyingine yoyote ya ufisadi.
Itakumbukwa kwamba Serikali ya Tanzania ilifanikiwa
kupata msaada wa kwanza wa MCC, kama sehemu ya mpango wa kwanza wa shirika hilo
(MCC-1), mwaka 2008.
Mpango huo wa kwanza wa miaka mitano, ambao ulikamilika
mwaka 2013, kabla ya Tanzania kuingizwa tena kwenye mpango wa pili, kama
ingekidhi vigezo na masharti ya mpango huo wa pili (MCC-2).
Katika mpango huo wa kwanza wa MCC-1, Tanzania
ilifanikiwa kupata msaada wa Dola za Marekani milioni 698, sawa na sh. trilioni
1.46. Fedha hizo, pamoja na mambo mengine, ndizo zilizowezesha ujenzi wa
barabara za Tanga-Horohoro, Tunduma-Sumbawanga na Namtumbo-Songea hadi Mbinga.
Aidha, fedha hizo, katika sekta hiyo ya ujenzi wa
barabara kwa viwango vya lami, zilitumika pia kujenga karibu barabara zote kuu
katika kisiwa cha Pemba, Zanzibar, kuanzia ile inayotoka uwanja wa ndege wa
Pemba.
Kwa upande wa sekta ya maji, fedha hizo zilitumika
kuboresha mitandao ya maji safi na salama katika miji ya mikoa ya Dar es Salaam
na Morogoro, wakati kwa upande wa nishati ya umeme, zilitumika kusambaza njia
ya pili ya umeme kutoka Bara kwenda visiwani Zanzibar.
Lakini pia, ni fedha hizo hizo za MCC-1 zilizotumika
kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), kiasi cha
kuwezesha sasa zaidi ya asilimia 40 ya Watanzania kupata huduma ya umeme kutoka
asilimia 13 wakati serikali hii inaingia madarakani mwaka 2005.
Taarifa hizi za kufuzu kwa Tanzania kuingia katika awamu
ya pili ya mpango wa MCC, zimekuja wakati baadhi ya wanasiasa wa kambi ya
upinzani, wakiongozwa na aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, wakiendelea kuupotosha umma kwamba
Tanzania imepoteza fursa hiyo ya kuingizwa katika mpango wa pili wa MMC-2,
kutokana na madai kwamba serikali hii ya CCM imeshindwa kupambana na ufisadi.
Taarifa hizo njema, zimeweka wazi kuwa Bodi ya MCC,
katika kikao chake cha Septemba 17, mwaka huu, iliridhishwa na hatua mbalimbali
zinazochukuliwa na Serikali ya Rais Kikwete katika mambo yote yanayohusiana na
utawala bora, likiwemo suala la kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi
mwingine.
Itakumbukwa kwamba katika Mkutano wa 16/17 wa Bunge
lililomaliza muda wake, uliofanyika Novemba, mwaka jana, pamoja na Mkutano wa
18 wa Februari mwaka huu, baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani, wakiongozwa
na aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, aliyekuwa mbunge wa
Ubungo, John Mnyika na aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe,
walisimama ndani ya mabunge hayo wakati wa kuchangia mijadala na kujiapiza
sakata la Tegeta Escrow limeipotezea fursa Tanzania kuingizwa katika mpango wa
pili wa MCC.
Kafulila na wezake hao walitokwa na madai hayo baada ya
Bodi ya Shirika la Maendeleo la Milenia (MCC) la Marekani, Novemba hiyo mwaka
jana, kutoa taarifa yake iliyoitaka Serikali ya Tanzania kuongeza jitihada za
kupambana na rushwa na ufisadi mwingine.
Msisitizo wa MCC katika taarifa yao hiyo, ilikuwa ni
kuitaka Serikali ya Tanzania kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika wakuu wa
sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, vingenevyo Tanzania ingeshindwa kuingizwa
katika Mpango wa Pili wa Shirika hilo (MCC-2).
Wakati ikitolewa taarifa hiyo ya MCC, mjadala wa sakata
la akaunti ya Tegeta Escrow ulikuwa umepamba moto ndani na nje ya Bunge,
ukihusu suala zima la utoaji wa fedha katika akaunti hiyo zinazofikia zaidi ya sh.
bilioni 200, hali iliyolilazimu Bunge kuiagiza Kamati ya Bunge ya Fedha za
Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, kuchunguza madai ya
uchotwaji wa fedha hizo alizokabidhiwa mwekezaji mpya wa IPTL, mfanyabiashara
Herbinder Seth na kampuni yake PAP.
Nakumbuka, katika moja ya mchango wake bungeni kuhusiana
na misaada hiyo ya MCC na sakata la Tegeta Escrow, Novemba, mwaka jana,
Kafulila alisimama bungeni na kusema:
“Taarifa hii (ya MCC ya kuitaka Serikali iongeze juhudi
katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi) imekuja wakati mwafaka. Imenivisha
nguo baada ya kuwa nimevuliwa nguo bungeni na kuitwa muongo.
“Nilisema hapa bungeni kwamba hasara tunayoipata
kutokana na ufisadi huo wa Escrow, ni zaidi kwani misaada tuliyokuwa
tunaisubiri ya Sh. 900 bilioni kutoka Ulaya na Marekani, dola milioni 700 na
ukizijumuisha Sh. 306 bilioni ni zaidi ya Sh. trilioni 2.0.
“Fedha hizi za MCC zilikuwa zitoke tangu Septemba, mwaka
huu (2014) kama ambavyo Ghana imezipata, lakini kutokana na uzembe wa Serikali
ya Tanzania, imepoteza kiasi hicho cha fedha.
“Waziri wa fedha (Saada Mkuya) na Profesa Muhongo
(aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo) walikana
bungeni hapa kwamba ninasema uwongo (kuhusu Tanzania kukosa msaada wa awamu ya
pili-MCC-2), sasa ukweli umejulikana. Ni nani mkweli na nani ni mwongo?”
Bila shaka, swali hilo la Kafulila aliloliuliza bungeni
juu ya ni nani mkweli na nani mwongo kati yake na mawaziri hao aliowataja,
litakuwa limepatiwa majibu sahihi na taarifa hii mpya ya Mtendaji Mkuu wa MCC, Dinna
Hyde, mbele ya Rais Kikwete, walipokutana hivi karibuni mjini New York,
Marekani. Akiweza, Kafulila akiri hadharani kwamba yeye ndiye alikuwa mwongo au
ajinyonge tu!
Katika hili lililofanywa na MCC kwa Tanzania, napenda
nichukue fursa hii kwa moyo wa dhati kabisa kuwashukuru Wamarekani na serikali
yao kwa kuziona juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kujenga
misingi ya utawala bora nchini, lakini pia katika mapambano dhidi ya rushwa na
ufisadi wa aina nyingine yoyote.
Nalazimika kuwashukuru Wamarekani na serikali yao katika
hili kwa sababu natambua kwamba wapo baadhi ya Watanzania wenzetu humu ndani,
wakiwemo kina Kafulila, ambao wana macho, masikio na akili timamu, lakini
wanapita kila siku mitaani na kwenye majukwaa ya siasa wakiwapotosha wananchi
kwamba serikali hii inakumbatia rushwa, ni serikali ya kifisadi, haijafanya
lolote tangu Uhuru wake wa mwaka 1961.
Nawashukuru pia Wamarekani na serikali yao kwa sababu
kufuzu kwa Tanzania kupata mabilioni hayo ya fedha mwakani, kunampa uhakika
mgombea urais wa CCM, Dk John Pombe Magufuli, wa kutekeleza baadhi ya ahadi
zake zinazohusu ujenzi wa miradi ya barabara, usambazaji wa umeme, maji na
kadhalika endapo Watanzania watamwamini na kumpigia kura nyingi Oktoba 25,
mwaka huu.
Kihesabu, kiasi hicho cha fedha cha Sh. bilioni 992.8
kitakachotolewa na Shirika hilo la MCC kwa Tanzania kama sehemu ya utekelezaji
wake wa mpango wa awamu ya pili (MCC-2), zinatosha kabisa kujenga kilomita
992.8 za barabara kwa kiwango cha lami, kwa hesabu ya wastani wa Sh. bilioni
moja kwa kilomita moja.
Lakini pia, fedha hizo zinaweza kutekeleza ahadi ya
kumaliza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, kwa kujenga
mabarabara za juu katika maeneo ya Ubungo mataa, Tazara, Magomeni Mapipa na Morocco.
Kisiasa, hasa katika kipindi hiki cha kampeni za
uchaguzi mkuu, kutolewa kwa fedha hizo za MCC-2 kwa Serikali ya Tanzania,
kutawafanya sasa baadhi ya wanasiasa wa kambi ya upinzani wanaotafuta madaraka
kwa hila na ulaghai, wakose cha kuzungumza majukwaani katika suala zima la
kushindwa kwa Serikali ya CCM katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi.
Ndiyo maana nasema ahsante sana Wamarekani katika hili
la kuruhusu msaada huo katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba
25, nikiamini kwamba taarifa hizo njema zimeendelea ‘kumvua’ nguo David
Kafulina kama alivyosema mwenyewe bungeni katika nukuu ya hapo juu pamoja na
wengine wote waliokuwa wakidai kuwa Tanzania haitapata tena msaada huo.
Nihitimishe makala haya kwa kusema hapa kwamba msaada
huo mkubwa wa mabilioni hayo ya shilingi, yatakayoingizwa katika mpango wa
maendeleo ya nchi kwa miaka mitano ijayo kuanzia mwakani, naamini utawatoa hofu
na wasiwasi wale wote waliokuwa na shaka juu ya uwezo wa Serikali ya Dk.
Magufuli kutekeleza ahadi zake nyingi anazoziahidi katika mikutano yake ya
kampeni. Nawasilisha!
No comments:
Post a Comment