Na Mwandishi Maalumu
WALIOFUATILIA siasa za Marekani wakati wa uchaguzi mkuu wake
wa mwaka 2008, wana kumbukumbu za kampeni ya aina yake iliyokuwa ikifanywa na
aliyekuwa mgombea urais wa chama cha Democrats, Barack Obama.
Nyakati za asubuhi, mchana na jioni, lilikuwa jambo la
kawaida kwa familia za Marekani kupokea wageni waliojitambulisha kama wapiga
kampeni wa Obama.
Hawa walikuwa wakitembea nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa na
jimbo kwa jimbo. Walifanyakazi hiyo kwa kujitolea, lakini baada ya kupata
mafunzo maalumu na pia wakiwa wanaamini kuwa Obama ndiye alikuwa mgombea sahihi
wa urais kwenye uchaguzi huo.
Takribani mwaka mmoja uliopita, baada ya kubaini upinzani
mkali dhidi ya mgombea wao wa nafasi ya Waziri Mkuu, Narendra Modi, chama chake
cha Bharatiya Janata (BJP) kilitumia mbinu hizi za Obama na hatimaye kuibuka na
ushindi kwenye uchaguzi huo.
Ni mbinu za namna hii za kisasa, kistaarabu na kisayansi,
ndizo ambazo CCM inazitumia katika kampeni zake za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Na nyuma ya mbinu hizo, ni mkakati unaoitwa Makepteni wa Magufuli.
Kwa bahati mbaya, vyama vya UKAWA vinatumia magazeti yake
kupotosha umma kuhusu kazi, hasa za hawa wanaoitwa Makepteni wa Magufuli.
Wiki mbili zilizopita, mojawapo ya magazeti hayo, liliandika
habari yake kuu ya ukurasa wa mbele kwamba makepteni hao ndiyo wamepangwa
kufanyakazi za kuiba kura.
Gazeti hilo la MAWIO, lilikwenda mbali kwa kutaja namba za
simu za wahusika wa mkakati huo. Kilichotokea ni kwamba baadhi ya waliotajwa
wameanza kutishiwa maisha yao. Wanatafutwa na kuambiwa watashughulikiwa.
Ni wazi kwamba vyombo hivi vya habari vya UKAWA, itabidi
viwajibike kwa tatizo lolote litakalowatokea wale ambao namba zao za simu
zilibandikwa kwenye gazeti la MAWIO. Hii ni kwa sababu, walichokifanya
kinakwenda kinyume hata na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Makepteni
wa Magufuli
CCM ilifanya uamuzi wa kimsingi kuwa kwenye uchaguzi wa mwaka
huu, itafanya kampeni zake kisayansi. Iliamua kuwa itatumia mbinu na mikakati
yote ya kisasa inayoweza kutumika.
Mkakati mmojawapo ni huo wa Makepteni wa Magufuli au kwa jina
lingine ‘Jeshi la Magufuli’. Mkakati huo unafanana sana na ule uliotumiwa na
Obama mwaka 2008, ukiwa umebuniwa na wapanga mikakati kama David Axelrod.
Ni mkakati usio wa kibabaishaji na usio na uhusiano wowote wa
wizi wa kura kama ambavyo UKAWA sasa wanashupaa kupotosha. Badala ya kuwa
wabunifu na kuiga vilivyo bora, wao wameamua kufanya kampeni bwete, zisizo na
ubunifu na za kulialia kuwa wataibiwa kura.
Wakati CCM ikitengeneza kifanisi mkakati huu, UKAWA
wanaendeleza siasa za kuzomea wagombea wa CCM na wananchi wanaoonekana kuvaa
sare za chama hicho.
Kwa mujibu wa Kitini cha Mafunzo kwa Makepteni wa Magufuli
(ambacho naambatanisha picha yake), kuna malengo kama sita ya kuanzisha mkakati
huo.
Moja ni kujenga mtandao wa ushindi kwenye majimbo yote ya
uchaguzi, kupata taarifa ya hali ya kisiasa kwenye kila jimbo wakati wote wa
uchaguzi, kupaza sauti za wananchi kuhusu kero zao, kuhakikisha mipango ya
kampeni inaendana na uhalisia wa hali ya kisiasa, kufikia idadi kubwa ya
wapigakura na kuhakikisha wana CCM wanapiga kura.
Mkakati wa Makepteni wa Magufuli unalenga makundi yote makuu
kwenye jamii wakiwamo wanawake, vijana, wazee, watu wenye ulemavu, wavuvi,
wafanyabiashara wadogo, wanamichezo, wasanii, waendesha pikipiki (bodaboda) na
makundi mengine.
Kila jimbo la uchaguzi lina makapteni waliopatiwa mafunzo ya
kutosha kupitia kitini hiki. Kazi ya makepteni hawa, kwa kushirikiana na
wagombea wa ubunge na udiwani nchini kote, ni kuhakikisha kuwa CCM inaibuka na
ushindi kwenye uchaguzi huo.
Ukiona watu kwenye vituo vya mabasi wakishawishi wananchi
wapigie kura CCM, ujue hao ni Makepteni wa Magufuli. Ukiona watu wanagonga hodi
nyumbani kwako wakiomba umpigie kura Magufuli na wagombea wa ubunge na udiwani
katika eneo lako, ujue hao ni Makepteni wa Magufuli.
Kwenye gazeti la MAWIO, iliandikwa kwamba makepteni hao
wanachukua namba za vitambulisho vya kupigia kura, jambo lililoelezwa kama ni
ukiukaji wa taarifa.
Huu ni upotoshaji kwa sababu makapteni hawachukui namba za
vitambulisho. Wanachofanya Makepteni wa
Magufuli ni kuwashawishi wapigakura kuchagua wagombea wa CCM katika ngazi zote.
Maajabu ni kwamba, wale wanaofanya siasa za kistaarabu na
ambazo zinatumika katika mataifa yote yaliyokomaa kidemokrasia, sasa
wanatengenezewa fitna waonekane wabaya, lakini wanaofanya siasa za kihuni za
kuzomea na kudhalilisha wanawake, waonekane watu wa maana.
Majukumu ya
Makepteni
Kwa mujibu wa kitini cha mafunzo, kuna majukumu mbalimbali ya
Makepteni wa Magufuli. Kwenye makala haya, nitanukuu maelezo rasmi kutoka
kwenye kitini kueleza majukumu ya msingi ya makepteni.
“Hawa watakuwa
wafanyakazi wa kudumu katika muda wote wa kampeni na watafanya mambo
yatakayowafanya wapigakura waone CCM ndiyo chama pekee kinachotakiwa kuendelea
kutawala.”
Ukiona majukumu hayo ya Makepteni wa Magufuli, utashangaa ni
kwa vipi magazeti yanayoheshimika yanavyokubali kuwatia hofu wananchi kwa dhana
ambazo hazipo na kwa mambo ya kusingizia.
Wiki iliyopita, kuna kinamama wawili waliojitolea kuwa
makepteni wilayani Mbozi, mkoani Mbeya, walikimbia makazi yao wakikwepa vitisho
walivyokuwa wakivitoa viongozi wa UKAWA majukwaani kuhusu Makepteni wa
Magufuli.
Ningefurahi sana kama UKAWA nao wangejikita katika kufanya
kampeni za kisasa. Wamekuwa na kampeni za kawaida, za mgombea kuzungumza kwa
dakika tatu na kubaki mijini kila siku.
CCM kimeweka utaratibu wa kwenda kuzungumza na watu wa mijini
na vijijini. UKAWA wanatakiwa kushindana na CCM kwenye ufanyaji wa kampeni za
kiteknolojia ya sasa, badala ya kubaki kulia kuibiwa kura kila uchao.
CCM inaposema itashinda kwenye uchaguzi wa mwaka huu,
inafanya hivyo ikijua inatumia mbinu zilizotumika kushinda kwingineko.
CCM inajiamini kuwa itashinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka
huu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, kwa sababu inajua itabebwa na wagombea
bora, sera sahihi na usasa pamoja na ufanisi wa mikakati yake ya kisiasa wakati
huu.
Tuache siasa za upotoshaji na uongo na tujikite kwenye siasa
za kweli.
No comments:
Post a Comment