Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
JUMUIA ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM),
imesema haijawahi kufikiria kuanzisha vikundi au kambi za vijana zenye lengo la
kutoa mafunzo ya uharamia.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu
Naibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdulhafar Idrissa, alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari mjini hapa.
Idrisa alikuwa akizungumzia tuhuma
zilizotolewa na Chama cha CUF kuwa, UVCCM imeanzisha vikundi vya aina hiyo.
Alisema UVCCM haina kambi mahali
popote iliyoanzishwa kwa ajili kuandaa vijana kuhujumu uchaguzi mkuu kwa kuwa hilo
siyo jukumu lao.
Idrissa alisema CCM haina sababu ya kufanya
vurugu wakati wa uchaguzi huo kwa vile ina uhakika mkubwa wa kuibuka na ushindi.
"UVCCM inatambua kuwa uharamia
ni kinyume cha sheria na kwa malezi tunayopewa na chama chetu, hatuwezi kutenda
mambo ambayo ni kinyume na sheria na hatuwezi kuruhusu kuivunja katiba ya nchi
yetu," alisema.
Aliongeza kuwa UVCCM imesikitishwa
na kauli za kichochezi zilizotolewa na CUF, zinazodai kwamba wameandaa vijana
wenye lengo la kuharibu uchaguzi kwa kufanya fujo siku za mwisho za kampeni na
siku ya upigaji kura.
"Tunawaomba wananchi wapuuze kauli hiyo na hizo ni ishara za waziwazi za kushindwa kwa CUF, hivyo wanatafuta mahali pa kutua lawama au visingizio baada ya matokeo ya ushindi kutangazwa," alisisitiza.
Alisema CCM Zanzibar ina hakika
itashinda uchaguzi mkuu kama kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, kutokana na hamasa
kubwa ya wananchi wanaojitokeza katika mikutano na kukubalika kwa sera za
chama.
Alisema UVCCM itaendelea kuhamasisha
vijana kujitokeza katika mikutano hiyo ili waweze kupata fursa ya kusikia Ilani
na pia wataendelea kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi kupigakura.
No comments:
Post a Comment