NA
LILIAN JOEL, ARUSHA
HALI
bado ni tete ndani ya CHADEMA, kutokana na wimbi la wanachama wake kukihama na
kujiunga na CCM, ambapo zaidi ya wafuasi wake 30 wilayani Karatu wamekihama
chama hicho.
Wanachama
hao walikihama chama hicho juzi, wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni uliohutubiwa
na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadifa Juma Hamis, alipokuwa akimuombea kura
mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, mgombea ubunge wa Karatu, Dk. Wilbard
Lory na madiwani wa CCM.
Mkutano
huo ulifanyika katika kata ya Dumbechand na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi,
ambapo wanachama wa upinzani, hususan CHADEMA, waliokuwa kwenye mkutano huo,
walivutiwa na sera nzuri na kuamua kurejesha kadi zao na kupewa za CCM.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake, Anna Bohay alisema kata yao inakabiliwa na changamoto
kubwa ya maji pamoja na miundombinu na kwamba, kipindi cha uchaguzi CHADEMA iliahidi
kuwaletea maendeleo lakini haikufanya hivyo.
“Tulipotea
njia, tumedanganywa vya kutosha, hatudanganyiki tena na sasa tumeamua kurudi
CCM kwa kuwa ahadi zake zinatekelezeka na tutafanya kampeni usiku na mchana
kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika wilaya ya Karatu,” alisema.
Akizungumza
katika mkutano huo, Sadifa aliwataka wananchi kuichagua CCM katika uchaguzi wa
mwaka huu, utakaofanyika Oktoba 25, ili iweze kuwaletea maendeleo ya uhakika na
kwa wakati.
Alisema
serikali itakayoongozwa na Dk. Magufuli, itakuwa ya mapinduzi ya viwanda,
ambapo itatoa ajira za uhakika kwa vijana ili kutatua changamoto hiyo kubwa,
ambayo kwa sasa inawakabili vijana wengi hapa nchini, wakiwemo wasomi.
Akizungumzia
migogoro ya ardhi katika kata ya Mang’ola, inayosababishwa na wawekezaji waliohodhi
ardhi kinyemela, alisema baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, kero hiyo
itatatuliwa mara moja na kurejesha mashamba hayo kwa wananchi.
“Mwekezaji
hawezi kuhodhi ardhi na kukaa nayo bila kuiendeleza. Mashamba yote ambayo
hayaendelezwi, nitamuomba rais ayafutie hati na kuwamilikisha wanachi ili waweze
kulima na kuongeza kipato cha familia,”alisema.
No comments:
Post a Comment