Thursday, 1 October 2015

WANANCHI SERENGETI WATOA KILIO KWA SAMIA




NA KHADIJA MUSSA, SERENGETI
SERIKALI ya awamu ya tano, ambayo inaaminika itakuwa chini ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, imeombwa kutoa kipaumbele kwa wilaya ya Serengeti kwa kuhakikisha inamaliza changamoto ya watu kuuawa na wanyama.
Imeelezwa kuwa matukio hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwa kuwa asilimia 94 ya wilaya hiyo ni hifadhi za wanyama na mapori tengefu.
Aidha, serikali imeombwa kuangalia upya mgawanyo wa nafasi za ajira zinazotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), katika hifadhi kwa kutoa kipaumbele kwa wananchi wa wilaya hiyo, ambayo asilimia 70 ya Hifadhi ya Serengeti ipo katika wilaya hiyo.
Serikali pia imeombwa kuongeza bei ya tumbaku ambayo ni moja ya zao la biashara linalotegemewa na wananchi hao, ambapo kwa sasa inauzwa sh. 4,000 kwa kilo.
Hayo yalisemwa jana na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk. Steven Kebwe, katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye viwanja vya Mbuzi, Magumu, mjini hapa.
Dk. Kebwe alisema moja ya changamoto zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo ni uvamizi wa wanyama, ambao umekuwa ukisababisha vifo na ulemavu huku baadhi ya wananchi wakikosa chakula kutokana na wanyama kuvamia mashamba yao.
Kilio cha wananchi hao kimekuja wiki tatu baada ya watu watatu kuuawa na tembo, aliyevamia kwenye moja ya vijiji vilivyoko Magumu.
Dk. Kebwe aliomba serikali ijayo kuifanyia marekebisho sheria ya viwango vya fidia kwa wananchi wanaouawa na wanyama au mashamba yao kuharibiwa.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika jimbo hilo, Dk. Kebwe alisema umefanikiwa kwa kiwango kikubwa, ambapo kwa kutumia fedha zake binafsi, alinunua magari mawili ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya vituo vya afya.
Kwa upande wake, Samia alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kupokea kijiti cha maendeleo kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete, hivyo aliwaomba wananchi kuhakikisha wanamchagua Dk. Magufuli ili aweze kuwa rais na kuwaletea maendeleo.
Samia alisema suala la fidia litafanyiwa kazi na wahusika watalipwa stahiki zao, wakiwemo waliovamiwa na wanyama, kuharibiwa mazao yao pamoja na wale waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Kuhusu suala la upatikanaji wa maji safi na salama, Samia aliwapongeza wananchi kwa kufanikisha miradi hiyo, ambapo mradi mmoja mkubwa upo katika hatua za mwisho kukamilika na kwa sasa wanamalizia ujenzi wa chujio ili waanze kuyasambaza.
Mbali na mradi huo, upo mradi mwingine mkubwa utakaogharimu sh. bilioni 13, ambao unajengwa katika wilaya hiyo kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania na India, ambao utaifanya wilaya hiyo kutokuwa na shida ya maji.
Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa ajira, Samia alisema suala hilo litafanyiwa kazi na serikali ijayo, kwa sababu ni moja kati ya vipaumbele vilivyoko katika ilani.

No comments:

Post a Comment