Thursday, 5 November 2015

HISTORIA MPYA, DK. MAGUFULI KUAPISHWA RASMI LEO






NA MUSSA YUSUPH

ILIKUWA miezi, wiki, siku na hatimaye saa. Tanzania inaingia katika uongozi wa awamu ya tano tangu kuasisiwa kwa taifa hili mwaka 1964.

Alianza mwalimu Julius Nyerere (1964-1985), Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005), Jakaya Kikwete 2005 hadi leo na sasa ni Dk. John Magufuli.

Kwa mantiki hiyo, Watanzania leo wanashuhudia kuapishwa kwa Dk. Magufuli kuwa Rais wa awamu ya tano huku Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais.

Si hivyo tu kwani tukio hilo la Samia kuwa Makamu wa Rais, linaandika historia ya kipekee nchini kwa kuwa mwanamama wa kwanza kushika wadhifa huo tangu kuanzishwa kwa taifa la Tanzania.

Waliomtangulia ni Sheikh Abeid Aman Karume (1964-1972), Aboud Jumbe Mwinyi (1972-1984), Ali Hassan Mwinyi (1984-1985), Joseph Warioba (1985-1990), John Malecela (1990-1994), Cleopa Msuya (1994-1995), Dk. Omar Ali Juma (1995-2001), Dk. Ali Mohamed Shein (2001-2010) na Dk. Mohamed Gharib Bilal (2010-leo).

Tukio hilo la kuapishwa kwa Dk. Magufuli na Samia, litaashiria kuanza kwa uongozi wa awamu ya tano na kukamilika kwa utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Kutokana na umuhimu wa siku ya leo, Rais Kikwete ametangaza leo kuwa siku ya mapumziko ili kuwawezesha wananchi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,  ilisema Rais Kikwete ametoa uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa nchi anatakiwa kuwepo madarakani kwa miaka 10 kwa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.

Dk. Magufuli alipata nafasi hiyo baada ya kuibuka na ushindi kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kushirikisha wagombea wanane kutoka vyama mbalimbali. Alipata ushindi wa kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46.

Mbali na Dk. Magufuli, wagombea wengine waliowania nafasi hiyo ni Edward Lowassa (CHADEMA), Anna Nghwila (ACT-Wazalendo), Hashim Rungwe (CHAUMMA) ,  Fahmi Dovutwa (UPDP), Macmillan Lyimo (TLP), Janken Kasambala (NRA) na Chief Lutalosa Yemba (ADC).

WAGENI WATAKAOHUDHURIA
Tukio hilo linatarajiwa kushuhudiwa na marais wanane kutoka mataifa mbalimbali duniani, makamu wa rais, mawaziri wakuu  na viongozi wengine.

Pia kwa mara ya kwanza Nabii na Mtume wa Kanisa la Synagogue Church of All Nations (SCOAN) la Nigeria, Temitope Balogun, maarufu kama ‘TB Joshua’, atashuhudia sherehe hizo za kihistoria.

Marais wanaotarajiwa kuwepo na nchi zao kwenye mabano ni Robert Mugabe (Zimbabwe), Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Jacob Zuma (Afrika Kusini), Joseph Kabila (DRC), Uhuru Kenyatta (Kenya), Filipe Nyusi (Msumbiji) na Edgar Lungu (Zambia).

Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima, huku Namibia ikiwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Serikali ya China kwa upande wake itawakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo (CPC), ambacho ni chama tawala.

Nchi zingine ambazo zimethibitisha kuhudhuria sherehe hizo na zitawakilishwa na makamu wa rais,  waziri mkuu,  spika au balozi ni pamoja na Burundi, Comoro, Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar na Mauritius.

Zingine ni Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli, Swaziland, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria.

Kwa upande wa wakuu wa mashirika ya kimataifa na kikanda, waliothibitisha kushiriki ni Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika  (SADC), Umoja wa Ulaya (EU), Jumuia ya Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).

Wageni hao sambamba na viongozi wakuu wa serikali, wanatarajia kuwasili kwenye uwanja wa Uhuru kuanzia saa tatu  asubuhi.

MAANDAMANO
Kitendo hicho kitafanyika baada ya kuwasili kwa wageni mashuhuri na kuingia kwa gwaride uwanjani.

Inatarajiwa Jaji Mkuu, Othmani Chande pamoja na Spika wa Bunge, Anna Makinda, wataongoza maandamano saa 4: 10 asubuhi, kuelekea kwenye jukwaa lililoandaliwa kwa ajili ya kuapishwa Dk. Magufuli na Samia.

Viongozi wengine watakaokuwepo kwenye maandamano hayo ni Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu na Katibu Mkuu Kiongozi.

Wengine ni viongozi wa madhehebu ya dini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Karani wa Baraza la Mawaziri na wazee wawili.

Hata hivyo, viongozi watakaopata nafasi ya kupanda kwenye jukwaa hilo ni Jaji Mkuu, ambaye atawaapisha Rais na makamu wake, Spika wa Bunge, Katibu Mkuu Kiongozi, Karani wa Baraza la Mawaziri, wazee wawili na viongozi wa madhehebu ya dini.

DK. MAGUFULI NA SAMIA
Makamu wa rais mteule, Samia Suluhu Hassan, atawasili uwanjani saa 4: 25 asubuhi, akifuatiwa na Rais mteule, ambaye ataingia kwenye uwanja huo wa kihistoria saa 4:30 asubuhi.

Baada ya kuwasili kwa viongozi hao wateule, wataongozwa kwenda kwenye jukwaa la kiapo.

Kama ilivyokuwa wakati wa kuapishwa kwa marais waliotangulia,  tukio hilo huwa linawavutia zaidi wananchi na kusababisha nderemo na vifijo kutawala uwanjani hapo.

Wanatarajiwa kuketi kwenye viti maalamu vilivyoandaliwa kwa ajili yao ili kusubiri kuwasili kwa rais anayemaliza muda wake, Dk. Kikwete.

KUINGIA KWA JK
Itakapofika saa 4:40 asubuhi, Rais Kikwete ataingia uwanjani akiwa kwenye gari maalumu la wazi, akiambatana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, wakisindikizwa na msafara wa pikipiki zinazokadiriwa kuwa 16.

Baada ya kuingia, atakwenda moja kwa moja kwenye jukwaa la kupokelea heshima kutoka gwaride rasmi lililoandaliwa kumuaga na kumkaribisha rais mpya, kisha litaunda umbo la Omega kuashiria mwisho wa utawala wake.

Kama ilivyoa ada kwa Amiri Jeshi Mkuu, atapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride la heshima.

Baada  ya tukio hilo la kipekee, utapigwa wimbo wa taifa, ukifuatiwa na wimbo maalumu wa kwa ajili ya kuteremsha bendera ya rais, kisha Rais Kikwete kwenda moja kwa moja kwenye jukwaa la kiapo.

KIAPO
Kufika kwa Rais Kikwete kwenye jukwaa hilo, kutatoa fursa ya kuanza kwa shughuli za kiapo kwa rais mteule na makamu wake.

Kwa mujibu wa ratiba, Dk. Magufuli ataapishwa saa tano  asubuhi na Jaji Mkuu Chande, kisha kutia saini hati ya kiapo na kukabidhiwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Cha kuvutia zaidi ni kwamba wakati huo wa kiapo, mpambe wa Rais atahama kutoka kwa Rais anayemaliza muda wake na kwenda kusimama nyuma ya Rais mpya.

Baada ya hapo, Dk Magufuli atakalishwa kwenye kigoda na kukabidhiwa ngao na mkuki kutoka kwa wazee, ambao mmoja anatoka Tanzania Bara na mwingine Tanzania Visiwani, ikiwa ni ishara ya kudumisha Muungano.

Pia, Makamu wa Rais mteule naye ataapa na kisha kusaini hati ya kiapo pamoja na kukabidhiwa Katiba.

Rais Kikwete, atampisha kiti chake kuketi Dk. Magufuli baada ya kuapishwa na kuwa rais wa awamu ya tano.

GWARIDE
Baada ya kuapishwa na kusomewa dua kutoka kwa viongozi wa madhehebu ya dini, Dk. Magufuli atakwenda kwenye jukwaa la suluti kupokea heshima na salamu za utii kutoka kwa majeshi ya ulinzi na usalama.

Sambamba na hilo, atapigiwa wimbo wa taifa, mizinga 21 na kupandishwa kwa bendera ya rais kuashiria mwanzo wa utawala wake.

Gwaride pia litaunda umbo la Alpha kuashiria mwanzo wa enzi, kisha Dk. Magufuli kulikagua na kupewa heshima kuashiria mwanzo wa serikali ya awamu ya tano na Amiri Jeshi Mkuu mpya.

Rais mpya atakwenda jukwaa kuu, kisha gwaride kupita mbele kutoa heshima kwa mwendo wa haraka na baada ya hapo litasonga mbele kwa hatua 15 kutoa salamu ya utii.
Tukio hilo litafuatiwa na ndege vita kupita na kutoa heshima kwa rais.

Baada ya hatua hiyo, itakapotimu saa 6:05 mchana, Rais huyo wa awamu ya tano atawahutubia wananchi.

No comments:

Post a Comment