NA
PETER KATULANDA, MWANZA
MAANDAMANO
ya uchochezi na uvunjifu wa amani yaliyopangwa
kufanyika jana na CHADEMA mkoani hapa, sambamba na mikoa mingine nchini,
‘yameyeyuka’ baada ya polisi kuimarisha ulinzi kila sehemu.
Kwa
mujibu wa baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliozungumza na mwandishi wa habari
hizi kwa masharti ya kutotajwa majina, mbali na polisi kuyazuia na kuimarisha
ulinzi, wameshtuka kutumiwa ovyo na viongozi wao.
“Uchaguzi
umemalizika, tunapaswa kuangalia maisha yaliyo mbele yetu, hivyo viongozi
wanaotuhamasisha kuandamana tumewaambia waje waongoze maandamano hayo, siyo
kututumia kuandamana wakati wao wako majumbani kwao,” alisema kiongozi mmoja wa
CHADEMA wa Igoma.
Mfuasi
mwingine wa chama hicho aliyekuwa katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha
Nyegezi jijini hapa, alisema viongozi walioandika barua polisi kuomba
kuandamana ili kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliomweka madarakani Rais
Mteule Dk. John Magufuli , wana matatizo ya akili kama si kutaka watoto wa
wengine wauawe.
“Kweli
tulijaribu kutaka kukusanyana asubuhi maeneo haya ya Nyegezi, lakini kwa hali
tuliyoona polisi walivyokuwa wamejipanga, nimewashauri wenzangu tuachane nayo,
vinginevyo wanaotaka tuandamane waje mstari wa mbele tufe au kuishia gerezani
wote,” alisema mfuasi huyo.
Mwingine
aliyedai ni dereva wa daladala ziendazo Igoma-Buhongwa, alisema vijana
watakaoandamana wajue kuna kupoteza uhai na viungo iwapo watazua vurugu na
kwamba vitendo kama hivyo vinawakera wananchi wengi ndiyo maana chama hicho
kimenyimwa kura na kupoteza majimbo ya Nyamagana na Ilemela.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza,
Charles Mkumbo, alisema hadi nyakati za mchana hakukuwa na wafuasi wa CHADEMA
waliokuwa wameandamana na kwamba jeshi lake lilikuwa limejipanga kukabiliana na
maandamano hayo na litaendelea kufanya hivyo.
“Maandamano
yoyote lazima yawe na maudhui, haya ni uchochezi, shari na uvunjifu wa amani. Yangekuwa
maandamano ya heri, tungeyapa ulinzi, lakini maudhui yake ni kupinga matokeo ya
uchaguzi mkuu wakati sheria za uchaguzi zipo na zinapaswa kuchukuliwa, siyo
maandamano,” alisema Mkumbo.
Bila
kutaja majina, alisema viongozi wa CHADEMA wa wilaya za Nyamagana na Kwimba,
walipeleka barua za kuomba kuandamana sambamba na maeneo mengine ya nchi kama
ilivyolipotiwa katika vyombo vya habari, lakini waliwakatalia na kuonya
wasithubutu kufanya hivyo.
Kamanda
huyo amewapongeza wafuasi wa chama hicho, hasa vijana, ambao ndiyo walengwa wa
maandamano hayo, kutii amri bila shuruti na kuwataka waendelee kujenga uchumi
wa nchi na kuinua vipato vyao kwa amani.
Alisema
jeshi lake lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wote pamoja na mali zao, hivyo
washirikiane na Watanzania wengine kudumisha amani.
No comments:
Post a Comment