HATIMAYE Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Samuel Sitta, amevunja ukimya na kutangaza rasmi kuwa wakati wa
mchakato wa kinyang’anyiro cha Spika wa Bunge la 11, atawania nafasi hiyo.
Sitta, amekuwa kada wa kwanza wa CCM kutangaza rasmi
kuingia katika mchuano wa kuwania nafasi hiyo nyeti.
Habari kutoka miongoni mwa wasaidizi wa Sitta, zimesema
spika huyo wa zamani ameamua kuwania nafasi hiyo kutokana na uwezo na uzoefu
alionao wa kuendesha Bunge.
Msaidizi huyo alisema Sitta anaamini kuwa uwezo wake
aliouonyesha katika kuendesha Bunge la Tisa (mwaka 2005 hadi 2010), akitumia
kauli mbiu yake ya 'Spika wa kasi na viwango’, itamfanya aendane na kasi ya
utendaji wa Rais Mteule, Dk John Magufuli.
Alisema Sitta ameahidi akichaguliwa kuwa Spika wa Bunge
la 11, atasimamia suala la Muungano na Umoja wa Taifa bila kuyumba.
Kuhusu Katiba mpya, alisema ameahidi atasimamia na
kuukamilisha mchakato wa Katiba Inayopendekezwa
kwa ufanisi na atasimamia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi kwa
ajili ya uchumi bora wa viwanda, kilimo, huduma na mauzo nje.
Sitta alijizolea sifa nyingi wakati akiwa Spika wa Bunge
la Tisa, ikiwamo Bunge hilo kufanyia marekebisho ya kanuni mbalimbali
zilizolifanya liwe na makali na kuibua kashfa nzito, ikiwamo ya Richmond,
ambayo ilisababisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu na alilirejeshea makali.
Tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano limetangaza kuanza
kwa mchakato wa kumpata Spika mpya wa Bunge, atakayerithi mikoba ya Spika Anne
Makinda.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, akizungumza na vyombo
vya habari mapema wiki hii, alivitaka vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu,
kuandaa watu wao watakaowania nafasi hiyo.
Alisema vyama hivyo havina budi kuzingatia kuwa mgombea
wa nafasi ya Spika, anaweza kuwa mbunge au mwanachama yeyote wa chama hicho kwa
masharti kwamba kama si mbunge, jina lake lazima liwasilishwe kwanza Tume ya
Uchaguzi siku tano kabla ya uchaguzi, kujiridhisha kuwa mgombea huyo ana sifa
za kuwa mbunge.
Mbali na kutangaza kuanza kwa mchakato wa uspika, Joel pia
aliwataka wabunge waliopo majimboni kuwasili Dar es Salaam, kuanzia jana, ili washiriki hafla ya kuapishwa kwa
Rais Mteule, Dk. John Magufuli, kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es
Salaam.
Ripoti ya tathmini juu ya utendaji kazi wa Bunge la tisa
chini ya Spika Sitta, iliyofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), inaonyesha kuwa Bunge hilo lilikuwa na ufanisi na ubunifu.
Ilisema Bunge hilo la tisa lilipata ufanisi na mafanikio
kadhaa, kutokana na ubunifu na ujasiri wa baadhi ya wabunge, wakiongozwa na
utayari wa Sitta, ambaye wakati akishika nafasi hiyo aliahidi kuwa 'spika wa
kasi na viwango.'
Mafanikio yaliyopatikana katika Bunge hilo, kwa mujibu
wa ripoti hiyo ni pamoja na kutungwa kwa kanuni mpya za Bunge za mwaka 2007,
ambazo zimeelezwa kuwa zilisaidia kwa kiasi kikubwa kuliwezesha lifanyekazi kwa
ufanisi, kama vile kuondoa ukiritimba wa serikali kuwa ndiyo pekee inayoweza
kupeleka muswada bungeni.
Kanuni hizo mpya za mwaka 2007, ambazo zilitokana na
kufanyia marekebisho makubwa kanuni za Bunge za mwaka 2004, zilitoa mamlaka kwa
Kamati za Kudumu za Bunge kuwa na uwezo wa kupeleka miswada kwa ajili ya
kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwa sheria.
Mambo mengine yaliyolipatia sifa Bunge la tisa chini ya
Sitta ni kubadili kanuni za Bunge, ambazo ziliruhusu uwasilishwaji wa hoja
binafsi bungeni na ulazima wa kamati za kudumu za Bunge kushirikisha umma
katika kujadili mapendekezo ya miswada mbalimbali.
Masuala mengine ni Kamati za Kudumu za Bunge kuwa na
uwezo wa kujadili na kuwasilisha mapendekezo yao bungeni kwa ajili ya
kujadiliwa, Bunge kuwa na uwezo wa kuanzisha kamati maalumu zilizo na uwezo wa
kuchunguza mambo kama ile iliyochunguza kashfa ya Richmond na uvunjifu wa haki
za binadamu kwa kuchafua maji ya Mto Tigiti huko Mara.
Ripoti hiyo inasema katika kutimiza moja ya majukumu
yake ya msingi ya kikatiba, Bunge hilo lilibadili na kutunga sheria kadhaa kwa
maslahi ya jamii, zilizokuwa na mtazamo wa haki za binadamu, kama vile Sheria
ya Mtoto ya 2009, Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Watu wenye Ulemavu
(2010).
Mbali ya uspika, Sitta ameshika nyadhifa mbalimbali
kuanzia katika serikali ya awamu ya kwanza hadi awamu ya nne inayomaliza muda
wake ya Rais Jakaya Kikwete.
Nyadhifa hizo ni pamoja na kuwa Waziri wa Uchukuzi,
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Katiba na Sheria,
Mkurugenzi Mkuu Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la
Katiba
No comments:
Post a Comment