Marais wanane, mawaziri wakuu
kushuhudia akiapa
Kenyatta, Kagame, Museveni,
Mugabe kuhudhuria
TB Joshua atua nchini kushuhudia,
aelezea uchaguzi
Polisi yajipanga, ulinzi
waimarishwa kila kona ya Jiji
Na Waandishi Wetu
RAIS Mteule wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kesho anakula kiapo na kukabidhiwa rasmi mikoba
ya kuliongoza taifa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye amemaliza muda wake
wa uongozi wa miaka 10.
Katika tukio hilo linalosubiriwa
kwa hamu kubwa na mamilioni ya Watanzania ndani na nje ya nchi, Dk. Magufuli ataapa
huku akishuhudiwa na marais zaidi ya wanane kutoka mataifa mbalimbali duniani, makamu wa rais, mawaziri wakuu na viongozi
wengine wa ngazi za juu.
Sherehe hizo zitafanyika katika
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa mamlaka husika, maandalizi
yote yamekamilika huku ulinzi ukizidi kuimarishwa ili kuhakikisha amani na
utulivu vinatawala.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakuu wa nchi na serikali kutoka
mataifa mbalimbali, wakuu wa mashirika ya kimataifa na kikanda na wawakilishi wa
ndani na nje watashiriki.
Miongoni mwa marais
watakaohudhuria sherehe hizo ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Yoweri Museveni
(Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Jacob Zuma (Afrika Kusini).
Wengine ni Joseph Kabila (DRC), Uhuru
Kenyatta (Kenya), Filipe Nyusi (Msumbiji) na Edgar Lungu (Zambia).
Taarifa hiyo imesema kuwa Malawi
itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima huku Namibia ikiwakilishwa na
Naibu Waziri Mkuu, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Netumbo Nandi-Ndaitwah
na kwa upande wa Serikali ya China , itawakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa
Chama Tawala.
Nchi zingine ambazo tayari zimethibitisha
kushiriki katika sherehe hizo na zitawakilishwa na makamu wa rais, waziri mkuu, spika au balozi ni pamoja na Burundi, Comoro,
Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar na Mauritius.
Nyingine ni Norway, Oman, Sudan
Kusini, Sweden, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli,
Swaziland, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana,
India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria.
Kwa upande wa wakuu wa mashirika
ya kimataifa na kikanda, waliothibitisha kushiriki ni Umoja wa Mataifa (UN),
Umoja wa Afrika (AU), Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuia ya Maendeleo ya
Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja
wa Ulaya (EU), Jumuia ya Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).
TB Joshua atua kushuhudia
MTUME TB Joshua wa Kanisa la Church of All Nations la
nchini Nigeria, amewasili jijini Dar es Salaam jana, kwa ajili ya kushuhudia
kuapishwa kwa Dk. Magufuli.
Mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, TB Joshua alikwenda moja kwa moja Ikulu,
kumsalimia Rais Jakaya Kikwete.
Katika mazungumzo yao, TB Joshua alimpongeza Rais
Kikwete kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, ambao
alisema ulifanyika kwa uhuru na amani.
Alimweleza kuwa kutokana na kufanikisha uchaguzi huo,
anaondoka madarakani kwa furaha na amani na kuwaacha Watanzania wakimkumbuka
daima.
Aidha, alimpongeza Rais Kikwete kwa kukiwezesha Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kumpata Dk. Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano, ambaye
alimwelezea kuwa ni Rais wa Baraka na Fanaka tele katika awamu hii mpya.
Polisi yaonya, yataka
amani
JESHI la Polisi limewataka wananchi kudumisha amani wakati huu, ambao Taifa
linaingia kwenye tukio muhimu la kuapishwa kwa Dk. Magufuli.
Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi,
Paul Changoja, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa, tukio hilo ni muhimu
na kwamba, ulinzi umeimarishwa kila kona.
Aliwataka wananchi kuhakikisha amani iliyokuwepo wakati
wa uchaguzi mkuu, inaendelea hata siku
zote, ikiwa ni pamoja na siku ya kuapishwa rais mteule.
Chagonja
aliwataka wananchi kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya
aina yoyote, ambavyo vinaweza kuhatarisha
usalama wa raia na mali zao.
Aliwataka kujiepusha na maandamano yanayopangwa kufanyika bila kufuata
utaratibu, vurugu na ushabiki wa kisiasa na
kueneza uvumi usio wa kweli.
Chagonja aliwataka wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii
katika kulinda amani ya nchi.
“Wananchi tuhakikishe tunaiweka nchi katika hali ya
usalama kama ilivyokuwa kipindi chote
cha uchaguzi,” alisema.
Chagonja alisema jeshi la polisi na vyombo vingine vya
usalama, vimejipanga kikamilifu
kuhakikisha usalama wa raia na mali zao
unaimarishwa.
Alisema polisi hawatasita kuchukua hatua kali kwa mtu
au kikundi chochote kitakachoonyesha viashiria vya uvunjifu wa amani.
Akizungumzia maandamano ya CHADEMA, Chagonja alisema
maandamano hayo ni batili na kwamba waliwasilisha maombi nje ya muda.
“Hatuoni haja ya kuwa na maandamano kwa sasa na kama
chama kimojawapo kinaona hakijatendewa haki, kifuate sheria kwa maana kimepewa
njia ya kufuata,’’ alisema.
No comments:
Post a Comment