Monday, 21 December 2015
MSUYA AWASHUKIA WASALITI NA WANAFIKI NDANI YA CCM
WILIUM PAUL, MOSHI
WAZIRI Mkuu mstaafu na mwanachama mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Cleopa Msuya, amewajia juu viongozi wa chama mkoa wa Kilimanjaro, kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kuwataka wajitathmini.
Aidha, ameushauri uongozi wa CCM, kuachana na viongozi na wanachama wasaliti na kwamba ni vyema kubaki na watu wachache wenye uchungu, watiifu na waaminifu kwa chama
Msuya alitoa kauli hiyo katika ufunguzi wa kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Kilimanjaro, kilichofanyika jana katika ukumbi wa Pius Msekwa, uliopo kwenye Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.
Alisema CCM imepata aibu kubwa mkoani humo kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi huo, baada ya kupoteza majimbo saba ya ubunge katika tisa yaliyopo na kuambulia mawili tu ya Same Magharibi na Mwanga.
“CCM ina viongozi wazuri kuanzia ngazi ya mkoa hadi matawi pamoja na mtaji mkubwa wa wanachama wengi, sasa mmeshindwa nini katika uchaguzi huu? Je mkoa wa Kilimanjaro CCM imeshindwa kutekeleza sera zilizolenga kuwaondolea kero wananchi wa mkoa huu? Alihoji na kuwaasa viongozi kujitafakari upya.
Alisema umefi ka wakati viongozi na wanachama wa CCM kujitathmini upya ni kwa nini wananchi wameondoa imani kwa chama, hali iliyowafanya wawaunge mkono wapinzani walionyakua majimbo ya Moshi Vijijini, Siha na Same Mashariki.
Waziri huyo alisema matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa mkoa wa Kilimanjaro si mazuri, ambapo Rais Dk. John Magufuli, alipata kura za wastani wa asilimia 38, huku mpinzani wake Edward Lowassa (CHADEMA), akipata mara mbili yake na kusema kuwa atamshangaa kiongozi wa CCM atakayeridhika na matokeo hayo na kulala usingizi mzuri.
Aidha Msuya alisema katika historia za kisiasa, matokeo ambayo mkoa wa Kilimanjaro wameyapata mwaka huu, yamemkumbusha mwaka 1995, ambapo enzi hizo Augustino Mrema, alikuwa akivuma katika medani ya siasa.
“Ingekuwa katika nchi za wenzetu matokeo ambayo mmeyapata mkoa wa Kilimanjaro, viongozi wote wangejiuzulu…si kwamba nakwambieni mjiuzulu leo, hapana, bali mnapaswa kutafakari ni wapi mmekosea na ni lazima mseme ukweli na kuwabainisha wasaliti wote,” alisema.
Awali akimkaribisha Msuya, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Idd Juma, alisema kikao hicho, kinalenga kueleza ukweli juu ya kilichotokea kwenye uchaguzi huo na kusababisha chama kishindwe kwenye majimbo mengi.
Juma alisema sababu za CCM kushindwa zinatokana na mivurugano yawanachama wake pamoja na viongozi, hivyo umefi ka wakati ambapo ukweli unapaswa kuwekwa bayana, ili mchawi ajulikane. “Tumepokea maelekezo kutoka CCM, ngazi ya taifa, yakitaka tueleze sababu za kushindwa katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kila kata, pamoja na kuwataja wasaliti wote walioko ndani ya CCM ambao baada ya uchunguzi watachukuliwa hatua,” alisema Juma.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Deogratius Rutta, alisema wajumbe waliotakiwa kuhudhuria kikao hicho ni 65, lakini waliofika walikuwa ni 48 na kudai kutokana na akidi kutimia kikao hicho ni halali na uamuzi utakaotolewa utakuwa halali kwa mujibu wa sheria.
Rutta alidai katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu, CCM ilisimamisha wagombea wazuri na wenye sifa zote zinazokubalika na wananchi, lakini katika hali ya kushangaza waliambulia majimbo mawili ya ubunge, huku mengine yakichukuliwa na wapinzani.
Aidha Rutta aliendelea kudai kuwa katika uongozi wa wenyeviti wa halmashauri, CCM imeshinda halmashauri mbili, ambazo ni Same na Mwanga, kati ya saba, huku tano zikichukuliwa na wapinzani.
CHANZO CHA HABARI: GAZETI LA UHURU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment