Tuesday 5 January 2016

BEI YA MAFUTA YASHUKA





MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imesema bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini zimeshuka katika mwezi huu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka uliopita.

Imesema bei hizo mpya za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, zitaanza kutumika rasmi kesho, maeneo yote ya nchi kwa viwango vya sh. 79 kwa lita, sawa na asilimia 4.01, sh. 76 kwa lita, sawa na asilimia 4.20 na sh. 66 kwa lita, sawa na asilimia 3.73.

Vilevile kwa kulinganisha na bei za Desemba, mwaka jana, EWURA imesema bei za jumla kwa mafuta ya petroli, dizeli na ya taa nazo zimepungua kwa sh. 79.19 kwa lita, sawa na asilimia 4.23, sh. 76.49 kwa lita, sawa na asilimia 4.45 na sh. 65.86 kwa lita, sawa na asilimia 3.97. 

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi, ilisema kupungua huko kwa bei za mafuta, kwa kiasi kikubwa kumetokana na kushuka kwa  bei za mafuta katika soko la dunia na pia kushuka kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa za mafuta kuja nchini.

Taarifa hiyo ilisema kulingana na Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, hivyo EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta kwa lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa hizo.

Kupitia taarifa hiyo, Ngamlamgosi alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo kama ilivyokokotolewa na mfumo uliopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 405/2015 la Julai, 2015.

Aidha, taarifa hiyo imevielekeza vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za mafuta katika mabango, ambayo yataonyesha bei, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika na kwamba pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.

Taarifa hiyo ilitahadharisha kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika.

Pamoja na hayo, wateja wameshauriwa kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

Stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.

No comments:

Post a Comment