Tuesday 5 January 2016

DK. MWAKYEMBE AWASHA MOTO





NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harison Mwakyembe, amesema sekta ya sheria imegubikwa na majipu sugu yanayohitaji kupasuka yenyewe kabla Rais Dk. John Magufuli hajayatumbua kwa uchungu.
Ametahadharisha kuwa majipu makubwa na vijipu uchungu, visisubiri kutumbuliwa bila ganzi kwa kuwa hayuko tayari kuonekana mzembe kwa kucheka na wala rushwa, wanaoathiri utendaji kazi wa serikali katika kutoa haki kwa wananchi.
Aidha, Dk. Mwakyembe amesema mchakato wa kuundwa kwa mahakama ya mafisadi, ulioahidiwa na Rais Magufuli wakati wa kampeni, bado upo pale pale kwa kuwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Waziri huyo wa katiba na sheria, pia ameahidi kumuunga mkono kikamilifu Dk. Magufuli katika kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya ili Tanzania iwe na katiba bora yenye kukidhi mahitaji ya wananchi
Dk. Mwakyembe alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kukutana kwa zaidi ya saa tatu na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga pamoja na vigogo wengine wa sekta hiyo.
Katika kikao hicho kilichofanyika ofisini kwa DPP, mjini Dar es Salaam, Dk, Mwakyembe na Mganga, walijadili kwa kina kuhusu mikakati ya utendaji kazi mpya wenye tija katika serikali ya awamu ya tano.
Dk. Mwakyembe alisema  utendaji haki unagusa maisha ya wananchi, hivyo ubora wa huduma ni muhimu.
“Utendaji kazi wenu sasa uwe karibu na wananchi kwa kuwa hakuna siri, makarani, washauri, mahakimu, wasimamizi wa magereza ni tatizo, hivyo mjitambue kuwa ni sehemu ya serikali, mkitetereka mnatutia dosari na kwa sasa mko rehani,”alisema.
Alisema utoaji huduma wa haki kwa wanasheria, polisi, majaji una vijipu uchungu, ambavyo havivumiliki na kamwe hawezi kuwavumilia, hivyo kabla Rais Dk. Magufuli hajavitupia jicho na kuvitumbua bila ganzi, atahakikisha amevisafisha vya kutosha.
“Rushwa ni jipu kubwa linaloudhi serikalini na wananchi wanajua toka uhuru na tangu uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, kuwa jipu hili ni adui wa haki. Uzuri mimi waziri wenu pia ni mwanasheria na wengi wenu ni wanafunzi wangu, hapa tuache kujipa matumaini, sasa ni kazi tu na kila mtu ajisafishe leo, asingoje kesho maana ameshachelewa,”alisema.
Aliongeza: “Wanasheria tunajijua, ni mafundi wa kujiliwaza kwa kuwa tunajidanganya na vifungu vya sheria. Sasa mtambue kampeni ya serikali ya awamu ya tano ni kusafisha uchafu serikalini na rais wetu amejitoa mhanga kubadili nchi,”alisema.
Aliwataka watendaji wa sekta hiyo kutambua kuwa atakayechukuliwa hatua, asitarajie wananchi watampa nafasi ya kujitetea kwa kuwa wamechoshwa na vyombo vinavyotoa haki kuwa sehemu ya ubadhirifu.
Alisema hakuna vyombo vya serikali vinavyoweza kubadili mfumo wa uozo kama vyombo vya sheria kwa kuzingatia maadili katika uandaaji mashitaka na hukumu.
Dk. Mwakyembe alisema anaelewa mazingira magumu ya kazi za mawakili wa serikali, kwa kuwa mawakili binafsi wana malipo makubwa, hivyo wakati serikali inajipanga kuiwezesha sekta hiyo, lazima kufumuliwa  wachache walio wachafu ili wakae pembeni.
“Watanzania wamechoka, wanataka mabadiliko, mchezo wa kuchelewesha mafaili mahakamani kwa makusudi, kubambikia watu kesi, sasa basi. Ubora wa huduma unaeleweka, hivyo badilikeni haraka, wengi humu ni wachafu na mimi sipo tayari kusubiri hatua za Dk. Magufuli,”alisema.
Alimuahidi DPP Mganga kuijengea uwezo ofisi hiyo katika kukabiliana na kesi za dawa za kulevya kwa kuwa ni changamoto kubwa kwa serikali.
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, Dk. Mwakyembe aliwatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa, Rais Magufuli ndiye msemaji wa mwisho wa serikali na amelizungumzia jambo hilo mara kwa mara, kwamba ni kiporo alichoachiwa katika serikali awamu ya nne.
Alisema kutokana na ahadi za Dk Magufuli katika kufanyiakazi mchakato wa katiba mpya, atahakikisha anamuunga mkono kikamilifu ili Tanzania iwe na katiba bora yenye kukidhi mahitaji ya wananchi.
Pia, alisema mchakato wa kuundwa kwa mahakama ya mafisadi upo pale pale na muda mfupi ujao majibu yatapatikana.
“Mahakama ya mafisadi ni suala lililo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na imebaki utekelezaji, muda mfupi ujao majibu yatapatikana,”alisema.

No comments:

Post a Comment