Tuesday 12 January 2016

CCM YAJIPANGA UPYA MONDULI




CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Monduli, kimetangaza vita dhidi ya mapandikizi na mamluki ndani na nje ya CCM, wanaotumiwa na vyama vya upinzani.
Mapandikizi hayo yamekuwa yakitumiwa kuhujumu mikakati ya CCM pamoja na kuwagombanisha viongozi na wanachama.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Arusha, Paul Kiteleki, alisema hayo jana, wakati wa kikao cha viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya, wakiwemo madiwani tisa walioshinda kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Lotha Sanare na Namelok Sokoine, ambapo ilielezwa bayana kuwa kiama cha wasaliti kimefika.
“Hatuko tayari kuona CCM Monduli ikisarambatika kwa sababu ya watu wachache. Mnavaa rangi za kijani, lakini mnafanya kazi za UKAWA. Mbele yenu mnawaona Namelock na Lotha, makada hawa walikuwa mahasimu wakubwa, lakini kwa sasa tofauti zimeisha na ni kitu kimoja. Tunataka heshima ya CCM irejee,” alisema.
Aliweka bayana kuwa ndani ya kikao hicho wapo wanachama, ambao walitumwa kurekodi kila kinachoendelea na kumpelekea ‘Mzee’, ambaye hata hivyo hakumtaja jina.
Akitoa tamko kwa niaba ya viongozi hao, Lotha, ambaye amejitosa kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM wilaya ya Monduli, alimtaka aliyekuwa  mbunge wa jimbo hilo, Edward Lowassa, kuachana na siasa za Monduli na kumtaka atulie nyumbani kwake.
“Hatutakiwi kuwaacha wasaliti watambe ndani ya CCM. Lowassa tulimuamini na tukampa heshima, lakini ameshindwa kuithamini na kukimbilia upinzani. Amechepuka mwenyewe, sisi tumebaki njia kuu, hivyo nimuombe tu akae nyumbani  kwake atulie, atuachie CCM yetu.
“Nimefarijika kumaliza tofauti zetu na Namelock, ambazo zilisababishwa na watu wanaopenda kufitinisha. Sasa tuna kazi moja tu ya  kuimarisha CCM Monduli,” alisema.
Naye Namelock alisema alikaa na kutafakari kwa kina baada ya uchaguzi na kuona, hana sababu ya kugombana  na Lotha, hivyo alilazimika kumfuata na kumuomba radhi kama kaka yake kwa kutumia njia za kabila lao la kimasai.
“Nimetafakari nikaona hakuna haja ya kugombana na kaka yangu. Tulikuwa na mgogoro mkubwa kipindi cha kampeni za ubunge, lakini hakuwa na kinyongo, aliniombea kura,” alisema.
Baada ya kikao hicho, wajumbe waliwasindikiza Namelok na Lotha katika ofisi ya Katibu wa CCM Wilaya kurudisha fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti na Namelock aliyekuwa akirejesha  fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa  Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.

No comments:

Post a Comment