Tuesday 12 January 2016

MASAUNI AWAONYA MAOFISA UHAMIAJI





NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amewataka maofisa uhamiaji kutotumia nafasi ya kukamata wahamiaji haramu kinyume na matakwa ya serikali pamoja na sheria za nchi.
Aliyazungumza hayo katika ofisi kuu ya Uhamiaji, Zanzibar, iliyoko eneo la Kilimani, alipofanya ziara ya kikazi ili kujionea shughuli za utendaji wa ofisi hiyo.
Alisema serikali chini ya Idara ya Uhamiaji, itapambana na wahamiaji waliopo nchini bila vibali ama kufuata kanuni na sheria zinazoruhusu ukaazi wao na si vinginevyo.
Alisema wageni wote wenye vibali vinavyowaruhusu kuwepo nchini, hawatabugudhiwa kwa namna yoyote ile, na kwamba yeyoye atakayebainika kunyanyasa wageni hao wenye vibali, atachukuliwa hatua za kinidhamu.
“Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani kote, tunapenda wageni, tunajua kwamba watalii na wawekezaji waliopo nchini wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa taifa letu, hivyo hatuwezi kuwafukuza ama kuwanyanyasa kama wako nchini kihalali,” alisema Masauni.
Aidha, amewataka maofisa wa uhamiji kutotumia zoezi hilo la kubaini wakaazi haramu kwa manufaa yao na yeyote atakayebainika kutumia zoezi hilo kinyume na agizo la serikali, atashughulikiwa kwani serikali haijapanga kuonea wala kunyanyasa mtu yeyote.
Naibu waziri huyo aliongeza kuwa sheria zilizopo nchini ni kwa ajili ya manufaa ya nchi, hivyo ni lazima kila mtu aziheshimu na kuwa serikali haina lengo la kutumia sheria hizo kukandamiza wageni.
Pamoja na hayo, Masauni alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kutatua kero za wananchi, hivyo Idara ya Uhamiji itaendelea kuwatumikia wananchi kwa weledi wa hali ya juu na kuhakikisha kero zote za awali zinatatuliwa.

No comments:

Post a Comment