Monday 25 January 2016

WALIOPIMA MOYO WENGI WAGONJWA

UMATI mkubwa wa watu kujitokeza na wengine kulia, wakitaka kupewa huduma ya upimaji wa moyo, ni miongoni mwa mambo yaliyojitokeza kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar es Salaam.

Katika upimaji huo, ilibainika kuwa wananchi wengi waliojitokeza wana matatizo ya moyo na shinikizo la damu na hawakuwa wakijijua, hivyo baadhi yao walilazimika kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Kujitokeza kwa idadi kubwa ya watu, kulisababisha madaktari kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MMH) kuelemewa.

Kutokana na kuzidiwa kwa madakatri hao, waliamua kuwashauri watu waliojitokeza kupima moyo kwenda Muhimbili, lakini wananchi hao walipinga kwa madai kuwa wakienda huko hawapatiwi huduma, kuna usumbufu na gharama ni kubwa.

Daktari Bingwa wa Moyo na Mkuu wa Idara ya Utafiti kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk. Pedro Palangyo, amesema upimaji huo ulikuwa wa siku moja, lakini kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza, iliwalazimu kuongeza siku moja ili kumalizia waliofika juzi.

Hata hivyo, alisema changamoto imekuwa kubwa na madaktari kuzidiwa baada ya matarajio kuwa ni kuhudumia wagonjwa 1,800, ambapo jana walikwenda kumalizia wagonjwa 1,200 wa juzi.

Dk. Palangyo alisema walijikuta wakiwa na wakati mgumu baada ya kujitokeza wagonjwa wengi zaidi wapya.

“Hata hivyo, tukaona busara tuongeze siku ili tuweze kuhudumia hata wagonjwa 2,700. Sasa cha ajabu ukitoa hao 2,700, bado kuna 900, tena wamezidi na watu wanaendelea kufika. Cha kufanya hatuna na kila mmoja analia, anataka huduma, hatuelewi tufanye nini maana tumewaondoa hadi wale wenye bima, tunawambia waje Muhimbili, hawataki wanasema huko kuna usumbufu, hawapati huduma,”alisema Palangyo.

Alisema  kwa mazingira waliyonayo, uwezo wa kuhudumia wananchi wote hao hawana, hivyo wamejadiliana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ili kazi hiyo iweze kurudiwa hivi karibuni.

Daktari huyo alisema kutokana na tukio hilo wamebaini kiu ya masuala ya afya kwa jamii ni kubwa kwa kuwa wengi wanaihitaji na hawaamini kupata huduma bora Muhimbili huku suala la gharama kubwa ya matibabu hayo na umaskini unaowakabili wananchi wengi likiwa ni tatizo.

“Wapo ambao tumewaanzishia dawa na ambao tunawabadilishia baada ya kuona wanatumia dawa, ambazo sio stahiki na wananchi wengi tumegundua mioyo yao imetanuka, hivyo elimu zaidi ya lishe na mazoezi inahitajika kwa kuwa unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara ni sababu kubwa,”alisema.

Kwa upande wake, Makonda alisema ameshangaa kuona mwitikio umekuwa mkubwa hadi kwa wananchi walio nje ya Manispaa ya Kinondoni na juhudi za kuhakikisha wanawafikia wengi zaidi zinahitajika, ikiwemo wafadhili kujitokeza.

Alisema kutokana na gharama kubwa za matibabu hayo na wananchi wengi kugundulika kuwa na matatizo, ipo haja upimaji huo kurudiwa hivi karibuni.

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya watu wakifika kupata huduma wakiwa na magari yao, huku wengine wakiwa wamebeba vyakula na familia zao, wakiwemo watoto na kulala katika mikeka wakisisitiza hawataondoka hadi wapatiwe huduma.

Mkazi wa Kibaha, Bakari Salehe, alisema aliposikia matangazo hayo, alifika juzi, saa 11:00 asubuhi katika viwanja hivyo, lakini mwitikio wa watu na foleni aliyoikuta ilimlazimu kurudi tena jana na kupata huduma.

Mbali ya mkazi huyo, wengine waliojitokeza walitokea mikoa ya jirani ya Morogoro na Tanga.

Salehe, alisema kutokana na gharama na usumbufu wanapokwenda hospitali, hakuna ambaye yupo tayari kuondoka Leaders bila kupatiwa vipimo na matibabu, hivyo wanaiomba serikali iwasaidie.

Mwajuma Noti, aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni kupitia UMD, alisifu juhudi hizo na kushukuru kupata huduma kwa kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiteseka bila kujua ugonjwa alionao.

No comments:

Post a Comment