Saturday 6 February 2016

JK: SIKU ZA MAMLUKI NDANI YA CCM ZINAHESABIKA



MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amesema siku za mamluki ndani ya Chama zinahesabika na kwamba muda wowote wataondolewa.

Amesema Chama hakiwezi kuendelea kuwalea wanachama wa aina hiyo kwa sababu ni wasaliti na wanaweza kukibomoa badala ya kukijenga.

Aidha, Rais huyo wa awamu ya nne wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amevibeza vyama vya upinzani kwa kusema vitaendelea kuisoma namba kwa vile havina uwezo wa kuing'oa CCM madarakani.

Kikwete amesema hayo leo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Namfua, mkoani Singida.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na serikali, akiwemo Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Dk. Phillip Mangula, Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wanachama wa CCM na wananchi wa mkoa wa Singida, Kikwete alisema Chama kimekuwa kikisimamia mageuzi, mapinduzi na mabadiliko ya kweli na si ya kuzungusha mikono hewani.

Alisema mafanikio ya CCM yanatokana na misingi mizuri ya waasisi wa vyama vya TANU na ASP na pia kuwa na viongozi wanaoendeleza misingi hiyo na kuweka mbele maslahi ya Chama.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema uchaguzi mkuu wa mwaka jana, umetoa funzo kubwa kwa wana-CCM kwamba Chama kinapaswa kuwekwa mbele na mtu afuate baadaye.

"Mtu hata awe na sera nzuri kiasi gani au awe mkubwa, hapaswi kuwa na umuhimu ndani ya Chama. CCM inapaswa kuwa kubwa kuliko mwanachama,"alisema.

Aliwapongeza wanachama walioamua kuvunja makundi baada ya uteuzi wa mgombea urais licha ya kujitokeza kwa wasaliti wachache, ambao hawakuwa wakikitakia mema Chama.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa mwanzo mzuri alioanza nao katika kuiongoza serikali ya awamu ya tano na kuongeza kuwa wananchi wameonyesha imani kubwa kwake na kumuunga mkono.

Alimuahidi Rais Magufuli kwamba Chama kitaendelea kuwa naye bega kwa bega katika kila analolifanya na kumpongeza kwa kuanza kwake vizuri kuiongoza serikali ya awamu ya tano na kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Aliwataka wana-CCM kuutumia uchaguzi mkuu wa chama mwakani kuchagua viongozi makini watakaokijenga na kukiimarisha ili kiwe na nguvu na kuendelea kuongoza dola kwa miaka mingi zaidi.

Alisema kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2020, hivyo wanachama na viongozi  hawapaswi kubweteka.

Alisema huu ni wakati mwafaka kwa viongozi wa CCM waliopo madarakani kwa miaka mingi, kujiweka pembeni na kutoa nafasi kwa wengine wapya kukiongoza chama.

"Tuwaondoe viongozi wenye sifa mbaya na wanaotumia madaraka yao vibaya na wale wenye nongwa, ambao wakishindwa kwenye uchaguzi, wanahama Chama,"alisema.

Akizungumzia kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar, Kikwete alisema ni kinyume na matarajio ya wana-CCM kwa vile walishajiandaa kushinda.

Alisema kwa vile Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ilifuta uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa dosari nyingi, CCM ililazimika kukubaliana nayo kurudia uchaguzi huo kwa shingo upande.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wanachama wa CCM visiwani Zanzibar, kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya uchaguzi huo wa marudio, uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwapigia kura wagombea wa CCM.

Alisema wanachama wa CCM wa Tanzania Bara wapo bega kwa bega na wenzao wa Zanzibar katika shida na raha, mvua na jua ili kuhakikisha ushindi unapatikana.

Mwenyekiti huyo wa CCM alitumia fursa hiyo kuelekezea furaha yake kuona kuwa, anashiriki sherehe ya mwisho ya kuzaliwa kwa CCM akiwa katika mkoa wa Singida, ambako ndiko alikoanzia kazi mwaka 1974 akiwa katibu wa TANU.

Akiwasalimia wananchi katika mkutano huo, Rais Magufuli alisema serikali yake itaendeleza vita ilivyoanza navyo dhidi ya mafisadi na wala rushwa kwa lengo la kuwakomboa wanyonge.

Mapema Katibu Mkuu wa CCM, Kinana alimpongeza Kikwete kwa kuiongoza vyema serikali ya awamu ya nne ikiwa ni pamoja na kuiletea sifa kubwa nchi kimataifa.

Aidha, alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa aliyoanza kuifanya ya kutekeleza Ilani ya CCM kwa umakini na weledi mkubwa na hivyo kurejesha imani kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment