Tuesday 8 March 2016

CHADEMA KINA UBIA NA MAJIPU





MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani, ameuvaa uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiutuhumu kuwa una ushirika na wahujumu uchumi na baadhi ya watumishi ambao ni majipu.
Amesema hatua ya chama hicho kujaribu kuwatetea watumishi wanaokwenda kinyume na maadili na wabadhirifu wa mali za umma ni ishara ya kupoteza mwekeleo na sifa ya kuwa chama cha siasa.
Amemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, kukaa kimya wakati serikali ya Dk. John Magufuli ikiendelea kutimiza wajibu na ahadi zake kwa Watanzania kama ilivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
“Chama na wagombea wake kiliahidi huduma bora kwa wananchi bila kujali itikadi. Pia, kiliahidi kupambana na rushwa na ufisadi na ndio sababu majipu yameendelea kutumbuliwa bila kujali jina, cheo wala rangi ya mtu.
“Nidhamu kwa baadhi ya watumishi wa umma imeshuka sana na kusababisha malalamiko kwa wananchi. Sasa Dk. Magufuli ameamua kuirejesha ili nchi isonge mbele kwa mafanikio na Watanzania wafurahie matunda,” alisema Dk. Kamani.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kuendelea na mchakato wa kutumbua majipu kwa watumishi na watendaji wasio waadilifu, ambao wamekuwa wakiipaka matope kwa kufanya mambo yanayokwenda kinyume na matarajio ya wananchi.
Kauli ya Dk. Kamani imetokana na shutuma za Mbowe kwa serikali wakati akijaribu kuwatetea watumishi wa umma wanaowajibishwa na serikali kutokana kukiuka maadili, akidai ni ukiukwaji wa haki za binadamu, utawala bora na demokrasia jambo ambalo si sahihi.
Alikuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Meatu mkoani hapa, ambapo alimtaka Mbowe kukaa kimya na kwamba, huenda chama hicho kwa sasa kinashirikiana na wahujumu uchumi.
"Jamani wananchi tuwapuuze hawa watu kwani wameishiwa hoja…. hizo haki za binadamu zinatakiwa kuwalinda watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu, ambao wamekuwa wakisababisha hadi vifo kwa wananchi wanaohitaji huduma?” Alihoji.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona kiongozi mkubwa wa chama cha siasa akiibuka na kutetea genge la wezi wa mali za umma na watumishi wasiokuwa waadilifu, wakiwemo waliokwapua mamilioni  ya fedha za serikali, jambo  ambalo linadhihirisha kuna ushirika na chama hicho.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye yuko ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, alisema kazi ya utumbuaji majipu itaendelea hadi kieleweke na kuwataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria.
Alisema mtumishi atakayekwenda kinyume na maadili ya utumishi, ni vyema akajiondoa mapema na kwamba, atashughulikiwa papo hapo.
Pia, alisema wanachokifanya ni utekelezaji wa Ilani, ambayo inazielekeza serikali zake kufanya jitihada za kuinua uchumi na kuongeza huduma za jamii, ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa katika taasisi za umma kwa kuchukua hatua kali na za haraka kwa wale wote watakaobainika kuendeleza rushwa nchini.
"Ilani inatuagiza kuchukua hatua kali na za haraka kwa wale wote watakaobainika kuendeleza rushwa serikalini, katika sekta binafsi na kuimarisha vyombo na taasisi zinazohusika na kuzuia na kupambana na rushwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mahakama  Maalumu kwa ajili ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi," alisema Majaliwa akinukuu sehemu ya Ilani.
Alisema sambamba na kupambana na tatizo la rushwa, pia Ilani inaitaka serikali kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka, ukiukwaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa umma, kuchelewesha kutoa maamuzi yenye maslahi kwa umma na kusimamia uwajibikaji katika kutekeleza masuala yenye maslahi kwa umma.
Alisema serikali imejipanga kutekeleza Ilani kwa vitendo, lengo likiwa ni kuhakikisha inaboresha huduma kwa wananchi wake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyao, makabila yao, nyadhifa zao pamoja na hali zao za kiuchumi, hivyo mchakato wa utumbuaji majipu ni endelevu.

No comments:

Post a Comment