Tuesday 8 March 2016

WAFANYAKAZI 597 WAFUTWA KAZI NIDA, WENGINE 802 WACHUNGUZWA KUBAINI MAJIPU





Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Modestus Kipilimba
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imetangaza kusitisha mikataba ya wafanyakazi 597, katika ofisi zake nchi nzima kutokana na kutokuwa na ufanisi.
Wafanyakazi hao ni wale walioajiriwa kwa ajira za mikataba huku ikitangaza kuanza kuwachunguza watumishi wake wengine 802, ambao ajira zao ni za kudumu.
Hatua hiyo inalenga kuikwamua mamlaka hiyo kuondokana na mzigo mzito wa kuwalipa watumishi, ambao ni wengi kuliko idadi halisi inayohitajika katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku kuwahudumia Watanzania.
Pia, NIDA imetangaza kuchunguza mikataba yote, ambayo mamlaka imeingia na kampuni ama watu binafsi, kuona iwapo ina tija na itakayobainika kuwa ya kinyonyaji, itavunjwa mara moja.
Kufutwa kazi kwa watumishi hao ni mwendelezo wa hatua za kuisafisha NIDA, zinazochukuliwa na serikali ya Rais Dk. John Magufuli, ambapo tayari alishamng’oa Mkurugenzi Mkuu wake, Dickson Maimu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Modestus Kipilimba, alisema idadi ya watumishi iliyopo haiendani na uzalishaji wa vitambulisho, ambavyo vinatakiwa kutengenezwa.
Amesema kuwa NIDA ina jumla ya wafanyakazi 1,399, wakiwemo wa kudumu na mikataba, lakini vitambulisho inavyozalisha kwa siku ni 1,200 tu badala ya 24, 000.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Kipilimbi alisema uongozi umelazimika kuchukua uamuzi mgumu wa kusitisha mara moja ajira zote 597, za mikataba kwa kuanzia na baadaye itachunguza zaidi watumishi waliobaki.
“Nina muda mfupi sana tangu nimepewa kukaimu nafasi hii, lakini nimegundua mambo mengi ambayo hayako sawa hapa NIDA. Tuna wafanyakazi wa mikataba 597 na wa kudumu 802, lakini tunazalisha vitambulisho 1,200 kwa siku wakati idadi halisi tunayotakiwa kuzalisha ni 24,000.
“Hili ni tatizo kubwa, huwezi kuwa na idadi kubwa ya watumishi kuliko bidhaa unayozalisha, sasa tumeona tuanze na hawa 597 na tutakuja kwa hawa wengine kuona kama uwepo wao una tija kwa mamlaka.
“Ukiangalia utaona hakuna ufanisi kabisa, yaani ni sawa na kila mfanyakazi kuzalisha kitambulisho kimoja kwa siku,” alisema Dk. Kipilimbi, ambaye alikabidhiwa nafasi hiyo Febrauri 15, mwaka huu, baada ya Maimu kutumbuliwa jipu.
Alisema kusitishwa kwa mikataba hiyo kutatoa fursa kwa mamlaka kujipanga upya ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kufikia malengo, ambayo serikali na Watanzania wanayatarajia.
Alisema malengo ya NIDA ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata vitambulisho na kwamba, kasi ya kutoa vitambulisho itaongezwa maradufu.
Aliongeza kuwa anataka kuona kila mtumishi ndani ya NIDA analipwa kulingana na kazi anayoifanya na kwamba, wasiostahili wataondolewa haraka.
“Hawa wafanyakazi wenye mikataba ya kudumu tutawangalia kwa umakini mkubwa kubaini kama wanastahili kuendelea kuwepo ama kuondolewa.
“Tukibaini kuna watumishi ambao hawastahili kuwepo hapa, tutawarudisha utumishi huko watafahamu ni wapi kwa kuwapeleka. Tunataka kufanya kazi na tutakuwa tayari kuwa na watu wanaofanya kazi.
“Tunapenda watu wawe na ajira, lakini kama huzalishi inavyotakiwa, huna sababu ya kuwepo…tutaendelea kuhakiki hadi hapo tutakapojiridhisha,” alisema.
Kuhusu uboreshaji wa huduma zake, alisema NIDA inatarajia kupata mashine 3,000 kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambazo kwa sasa zinafanyiwa marekebisho ili kuongeza kasi ya utoaji wa vitambulisho.
Aidha, alisema  uhakiki utakwenda sambamba na kupunguza gharama kwa kubaki na watumishi wachache na kufunga ofisi zake katika maeneo mbalimbali ili kuanza kushirikiana na halmashauri nchini.
Alisema hakuna sababu ya kuwa na ofisi nyingi zilizotapakaa kila mahali na kwamba, maofisa wake watakuwa na ofisi kwenye majengo ya halmashauri nchini, ambako shughuli zote zitafanyika huko kama kawaida.
Mikataba mibovu
Kuhusu mikataba mbalimbali, Dk. Kipilimbi alisema NIDA imeingia mikataba mingi na mingine ni mikubwa, hivyo ni lazima kujiridhisha iwapo yote ina tija na maslahi kwa mamlaka.
Alisema uchunguzi na uhakiki wa mikataba hiyo utaanza mara moja na kwamba, itakayobainika inainyonya mamlaka, itafanyiwa marekebisho ama kuvunjwa kabisa.
“Mamlaka imeingia mikataba mingi ambayo ni lazima tujiridhishe kama iko sawa, sasa tukibaini haina tija kwetu, tunaomba ushauri wa kisheria kwa mamlaka zingine ili kuondokana nayo haraka,” alisema.
Hata hivyo, mikataba ambayo huenda ikaibua majipu ni ile, ambayo NIDA imeingia kukodisha majengo kwa ajili ya ofisi zake katika maeneo mbalimbali nchini.
Miongoni mwa majengo hayo yapo maghorofa ambayo yanatumika kama ofisi za NIDA, yanayotajwa kumilikiwa na vigogo, wakiwemo wanasiasa, yanayogharimu mamilioni ya shilingi kama kodi ya pango.

Sahihi za vitambulisho
Kuhusu vitambulisho vingi kutokuwa na sahihi, Dk. Kipilimbi alisema hilo linaendelea kufanyiwa kazi na kwamba, vitaboreshwa zaidi na kwamba kwa sasa vinaweza kuendelea kutumika kwa waliokwishachukua.
Alisema vitambulisho vitakavyoanza kutolewa kwa sasa vitakuwa na sahihi ya mtoaji na mmiliki na kuwa, vilivyokwishatolewa vitarudishwa na wahusika kupewa vingine vya kisasa.
“Vitambulisho vipya vitakuwa na sahihi ya mmiliki na mtoaji, hivyo wananchi wasiwe na shaka kabisa…kwa waliokwishachukua tutaandaa utaratibu wa kuvikusanya na kuwapatia vingine. “Hili tutatangaza, lakini kwa sasa wanaweza kuendelea kutumia walivyonavyo kwa kuwa vinatambulika kisheria, wasifanye haraka,” alisema.

No comments:

Post a Comment