Wednesday 16 September 2015

AUNT EZEKIEL: WASANII RUDINI CCM




NA SOPHIA ASHERY
WASANII wa filamu nchini, Aunt Ezekiel na Raymond Kigosi ‘Ray’, wamejiunga na kundi la wasanii wanaomsapoti mgombea wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Joh Pombe Magufuli.
Aunt na Ray waliokuwa katika kundi la wasanii wa UKAWA, walitangaza kurudi CCM juzi jioni na kusema huko walikokuwa hawajaona sera ambazo zina mashiko kwa nchi.
Aunt aliandika katika ukurasa wake waTwitter na kusema anawaomba Watanzania kuungana na kuleta mabadiliko bora Tanzania kupitia mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli na si mgombea mwingine yeyote.
“Nawaomba wasanii wengine ambao mpo huko na mnatamani kurudi CCM japo mnaona aibu mtoroke mrudi nyumbani msipoteze muda wenu,” alisema Aunt.
Msanii huyo alisema huu ni wakati wa kuweka uzalendo kwa nchi kwanza ikiwa ni pamoja na kuinadi ilani ya CCM ambayo ni ilani pekee yenye kuonyesha vipaumbele vya maendeleo ya nchi yetu.
“Kwa siku 39 za kampeni zilizobaki nitaongea na mamilioni ya mashabiki wangu kuhusu msimamo wangu wa kuondoka huko nilikokuwa na kurudi nyumbani kumuunga mkono Magufuli,” alisema Aunt.
Nyota huyo alisema anapenda mabadiliko lakini mabadiliko yaliyo bora yenye viongozi waliojipanga vizuri, wenye busara na wasiokuwa na mambo ya kificho wapo CCM.
Alisema Watanzania wana nafasi kubwa ya kupata mabadiliko kupitia Magufuli na Watanzania wanahitaji viongozi wa aina ya Magufuli kwani ni mtu anayeeleweka.
Naye Ray alisema ameamua kurudi CCM kwani hajaona sera wala vitu vya msingi ambavyo vinaelezwa na wapinzani kwa ajili ya kuiletea Tanzania  maendeleo.
“Sijaona kitu zaidi ya maigizo ambayo yanazidi hata maigizo ambayo sisi wasanii tunafanya hivyo nimeona nisipoteze muda wangu kwa kuamini mambo ambayo hawawezi kufanya hata kwa kwa miaka 10,” alisema Ray.

No comments:

Post a Comment