Tuesday 8 March 2016

KIJAZI: NATAKA HESHIMA, UADILIFU KWA WATUMISHI




KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ameonya kuwa kasi ya utumbuaji majipu itaendelea na kusisitiza imelenga kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma.
Amesema kamwe watumishi hawapaswi kutekeleza majukumu yao kwa kusukumwa, hivyo atasimamia kikamilifu vipaumbele vya serikali ya awamu ya tano katika kupambana na rushwa, ufisadi pamoja na uwajibikaji kwa watumishi.
Balozi Kijazi, ambaye awali alikuwa Balozi wa Tanzania nchini India, aliyasema hayo jana, muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo na Rais Dk. John Magufuli.
Baada ya Dk. Magufuli kumuapisha jana, Ikulu Dar es Salaam, Balozi Kijazi anakuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa nane kushika wadhifa huo katika historia ya nchi tangu mwaka 1962.
Makatibu hao ni Dustan Omari (1962-1964), Joseph Namata (1964-1967), Dickson Nkendo (1967-1974), Timothy Apiyo (1974-1986), Paul Rupia (1986-1995).
Wengine ni Marten Lumbanga (1995-2006), Philemon Luhanjo (2006-2011) na Balozi Ombeni Sefue (2011-2016).
Balozi Kijazi alisema, atafanyakazi kwa karibu kuhakikisha vipaumbele vilivyowekwa vinafikiwa, ikiwemo kusimamia utendajikazi kwa watumishi wa serikali.
Aliongeza kuwa atamsaidia Dk. Magufuli katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuandaa vikao vya Baraza la Mawaziri na kushirikiana pamoja na viongozi wengine wakuu wa serikali.
Alivitaja vipaumbe ambavyo amejikita katika kufanikisha vinatekelezwa kama, ambavyo rais anavyohitaji kuwa ni kuongeza uwezo wa serikali kwenye makusanyo ya kodi, kupambana na rushwa na kurejesha nidhamu ya utendaji kwa watumishi wa umma.
Awali, Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake, Balozi Ombeni Sefue, alimshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kumwezesha kutumikia nafasi hiyo katika kipindi chake cha utumishi.
Pia, alimshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo mwaka 2010, wakati alipokuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa (UN).
Alisema licha ya kutumikia serikali ya awamu ya nne iliyomaliza muda wake, lakini Rais Dk. Magufuli alimwamini na kuendelea na wadhifa huo kwa kipindi cha miezi mitatu.
“Baada ya kumalizika kwa awamu ya nne ya serikali, sikuwa na ulazima wa kuendelea, lakini rais aliona ni vyema nibakie kushirikiana naye kwenye masuala mbalimbali,” alisema Balozi Sefue, ambaye atapangiwa majukumu mengine.

WASIFU WA BALOZI KIJAZI  
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Kijazi alikuwa Mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal, mwenye makazi yake jijini New Delhi, India, kuanzia mwaka 2007.
Vilevile, hadi uteuzi wake, Balozi Kijazi amekuwa Mkuu wa Mabalozi wa Afrika nchini India.
Akiwa nchini humo, alikuwa mtetezi mkuu wa wanafunzi wenye asili ya Kiafrika katika masuala mbalimbali, hususan yaliyohusiana na vitendo vya unyanyasaji.
Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006.
Baadaye aliteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India.
Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, Balozi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya wizara hiyo.
Balozi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.

No comments:

Post a Comment