Friday 11 March 2016

UMMY: WANAONUNUA MADADAPOA WAKAMATWE


WAKATI Wanawake wakiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, serikali imeagiza kufanyika kwa msako mkali dhidi ya wanaume wanaonunua kinadada wanaofanya biashara haramu ya ngono.
Biashara ya ngono imekuwa ikishamiri katika maeneo mbalimbali nchini, hususan kwenye majiji makubwa ya Dar es Salaa, Arusha, Mwanza, Mbeya, Tanga, Morogoro na Tanga.
Kutokana na hatua hiyo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema licha ya biashara hiyo kuwa hatari na kukuza maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, pia inachochea vitendo vya udhalilishaji kwa mwanamke.
Amesema waathirika wakubwa wa udhalilishaji huo ni wanawake, wakiwemo wasichana wenye umri mdogo, hivyo mikakati ya serikali ni kuikomesha kabisa na kwa kuanzia, itaanza kuwasaka wateja na wauzaji.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika katika Viwanja vya Biafra, Dar es Salaam, jana, Samia alimwagiza Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhakikisha wateja wote wa makahaba wanakamatwa.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine, lihakikishe sio tu kuwakamata makahaba bali na wanunuzi, ambao ndio wahusika wakubwa na chanzo cha biashara hiyo.
“Naliagiza jeshi la polisi kuanzisha msako haraka wa kuwakamata wanawake wanaofanya biashara hii haramu pamoja na wateja wao ili wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.

Benki ya Wanawake

Katika hatua nyingine, serikali imempa siku tatu Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake Tanzania, Magreth Chacha, kutoa maelezo kutokana na riba kubwa inayotozwa na benki kwa wanawake wanaokopa.
Alisema haoni sababu ya benki hiyo kutoza riba kubwa wakati fedha zinazotumika kuwakopesha wanawake ni mali ya serikali.
Agizo hilo limetokana na malalamiko yaliyotolewa na wanawake, kupitia hotuba yao iliyosomwa kwa mgeni rasmi, ambapo wamedai riba ya asilimia 19 inayotozwa kwa wakopaji ni kubwa na kikwazo.
Kutokana na riba hiyo, wanawake hao wamedai kuwa wamelazimika kutafuta mikopo kwenye benki zingine, ambazo riba yake ni nafuu na kuikwepa taasisi hiyo, ambayo imeanzishwa kwa lengo la kuwainua.
“Hili jambo linasikitisha sana na hata mkuu wangu wa nchi akilisikia, atanishangaa kama nitalifumbia macho…kabla sijatumbuliwa jipu, inabidi nianze na wewe kwa kunipa maelezo kwa nini riba ni kubwa,” alisema.

Haki sawa

Kuhusu upatikanaji wa haki sawa, alisema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kisera, kisheria na kuweka mipango mikakati ya kitaifa na kisekta, ili kuhakikisha wanawake wanapatiwa fursa mbalimbali za maendeleo na kuleta usawa wa kijinsia.
Alizitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na kurekebisha sheria kandamizi na kutunga sheria mpya ya ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi, kwa kuweka nafasi za viti maalumu ili kuleta uwiano mzuri katika ngazi za maamuzi.
Kuhusu uwezeshwaji kiuchumi, alisema kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya mwaka 2016/2020, inawataka kuimarisha wigo wa kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu, elimu ya ujasiriamali, ujuzi wa kujiajiri na fursa za kipato cha kujikimu.
Pia, alisema Ilani imeziagiza halmashauri zote nchini kutenga asilimia tano ya mapato yake kwa ajili ya mfuko wa maendeleo ya wanawake ili kuondoa kero na malalamiko ya wanawake.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecki Sadiki,  alisema bado wanawake ndio waathirika zaidi wa maradhi mbalimbali, ikiwemo ukimwi na vifo vinavyotokana na uzazi.
Alisema kutokana na changamoto hizo, serikali imekuwa ikihamasisha umuhimu wa kujikinga na magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo ukimwi.

No comments:

Post a Comment