MGOMBEA wa urais kwa tiketi ya CHADEMA, Edward Lowassa, ametakiwa kwenda kumaliza umasikini wilayani Monduli, ili kuonyesha kwa vitendo kama kweli anauchukia na kuacha kuwatapeli wananchi kwa kutoa ahadi za uongo, imeelezwa.
Imeelezwa kuwa kitendo cha Lowassa cha kudai kwamba anauchukia umasikini na kwamba wakifanikiwa kuingia madarakani atahakikisha anaumaliza katika pindi kifupi, ni jambo ambalo si sahihi kwa kuwa ameshindwa kuumaliza katika wilaya yake kwa miaka yote.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Msaidizi, Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mtela Mwampamba, katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye jimbo la Kigoma Mjini, ambapo aliwaomba wananchi kutomchagua Lowassa kwa kuwa si mkweli.
"Lowassa anasema anauchukia umasikini wakati Monduli kuna masikini wengi ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali na ameshindwa kuwakwamua, sasa ataweza kwa nchi nzima? Huu ni uongo ndugu zangu tusikubali, tumpe kura zote Dk. John Magufuli kwa sababu ndiye anayefaa kukabidhiwa nchi na kuachana na wababaishaji," alisema.
Alisema kama kweli anauchukia umasikini, katika jimbo la Monduli wamasai wanahangaika, hawana maji, wanazunguka nchi nzima, wanauza ugolo na ameshindwa kuwasaidia kwa kumaliza changamoto zinazowakabili.
Mwampamba alisema Lowassa hana uwezo wa kuwakomboa wananchi kiuchumi hivyo hafai kupewa uongozi wa nchi.
Alisema wapinzani hawatakiwi kupewa kura kutokana na kuishiwa sera kwa sababu agenda yao iliyokuwa inawabeba ya kuchukia ufisadi, imekwama baada ya kumchukua Lowassa.
Alisema wapinzani walikuwa wakimtuhumu Lowassa kwa kashfa hiyo, lakini wamemteua kuwa mgombea wao wa urais, hivyo aliwaomba wananchi hao kuchagua viongozi wa CCM katika ngazi zote.
Kwa upande wake, mbunge wa Afrika Mashariki, Angela Kizigha, aliwataka wananchi hao kumchagua Dk. Magufuli kwa sababu ni kiongozi muadilifu, mchapakazi na anayechukia rushwa, tofauti na wagombea wengine ambao hawapaswi kupewa nafasi hiyo kwa sababu hawana dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Dk. Amani Kabouru alisema Dk. Magufuli atashinda kwa zaidi ya asilimia 90, kutokana na imani kubwa waliyonayo wananchi kwa CCM, hasa kwa maendeleo makubwa yaliyofanyika ndani ya mkoa huo.
Pia, aliiomba serikali ijayo ya awamu ya tano kuwasaidia kwa kujenga barabara ya lami ndani ya mji wa Kigoma, kwa sababu wanataka kuubadili ili uwe Jiji.
Aliwaomba wananchi waliohudhuria mkutano huo kuhakikisha wanamchagua Dk Magufuli ili malengo yaweze kutimia.
Kwa upande wake, Samia aliwataka wananchi wa Kigoma kutobabaishwa na propaganda za wapinzani, ambao wanapita katika maeneo yao na kuahidi kuwa watawaletea mabadiliko, jambo ambalo si sahihi kwa sababu mabadiliko ya kweli yanafanywa na serikali ya CCM.
Samia alisema CCM imekuwa ikifanya mabadiliko ya mara kwa mara ambayo yana tija kwa maendeleo ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Alitolea mfano suala la kupunguza utegemezi katika bajeti kuu ya serikali iliyokuwa inategemea wahisani kwa asilimia 42, na kwa mwaka huu imepungua na kufikia asilimia nĂ ne.
Alisema CCM ndiyo yenye mipango kazi na mfumo madhubuti wa kusimamia serikali, hivyo aliwaomba wananchi kutopoteza muda kwa kuchagua viongozi, ambao wameshindwa hata kuelezea ilani yao kwao, badala yake wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura na kumchagua Dk Magufuli.
No comments:
Post a Comment