Wednesday, 7 October 2015

DK. SHEIN AAHIDI KIWANJACHA NDEGE NUNGWI




Na Hamis Shimye, Nungwi

MGOMBEA Urais wa CCM, Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema endapo atachaguliwa tena kuwa rais, katika miaka mitano ijayo ana mpango wa kujenga kiwanja cha ndege cha dharura eneo la Nungwi.

Mbali ya kujengwa kwa kiwanja hicho, pia alisema anakusudia kukiunganisha Chuo cha Utalii cha Maruhubi na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ili kianze kitoa shahada ya utalii.

Dk. Shein alisema Zanzibar ni mahali salama kwa kila kitu na ndio maana inapendwa na watu wengi toka karne ya 13, ambapo wanahistoria wengi akiwemo Marcopolo waliandika kitabu cha kuisifu Zanzibar.

Alisema uzuri wa Zanzibar na upekee wake, ndio unaoifanya kuwa ni kitivo cha amani na utulivu, hivyo kila mmoja anapaswa kuitunza amani hiyo ili maendeleo yadumu zaidi.

"Maendeleo yapo na yanakuja, nawaahidi watu wa Nungwi tutajenga kiwanja cha ndege cha dharura ili kusaidia ndege kutua na hata watalii kufika kwa wingi eneo hili,''alisema.

Alisema amejipanga kuhakikisha anaendeleza na kudumisha utalii wa ndani na nje ili kila Mzanzibari anaishi eneo hilo na kunufaika na utalii wa eneo hilo.

Hivyo, alisema kila analoahidi litafanikiwa kwa kuwa CCM inaongozwa na Ilani ya Uchaguzi na ndio maana wanaahidi mambo mengi yaliyopo kwenye ilani na sio vinginevyo.

No comments:

Post a Comment