NICHUKUE fursa hii kumpongeza Mzee Kingunge Ngombale
Mwiru kwa kutekeleza azma yake ya miaka
mingi ya kukisaliti chama kilichomlea cha CCM.
Nafurahi kuona kuwa Kingunge ameamua kukubaliana na ukweli
kwamba CCM ya sasa inaendeshwa na watu makini
tena wenye damu inayochemka. Watu ambao
kasi yao asingeweza kuimudu hata
kidogo kwa sababu umri wake umekwenda.
Wahenga walisema ‘Uzee ni kisima cha busara,’ lakini
ninampongeza Kingunge kwamba baada ya
kubaini kisima chake hicho kimekauka
busara zilizomfanya kuheshimika mpaka sasa
katika taifa hili, aliona hana budi kukifukia kabisa.
Ninampongeza kwa kujitathimini na kujikosoa kwamba hawezi tena kutoa
ushauri kuendana na kasi hiyo na CCM ya sasa siyo saizi yake hivyo kuamua
kujiweka pembeni.
Haya ni maamuzi ya msingi kabisa ambayo kama kuna
wengine wako ndani ya CCM wanaamini kuwa hawawezi kuendana na kasi ya
mabadiliko yanayoendelea, ni bora wajiondoe mapema.
CCM haiundwi na watu wanaohitaji huruma ya kusikilizwa
hata kama wanachoshauri hakifai. CCM ya sasa haiendeshwi kwa kauli ya ‘Zidumu
fikra za mwenyekiti’. CCM ya sasa
haiendeshwi kwa watu wanaotegemea hisani
ya kubebwa na fulani kama kina Kingunge walivyokuwa
wakibebwa na Mwalimu Nyerere kwa sababu ya busara zake.
Hii ni CCM mpya. CCM makini ya watu makini na wenye maono
thabiti. Wengi watashindwa kasi yake. Watashuka katika gari kubwa na
kuwaacha wenye CCM yao waendelee na safari ya mabadiliko ya kweli.
CCM ya sasa inaendeshwa na wenye moyo wa dhati wa kuleta
mabadiliko. Kingunge ameshindwa kasi hiyo na ndiyo maana ninampongeza kwa
kujipima na kufanya maamuzi hayo kisha kubaini kuwa hafai kuendelea na safari
ya mabadiliko ndani ya chama.
Ujana wake wote
amekula ndani ya CCM, eti leo hii uzee wake anaumalizia upinzani. Kuna
nini hapo?
Bila shaka ni tama. Kingunge ameingiwa na tamaa
kiasi cha kumsaliti swahiba wake Hayati Mwalimu Nyerere. Ameingiwa na tamaa
mbaya.
Lakini hii ni tamaa ya nini kwa umri alionao? Tamaa ya
uongozi? Tamaa ya umaarufu? Tamaa ya
fedha? Tamaa ya kutafuta sifa ? Anahangaikia nini? Anahitaji nini mzee
huyu?
Swali ni kwamba, kwa uzito wa Kingunge, ni mzee gani
anayefanana naye au anayemzidi kwa umri, ambaye alikwenda kumshauri ili achukue uamuzi huo wa kusaliti Chama?
Itanishangaza kuona kuwa, Kingunge alishawishiwa kuchukua uamuzi huo na
kama hakushawishiwa, basi inasikitisha
kama utakuwa ni uamuzi uliotoka ndani
ya kichwa chake mwenyewe.
Simfahamu vema Kingunge. Huu ndiyo ukweli. Nakiri hivyo kwa sababu uwepo wake serikalini nimeanza
kuusikia baada ya kuzaliwa na kupata
ufahamu.
Baada ya hapo nilianza kufuatilia sifa zake kwamba
alikuwepo hata enzi za babu wa babu wa baba yangu na alikuwa kiongozi katika taifa hili katika
ngazi mbalimbali.
Ameishi maisha marefu ndani ya CCM. Hata nyumba
aliyoishi ni ya CCM. Nashangaa eti Kingunge anaihama CCM leo hii mwaka 2015,
wakati alikuwepo tokea hamsini kweusi. Mbona
amechelewa sana?
Nasema hivyo kwa sababu ninakumbuka sana kuwa, katika nyadhifa nyingi alizowahi kupewa na
Mwalimu Nyerere, alikuwa akivuliwa baada ya kusaliti. Hata ukamanda wa vijana wa CCM (UVCCM) alivuliwa
na ndiyo wadhifa wa mwisho.
Ndiyo maana nasema amechelewa
kwa sababu alikuwa na chembechembe za usaliti tokea enzi za Mwalimu Nyerere.
Mwalimu alikuwa ni mtu mwenye huruma, hivyo alikuwa
akimsamehe. Kingunge ameishi hivyo na kukua hivyo kwa kuonewa huruma na
kubebwabebwa. Ameishi kwa kutegemea huruma ya Mwalimu. Kama si Mwalimu basi
Kingunge huyu angefanya usaliti kama huu uzeeni? Asingeweza.
Hapa ndipo ninapokumbuka nukuu anayopenda kuitumia Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi, James Mbatia, mara nyingi.
Amekuwa akinukuu kifungu cha Biblia kinachosema, “Heri kijana masikini, kuliko mfalme mzee mpumbavu, ambaye
hasikii tena maonyo.”
Nenda Kingunge.
Kama kuna kitu umesahau ndani ya CCM, tutakuletea.
No comments:
Post a Comment