Friday 11 March 2016

TUSIOGOPE-RAIS MAGUFULI






RAIS Dk. John Magufuli amesema, Tanzania haipaswi kuona aibu kujifunza maendeleo yaliyofikiwa na Vietnam na endapo ikishindwa kufanya hivyo, falsafa ya HapaKaziTu, haitofikia malengo yaliyokusudiwa.
Amesema licha ya taifa hilo kupigana vita kuanzia mwaka 1945 hadi 1976, lakini limepiga hatua kubwa kiuchumi na kufanikiwa kupunguza umasikini kwa asilimia  50.
Adha, Rais wa Vietnam, Truong Tang San, amebainisha kuwa wataongeza uhusiano na ushirikiano kati ya taifa hilo na Tanzania kwenye njanya za kijeshi, kilimo, ufugaji na uvuvi.
Awali, kabla ya kuwasili Ikulu, jijini Dar es Salaam, wananchi walikusanyika kwenye viwanja vya Ikulu, wakiwa na shauku ya kumlaki kiongozi huyo, ambaye aliambatana na ujumbe wa viongozi na wafanyabiashara zaidi ya 50.
Alipowasili kwenye viwanja hivyo saa tatu asubuhi, alilakiwa na mgeni wake, Rais Dk. Magufuli na baadaye kwenda kwenye jukwaa maalumu, kisha kupigwa nyimbo za taifa pamoja na mizinga 21.
Rais Truong, pia alipata fursa ya kukagua gwaride maalumu lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ).
Baada ya hapo, kiongozi huyo akiambatana na Rais Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi pamoja na viongozi wengine wa serikali, walilakiwa na wananchi kwenye viwanja vya Ikulu, wakati walipokuwa wakiingia kwa ajili ya mazungumzo.
Viongozi hao walifanya mazungumzo maalumu yaliyohusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Wakati viongozi hao wakiendelea na mazungumzo, ujumbe wa Rais Truong, ulionekana kupendezewa na mazingira, amani na ukarimu wa Watanzania.
Mara kwa mara walikuwa wakipiga picha na baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali yanayozunguka Ikulu, hususan ufukwe wa bahari ya Hindi.
Baada ya kumaliza mazungumzo, Rais Dk. Magufuli, alipata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari, ambapo alisisitiza umuhimu wa kujifunza kutoka kwa Vietnam.
Alisema licha ya nchi hiyo kuchukua mbegu ya korosho nchini, lakini kwa sasa inaongoza duniani kwenye uzalishaji wa zao hilo duniani.
Alisema mbali na korosho, pia imepiga hatua kubwa katika kilimo cha mpunga, ambacho kinalimwa mara tatu kwa mwaka wakati hapa nchini, zao hilo linalimwa mara moja kwa kila mwaka.
Dk. Magufuli aliongeza kuwa, taifa hilo lililopata Uhuru mwaka 1945 na kupigana vita hadi mwaka 1976, limeweza kupunguza umasikini kwa asilimia 50, huku pato la wananchi wake likifikia dola za Marekani 2,000, kutoka dola 100 kwa mwaka.
“Hatupaswi kuona aibu kujifuza katika nchi zilizotutangulia kimaendeleo, hivyo ujio huu ni fursa muhimu kwa sababu Vietnam imepiga hatua kubwa hususan kwenye kilimo.
“Licha ya kuwa na ardhi zaidi ya asilimia 80 yenye kufaa kwa kilimo, lakini bado haijatumika ipasavyo,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Rais Truong alisema, Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuanzisha mahusiano na Vietnam, katika kipindi cha harakati za ukombozi.
Alisema Vietnam itahakikisha inashirikiana na Tanzania kwenye nyanja za ulinzi, biashara, kilimo na ufugaji pamoja na kufanya mikutano ya mara kwa mara ili kuboresha mahusiano.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo utajikita pia katika kuhamasisha maendeleo, amani na utulivu kwenye mataifa mengine.
Rais huyo pia alitembelea Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM na kukutana na Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.
Baada ya mazungumzo yao, Kikwete alisema lengo la Rais huyo kuitembelea CCM ni kuimarisha uhusiano kati yake na Chama cha Kikomonisti cha Vietnam.
Alisema vyama hivyo vina uhusiano wa karibu kwa muda mrefu na kwamba, ipo haja ya kuuendeleza kwa maslahi ya vyama vyote.
Kwa mujibu wa Kikwete, wakati Vietnam ikipigana na Marekani, vyama vya TANU na ASP, vilifanya kazi kubwa kuwasaidia Wavietnam kwa kuwapa misaada mbalimbali.
"Vyama vyetu vina uhusiano wa karibu kwa muda mrefu sana. Wakati ule wakipigana na Marekani, sisi tukiwa vijana, tulikuwa tukikusanya michango na kuwasaidia mahitaji mbalimbali. Nakumbuka wakati fulani Rais mstaafu Mzee Benjamin Mkapa ndiye aliyeteuliwa kuifikisha nchini humo," alisema.
Wakati huo huo, Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli, amaemkaribisha, mke wa Rais wa Vietnam, Mama Mai Thi Hanl, ambapo alisema ujio huo utafungua fursa muhimu za kiuchumi.
Alisema Watanzania wanatarajia kupata wawekezaji kwenye sekta mbalimbali za kibiashara,zitakazosaidia kuiinua kiuchumi.
Baada ya kukaribishwa, Mama Mai Thi Hanl, alieleza kufurahishwa kwake na ushirikiano wa kihistoria uliodumu zaidi ya miaka 50.
Vilevile, Mama Janeth na mgeni wake, walimtembelea Makumbusho ya Taifa, ambapo walijionea mambo mbalimbali ya kihistoria.
Leo, Rais Truong anatarajiwa kutembelea Eneo Maalumu la Uwekezaji (EPZ), Ubungo, Dar es Salaam, kujionea shughuli mbalimbali kabla ya kwenda Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Kesho Rais Truong na ujumbe wake utaondoka nchini kwenda Msumbiji kuendelea na ziara.

No comments:

Post a Comment