Sunday 6 March 2016

MAKONDA AZINDUA RASMI VITAMBULISHO VYA WALIMU KUPANDA DALADALA BURE




MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amezindua vitambulisho vitakavyotumiwa na walimu kupanda daladala bure wakati wakitoka nyumbani kwenda kazini.

Katika hatua nyingine Makonda ameziomba sekta mbalimbali nchini kushiriki katika kutoa mawazo yao ya maendeleo ili taifa lizonge mbele badala ya kuwa watizamaji.

Makonda aliyasema hayo Dar es Salaam jana mbele ya wazazi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Turiani wakati akizindua vitambulisho hivyo vitakavyotumiwa na walimu wa wilaya yake kupanda daladala bure kufuatia mpango aliouanzisha wiki iliyopita wa kuwasaidia  walimu hao.

“Nawaomba watanzania na sekta mbalimbali kuwa na mawazo ya maendeleo ambayo yatawekwa mezani na kuyafanyia kazi jambo litakalo msaidia Rais wetu Dk.John Magufuli katika kuliinua taifa kiuchumi badala ya kumuachia kila kitu akifanye yeye” alisema Makonda.

Makonda alitoa mwito kwa makondakta wa daladala kutoa ushirikiano kwa walimu hao kesho wakati watakapoanza kupanda magari yao huku wakijua walimu ndio waliowafundisha na kufikia hatua hiyo ya kazi walizonazo.

Ofisa Elimu wa Sekondari wa Wilaya hiyo, Rogers Shemwelekwa aliwaomba wananchi hao na walimu kuendelea kuunga mkono jitihada za Makonda za kuwaletea maendeleo na kumuombea kwa mungu badala ya kumbeza kwani kazi hizo anazozifanya ni kwa ajili ya wananchi.

(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)

No comments:

Post a Comment