Thursday, 16 June 2016
MAHAKAMA KUU YATUPILIA MBALI KESI YA UCHAGUZI UKONGA
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi aliyokuwa amefunguliwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara (CHADEMA).
Kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo, iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jerry Silaa, kunatokana na kufunguliwa nje ya muda.
Shauri hilo la uchaguzi namba 10 la mwaka 2015, lilitupiliwa mbali jana na Jaji Fatuma Masengi, aliyekuwa analisikiliza.
Jerry alifungua shauri hilo Novemba, mwaka jana, dhidi ya Mbunge Waitara, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo.
Upande wa walalamikiwa walikuwa wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata na Waitara akiwakilishwa na Wakili Dk. Onesmo Kyauke.
“Mahakama imejiridhisha pasi na kuacha shaka yoyote na hoja za upande wa walalamikiwa kwamba, shauri hilo limefunguliwa nje ya muda,” alisema Jaji.
Aidha, alisema hakuna shahidi hata mmoja wa upande wa mlalamikaji aliyeweza kuithibitishia mahakama kwamba, alikuwepo siku ambayo matokeo hayo ya uchaguzi yalitangazwa.
Alisema Silaa alifungua kesi hiyo Novemba 27, mwaka jana, akipinga ushindi wa Waitara, ambapo upande wa walalamikiwa waliwasilisha pingamizi la awali mapema, wakidai kesi imefunguliwa nje ya muda, hata hivyo mahakama iliona isilipokee hadi hapo kesi itakapoanza kusikilizwa.
Jaji alisema mahakama ilipitia vifungu vya sheria kutokana na pingamizi hilo kuwasilishwa mapema na ilikubaliana kuanza kusikiliza ushahidi wa Jerry, ambaye alikuwa na mashahidi watatu kisha itoe uamuzi juu ya hoja za upande wa walalamikiwa kama kweli kesi ilifunguliwa nje ya muda au la.
Alisema hoja ya msingi iliyokuwa ikibishaniwa ni kuhusu tarehe ya kutangazwa kwa matokeo, ambapo ushahidi wa upande wa mlalamikaji ulikuwa ukijichanganya juu ya muda rasmi wa kutangazwa kwa matokeo, ambapo ulidai Novemba 27 ama Novemba 28, mwaka jana.
“Kutokana na kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imebaini kwamba mashahidi walikuwa wakijichanganya kwa kuwa hawakuwepo kituoni wakati matokeo yakitangazwa na walirudi kituo cha uchaguzi Novemba 28 na kukutana na walinzi waliowaambia kwamba matokeo yalikwishatangazwa” alisema.
Alisema mahakama ilipopitia kithibitisho ambacho ni fomu 24 B inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ilionyesha matokeo yalitangazwa Novemba 27, mwaka jana.
Jaji huyo alisema mlalamikaji Silaa alikubaaliana na karatasi hiyo, isipokuwa alidai kwamba, haikuwa sahihi, hivyo kutokana na hayo, mahakama inakubali kwamba matokeo yalitangazwa Novemba 27, mwaka huu.
Pia, alisema mahakama hiyo imejiridhisha kwamba kesi hiyo ilifunguliwa nje ya muda kwa sababu shauri la uchaguzi linatakiwa lifunguliwe ndani ya siku 30 baada ya kutangazwa matokeo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment