Thursday, 16 June 2016

MAJALIWA AZITAKA BENKI KUPITIA UPYA RIBA ZAKE



WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka benki nchini kupitia upya riba zake ili Watanzania waweze kukopa na kurejesha mikopo kwa urahisi.

Amesema riba kubwa zinazotozwa na baadhi ya benki, huduma zisizokidhi mahitaji na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha ni miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo wananchi wanapotaka huduma za kifedha.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Jumuia ya Benki za Wananchi (COBAT) mjini Dodoma.

Mkutano huo ulijumuisha wajumbe kutoka mikoa 10 ya Tanzania Bara, ambayo ni Kigoma, Lindi, Simiyu, Manyara, Katavi, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Singida na Dodoma.

Alisema changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa taarifa mbalimbali za sheria na taratibu, ambazo zinakwamisha ufanisi wa kiutendaji kwa baadhi ya taasisi, hasa zile zinazolenga kuwahudumia watu wa kipato cha chini.

“Tunahitaji kutafuta njia bora ya kutatua changamoto hizi na benki za wananchi ni kiungo muhimu katika kushughulikia changamoto zinazokabili utoaji wa huduma za kifedha,” amesema.

Waziri Mkuu alisema ni muhimu kuanzisha benki hizo katika kila mkoa ili kuweza kusambaza huduma hizo karibu zaidi na walengwa.

Alisema serikali itaangalia uwezekano wa kuiwezesha mikoa, ambayo itaonyesha ari zaidi ya kuanzisha benki zao na akatoa wito wa kuandaa mikakati ya kuhamasisha wananchi ili wakusanye mitaji ya kutosha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa COBAT, Elizabeth Makwabe alisema jumuia yao ilianzishwa mwaka 2006, ikiwa na wanachama saba na sasa hivi wamefika 10, huku wananchi wanaohudumiwa na benki hizo ni zaidi ya milioni mbili.

Alisema Jumuia ya Benki ya Wananchi, inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo mfumo hafifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na ufinyu wa mitaji.

No comments:

Post a Comment