Thursday, 16 June 2016
MWISHO WA SIMU FEKI NI LEO
WAKATI Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikitarajia kuzima simu 'feki' leo, imesema idadi ya simu nchini hazitazimwa kwa kuwa zinakidhi vigezo na ni halisi.
Imesema asilimia 96.95, ya simu nchini ni halisi, ambapo zimethibitika kupitia namba tambulishi za simu halisi (IMEI).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, aliwataka wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi, kutambua kuwa ni kosa kisheria kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu.
Pia, alisema yeyote atakayehusika kubadili namba hizo, atakumbana na adhabu ya kifungo cha hadi miaka 10 au faini isiyopungua sh. milioni 30 au vyote kwa pamoja.
Mhandisi Kilaba aliwataka wafanyabiashara wa simu nchini, kuhakikisha wanaleta simu zenye viwango na zilizohakikiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuwa na leseni kutoka TCRA.
Alisema leseni hizo ni kwa mafundi simu, ambao wanatakiwa kuanza mchakato wa kuzipata kwa ajili ya shughuli zao za utengenezaji simu na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wateja wao ili kuepuka mtandao wa wizi wa simu nchini.
Kilaba alieleza faida za mfumo rajisi wa namba tambuishi kuwa ni kupunguza wizi kwa njia ya simu, kuhimiza utii wa sheria na kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi zisizo bandia.
Alisema pamoja na jitihada zilizofanywa na mamlaka na wadau wengine, bado katika kuelekea kuzima mitambo ya simu bandia,
kuna changamoto ambazo ni uaminifu kuwa mdogo kwa baadhi ya wauzaji wa simu kwa kutoa punguzo kwa wananchi na kuwashawishi kununua simu bandia kwa bei nafuu.
Changamoto nyingine ni gharama kubwa kuwafikia wananchi na kuwaelimisha ili waweze kuelewa zaidi juu ya mpango mzima wa kuhakiki simu zao na uelewa mdogo kwa wananchi katika kuitikia wito wa kuhakiki simu zao kwa kipindi cha mpito.
“Tangu Desemba, mwaka jana, tumejitahidi kufanya kampeni ya kutoa elimu juu ya kuhakiki namba tambulishi na vifaa vya simu za mikononi katika mikoa ya Tanga, Kilinanjaro, Arusha na Manyara,"alisema na kuitaja mikoa mingine kuwa ni Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Iringa, Dodoma, Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara, Kagera na Zanzibar.
Aliwataka watanzania kuhakiki simu zako iwapo ni za bandia kwa kuwa kuanzia leo, hakutakuwepo na simu bandia itakayoweza kufanya kazi nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment