Thursday 16 June 2016

JPM: TUIOMBEE NCHI YETU IENDELEE KUWA NA AMANI


RAIS Dk. John Magufuli amewasihi Watanzania kuungana na Waislamu walioko kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, kuiombea Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani, utulivu, umoja na mshikamano ili iweze kutimiza malengo yake ya kimaendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo mbele ya masheikh, maimamu,
viongozi wa dini ya kiislamu na baadhi ya viongozi na waumini wa madhehebu mengine, aliowaalika katika futari juzi, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

"Kwa niaba ya serikali, mimi mwenyewe na Watanzania kwa ujumla, natumia fursa hii adhimu kuwatakia Waislamu wote nchini mfungo mwema wa Ramadhani, uwe mfungo wa amani na wenye baraka, lakini pia ninamuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema azikubali funga zenu na kuwalipa malipo stahili.

"Niwaombe ndugu zangu Waislamu, msisahau kuliombea taifa hili amani, palipo na amani ndipo palipo na maendeleo ya kweli, palipo na amani ndipo biashara itakwenda vizuri, palipo na amani hata mahubiri mazuri kwa watu yatasikika vizuri, tulisimamie hili kwa manufaa ya Tanzania," alisema.

Mbali na kuwatakaa Watanzania wote kuliombea taifa, Rais Magufuli pia amewahakikishia wananchi kuwa, serikali yake ipo imara kuhakikisha inailinda na kuidumisha amani iliyopo.

Aidha, Dk. Magufuli alilezea kufurahishwa kwake na umoja na ushirikiano wa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini wanaounda kamati za amani za mikoa.

Mbali na hilo, amewataka wafanyabiashara wa vyakula kuacha kupandisha bei za vyakula, hasa vinavyotumika wakati wa mfungo mtukufu wa Ramadhani, ili kuwawezesha waliofunga kumudu kununua vyakula hivyo.

Katika futari hiyo, Rais Magufuli na mkewe, Mama Janeth Magufuli waliungana na viongozi mbalimbali wa dini, wakiwemo Kaimu Mufti wa Tanzania, Alhaji Hamid Masoud Jongo, Askofu Mkuu wa Anglikana Mkoa wa Dar es salaam, Baba Askofu Valentino Mokiwa, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa na Mwenyekiti wa Wanawake Waislamu Tanzania, Hajjat Shamim Khan.

No comments:

Post a Comment