Thursday 16 June 2016

MKURUGENZI ATUMBULIWA KWA UTORO KAZINI

MKUU wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo,   ameagiza kusimamishwa kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Josephat Maganga, baada ya kuupuza maagizo ya uongozi wa mkoa na ya Rais Dk. John Magufuli.

Mkurugenzi huyo ameingia katika kitanzi   hicho  cha kutumbuliwa baada ya kudaiwa  kutoroka katika kituo chake cha kazi kwa siku zaidi ya  tatu bila ruhusa  ya  uongozi   wa  mkoa.

Alitoa agizo la kuchukuliwa hatua kwa   mkurugenzi huyo kupitia kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa  wa  Mara, Eldom  Anyosisye,    katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama   Wilaya ya Butiama, wakiwemo wakuu wa idara.

Alisema licha  ya kuwepo kwa agizo la viongozi kutoondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila ruhusa, hasa katika kipindi hiki cha agizo la  Rais la  utengenezaji wa madawati, mtendaji huyo kwa jeuri alishindwa kuzingatia maagizo na kuondoka kwenda Dar es Salaam.

Mulongo alisema mkurugenzi huyo wa Butiama  aliondoka kwenye kituo chake cha kazi zaidi ya  siku tatu, bila kupewa ruhusa na ofisi ya katibu tawala mkoa wala yeye kujulishwa na kudai hiyo  ni dharau na kuvunja taratibu na kanuni za  utumishi wa umma.

“Alijua wakuu wa wilaya, wakurugenzi hata  mimi mwenyewe kwa sasa siwezi kufunga safari  yoyote, tunashughulikia jambo muhimu la  utekelezaji wa agizo la Rais la kumaliza tatizo  la madawati, lakini mkurugenzi huyu kwa  dharau na kuona hawezi kufuata taratibu za  utumishi wa umma, anandoka na anakaa nje kwa  zaidi  ya  siku   tatu. Kwa taratibu za  kiutumishi, amejifuzisha kazi mwenyewe,”alisema Mulongo.

"Kwa mujibu wa taratibu za kazi, mtu akiondoka sehemu ya kazi ndani ya siku tatu bila kuwa na ruhusa wala taarifa zozote, moja kwa moja mtu huyo amejifukuzisha kazi mwenyewe na sheria iko hivyo,” alifafanua.

Mkuu huyo wa mkoa aliongeza: "Lazima nidhamu ya kazi iwepo kwa kila mmoja wenu katika eneo lake la kazi na serikali ipo makini katika suala la nidhamu katika utumishi wa umma na yule atakayeenda kinyume na taratibu za kazi lazima achukuliwe hatua."

Alidai serikali ilishatoa maagizo na maelekezo juu ya safari zote za watumishi na viongozi katika nafasi mbalimbali na kuwataka watumishi wa wilaya ya Butiama, kuwatumikia wananchi na kuzingatia taratibu za kazi.

Alisema tayari amemuagiza Katibu Tawala kwa mujibu wa taratibu, amuandikie barua mkurugenzi huyo juu ya hatua zilizochukuliwa na kutoa taarifa kwenye ofisi ya Katibu Mkuu.

"Nilifanya ziara hapa Butiama, Ijumaa na kuna maagizo nilitoa baada ya kuona baadhi ya mambo hayapo vizuri yafanyiwe kazi, lakini baada ya hapo mkurugenzi anaondoka tena bila ruhusa, sasa nidhamu za hivi haziwezi kukubadilika, lazima hatua zichukuliwe,"aliongeza.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Anyosisye, alisema mkurugenzi huyo amefanya makosa kutokana na kuondoka bila kupewa ruhusa wakati kukiwa na maelekezo.

Alisema katika maagizo ya Rais juu ya ukamilishaji wa madawati ifikapo Juni 30, mwaka huu, Halmashauri ya Butiama ina upungufu wa madawati 8,945, kwenye shule za msingi na zaidi ya 500 kwenye shule za sekondari.

"Nimeshatekeleza maagizo ya mkuu wa mkoa aliyoyatoa tulipokuwa kwenye kikao cha Butiama, ikiwemo kumteua Ofisa Kilimo wa Wilaya, Revocatus Tunda, kukaimu nafasi hiyo mpaka hapo maagizo mengine yatakapotolewa,"alisema.


No comments:

Post a Comment