Thursday 16 June 2016

KADUMA: JPM KAMA NYERERE


IWAPO Rais Dk. John Magufuli, ataendelea kuliongoza taifa namna alivyoanza, ipo imani kubwa ya kurudisha heshima na misingi bora iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Aidha, Watanzania wametakiwa kumuombea Rais Magufuli kutokana na mwelekeo nzuri alionao, ikiwemo kuwa wazi juu ya anayokusudia kuyafanya.

Hayo yalielezwa jana, Dar es Salaam na Mzee Ibrahim Kaduma, wakati akichangia mada katika kongamano la nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, ambapo alisema anatamani kuona nchi inakaa katika mstari.

Kaduma, aliwahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya Pius Msekwa na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, enzi za Mwalimu Nyerere.

"Viongozi wengi waliopita walishindwa kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere, lakini nategemea Rais Magufuli anaweza kutokana na uwazi na mwelekeo mzuri alionao," alisema Kaduma.

Alimshauri Rais Dk. Magufuli, kuweka wazi dira yake kama alivyofanya Mwalimu Nyerere katika Azimio la Arusha ili kufanikisha utekelezaji wake.

“Wasiotaka kukubali ukweli juu ya kazi nzuri na mwelekeo mzuri alionao Rais Magufuli, shauri yao, wakatae, lakini mimi lazima niseme ukweli huo na kuwaomba wananchi wamuombee afanikiwe, kwa ajili yao, maendeleo yao na taifa,”alisema Kaduma.

Alitaja sifa za Mwalimu Nyerere kuwa kila alichosimamia kilikwenda vizuri na alitekeleza mambo kwa vitendo, badala ya maneno peke yake.

"Hakuwa mtu wa anasa, hakujali pesa na raha, alikuwa tayari kujitoa kwa ajili ya manufaa ya umma, badala ya kuangalia kipato chake binafsi," alisema.

Aliongeza kuwa kiongozi ni lazima awe na tabia ya kutokuwa mbinafsi, ambapo Mwalimu Nyerere alikuwa na utayari hata wa kuacha madaraka kwa manufaa ya wote.

"Watu wote walimkubali na kumheshimu kama Baba wa Taifa, angetaka kung'ang'ania madaraka, hakuna ambaye angepinga, lakini ilifika mahali akasema 'lazima ning'atuke'," alisema  Kaduma.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alisisitiza kuwa hakuna sera zinazotekelezeka kwa asilimia 100 popote duniani, bali uongozi mzuri ni ule unaojitahidi kutatua changamoto.

"Awamu zote zimekuwa zikijitahidi, hii ya sasa inaonekana kujitahidi zaidi, suala la muhimu ni kushirikisha wananchi, kujenga demokrasia ya kweli, kukuza kilimo na masomo kwa maendeleo yao," alisema.

Alisema anamfahamu vizuri Mwalimu Nyerere kwa kuwa alifanya naye kazi, hivyo mada ya Sera ya Ujamaa na Kujitegemea anaielewa kuwa ni ya muhimu.

"Hivi sasa kuna zaidi ya vijiji 400 nchini, vingi alivianzisha Mwalimu, hivyo vinapaswa kutumiwa kikamilifu ili kuleta maendeleo hususani kwa kushirikisha wananchi," alisema.

Dk. Juma Bakari, Mkuu wa chuo mstaafu wa Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, aliishauri serikali, kabla ya kutoa fedha ilizoahidi sh. milioni 50 kwa kila kijiji, ziangaliwe rasilimali zilizopo vijijini, ikiwemo utoaji elimu na namna ya kizitumia ili kuleta tija.

Profesa Gaudence Mpangala, aliyekuwa Mhadhiri UDSM, sasa Chuo Kikuu cha Ruaha, aliwataka viongozi wa sasa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele kutekeleza kila alichozungumza.

Alivishauri vyama vya siasa kuacha migogoro kwa kuwa haina tija, badala yake inavidhoofisha, kuvipotezea malengo na kuwakosesha wananchi imani.

No comments:

Post a Comment