Thursday, 16 June 2016

UFISADI WA KUTISHA BODI YA MIKOPO

SAKATA la kusimamishwa kazi kwa baadhi ya watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), limechukua sura mpya baada ya kubainika ujanja uliokuwa ukifanywa katika uchotwaji wa fedha.

Taarifa hiyo ya ukaguzi imeonyesha mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji wa bodi hiyo, ambao wamekuwa wakitafuna fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuwapatia mikopo wanafunzi wa elimu ya juu.

Akizungumzia kubainika kwa mbinu za ulaji huo jana, mjini Dar es Saalam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema watendaji hao walikuwa wakitumia udhaifu wa mfumo wa utoaji na urejeshaji wa mikopo kujinufaisha.

Profesa Ndalichako alisema uchunguzi umeonyesha kuwa, baadhi ya wanafunzi hao wa elimu ya juu, wamenufaika mara mbili kwa kupitia mikopo inayotolewa na HESLB na mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (ZHESLB).

"Taarifa imeonyesha kuwa, kuna wanafunzi wamenufaika kupitia mikopo ya bodi hizi tena mara mbili, ambapo imechangia kuwakosesha fursa ya kupata mikopo wanafunzi wengine, ambao wamekosa mikopo hiyo,"alisema.

Alisema mchezo huo wa utafunaji wa pesa hizo, umefanyika kwa kutumia njia ya mfumo dhaifu wa utunzaji taarifa za marejesho ya mikopo hiyo huku ikibainika kuwa, wanafunzi 247 waliofanya marejesho ya mikopo ya awali kwa kiwango cha asilimia 25, kwa malipo ya sh. 270,894,198,  hawakuingizwa kwenye orodha ya waliorejesha.

Profesa Ndalichako alisema kumbukumbu za HESLB zinaonyesha madeni kwa kiwango pungufu ya deni halisi, huku zikionyesha wanafunzi 262, walinufaika na mikopo ya sh. 10,782,772,831,  lakini imeonyesha wanatakiwa kurejesha sh. 5,535,738,393, badala ya kiasi hicho halisi.

Alisema mchezo huo uliotumika katika mfumo wa utunzaji taarifa za marejesho, hauonyeshi taarifa muhimu za mkopaji, ikiwemo mdhamini wake, mahala anapoishi na hivyo kutumia njia hiyo kuchota pesa hizo.

Waziri huyo alidai kuwa kuna kila dalili za kuwepo kwa wanafunzi hewa 20, huku wanafunzi 168, wa Chuo Kikuu Cha Dar es Saalam wanaonekana kukopeshwa sh. 531,323,125, na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walionekana kukopeshwa sh. 2,530,417,440, lakini
hawakuwzea kutambuliwa na vyuo hivyo kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi wa fedha hizo kama  zimerejeshwa.

Profesa huyo alisema mfumo huo wa urejeshaji wa mikopo haujaunganishwa na mfumo wa utoaji mikopo, hivyo kusababisha kutokuwepo kwa taarifa sahihi za marejesho ya wahusika na kusababisha pesa hizo kuchotwa kinyemela bila ya kuwepo kwa taarifa sahihi za kumbukumbu.

Aidha, taarifa hiyo ya uchunguzi imebaini kuwepo kwa ujanja uliofanyika wa uchotwaji pesa hizo wakitumia udhaifu wa mfumo wa ufuatiliaji wa urejeshaji wa mikopo hiyo, ambapo wanafunzi 105,202, wenye mikopo ilioiva ya sh. 712,8772,822,863, hawajaanza kurejesha kuanzia mwaka 1994-2013.

"Taarifa ya ukaguzi inaonyesha kuwa wanafunzi 2,619, wenye mikopo iliyoiva ya sh. 14,468,564,375, wanadaiwa kwa kukopeshwa wakiwa katika vyuo tofauti, lakini wanatumia namba moja ya kidato cha nne na wanafunzi hao walikopeshwa sh.7,126,694,729, katika chuo cha kwanza na sh.7,341,869,646, katika chuo cha pili,"alifafanua Ndalichako.

Alisema uchunguzi umeonyesha kuwepo kwa dalili za kuchotwa kwa fedha hizo kinyemela kwa kutumia mikataba ya utambuaji na ukusanyaji wa madeni, kazi iliyokuwa ikifanywa na kampuni za zabuni, ambapo waliongeza kiasi kikubwa cha madeni hayo.

Alisema uchunguzi umebaini kuwa, kampuni hizo za utambuaji na ukusanyaji madeni hayo, miongoni mwao hazikusajiliwa kisheria huku nyingine zikimilikiwa na mtu mmoja na zikifanyakazi moja kinyume na taratibu.

Alisema taarifa imeonyesha kuwa, wanafunzi 462 walitambulika na wazabuni tofauti, ambapo Bodi ya HESLB walipewa orodha hiyo huku ikiwa na kiasi kikubwa cha mkopo kuliko mkopo wao halisi wa sh. 2,842,350,188, huku deni likionyesha ni sh. 3,670,698,220.

"Mchezo huo wa uchotwaji fedha hizo ilikuwa ni sawa na ongezeko la sh. 828,348,032, ambapo ongzeko hili lilifanywa kwa kamisheni kuwa kubwa kuliko ilivyostahili na jambo linalosikitisha ni kuwa, wazabuni hawa tofauti wamekuwa wakilipwa kamisheni kwa kuwatambua watu wanaofanana,"alisema Ndalichako.

Mbali na hilo,Profesa Ndalichako alisema kumekuwepo na ubadhirifu wa matumizi makubwa ya fedha za bodi hiyo na kwamba, pesa za marejesho, ambazo zilipatikana kama faida ya mikopo hiyo, zimekuwa zikitumika kujilipa posho kubwa kwa watumishi wa bodi.

"Imekuwa ni tabia na kamchezo kwa watendaji wa HESLB kujinufaisha na fedha zinazotokana na marejesho ya mikopo huku zikitumika kinyume na inavyotakiwa, ambapo wanajiamulia kujilipa posho ya usafiri kwa asilimia 20, huku kila mwaka wanapandisha bajeti ya matumizi,"alisema.

Alisema uchunguzi umeonyesha kuwa, kumekuwepo na kamchezo katika orodha ya majina halisi ya wanafunzi wanaotakiwa kuingiziwa pesa hizo kwenye akaunti zao, ambapo zilikuwa zikibadilishwa na kuingizwa orodha ambayo si halisi.

Profesa huyo alidai kuwa uchunguzi zaidi umebaini kuwepo wanafunzi, ambao walikuwa na  akaunti zaidi ya mbili benki, ambapo benki husika zimekuwa zikikataa kuonyesha ushirikiano kuhusu  mihamala ya uingizwaji wa pesa hizo ili kuhakiki pesa za mikopo hiyo.

Alisema serikali itaendelea kupambana kurejesha fedha hizo na kwamba, waliokuwa wakifanya mchezo huo sasa kiama chao kimefika pamoja na wanaofanya ubadhirifu wa fedha za mikopo ya wanafunzi hao.

Aidha, taarifa hiyo ya uchunguzi imekwenda mbali zaidi hadi Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), ambapo imebaini kuwepo kwa udhaifu wa usimamizi wa mafunzo yanayotolewa vyuoni.

NACTE inapaswa kusimamia vyuo 567, katika eneo la uboreshaji mitaala.

Profesa Ndalichako alisema uchunguzi umeonyesha kuwa NACTE haina wataalamu wa kutosha wenye sifa stahiki za kusimamia jukumu hilo huku ikiwepo tabia ya wafanyakazi kupangiwa majukumu bila kujali ujuzi walionao.

"Kamati ya uchunguzi imebaini NACTE kumekuwepo na udhaifu wa kuwapanga wafanyakazi kulingana na sifa zao na kazi wanazofanya.
Kwa mfano, aliyesomea masuala ya utumishi, amepangiwa kusimamia ukuzaji na uboreshaji mitaala,"alifafanua

Alisema kumekuwepo na udhaifu mkubwa katika suala la NACTE kutotilia mkazo ufuatiliaji wa ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo inavyosimamia na kuwa, katika mwaka wa fedha 2014/2015, NACTE ilikusanya sh.  1,568,003,958, lakini ilitumia sh.174,166,770,  kwa ajili ya kudhibiti ubora wa elimu.

Aidha, alisema NACTE imeweka sifa ya chini kwa mwanafunzi kujiunga na vyuo, lakini imekuwa ikiviagiza vyuo kupokea wanafunzi wenye sifa za chini kuliko sifa za kujiunga na chuo husika, ambapo suala hilo limeshusha viwango vya elimu na ubora wake na halina tija kwa maendeleo ya elimu.

Alisema NACTE imekuwa ikiuza mitaala ya vyuo baada ya kutoa ithibati, badala yake wanageuza kuwa mali yao na kuanza kuigawa vyuo vingine bila idhini ya chuo husika.

Baada ya uchunguzi huo kubainika, serikali imetoa muda wa wiki mbili kwa watumishi waliosimamishwa kazi, kuwapatia mashitaka ya kujibu kutokana na udhaifu uliobainika katika mfumo wa usimamizi wa fedha, utoaji na urejeshaji mikopo ya wanafunzi hao.

Aidha, HSELB imetakiwa kuhakikisha mfumo wa utaoji mikopo unaunganishwa na mfumo wa urejeshaji mara moja na kuanza mara moja makato kwa wanufaika wote, ambao mikopo yao imeiva.

Serikali imeitaka HSELB kuwafuatilia wanafunzi 2,619, ambao walipewa mikopo kwa kutumia namba za mitihani za kidato cha nne zinazofanana na kuhakikisha fedha walizochukua katika vyuo viwili tofauti zinarejeshwa mara moja.

Pia, imetoa muda wa wiki mbili kwa bodi hiyo kutoa maelezo ya kina kuhusu wanafunzi 168, wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam wanaoonekana kukopeshwa sh.531,323,125 na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, walioonekana kukopeshwa sh.2,530,417,440, ambao hawakuweza kutambuliwa na vyuo hivyo kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi.

Serikali imeagiza kupitia upya mfumo mzima wa usajili wa vyuo na kuhakiki ubora wa vyuo, ambavyo tayari vimepata ithibati ili kujiridhisha kama vinakidhi vigezo stahiki.

Vilevile serikali imesitisha mfumo wa mafunzo ya aina ya Cross-Border Education na kwamba, kwa sasa imesitisha ulinganifu wa sifa zinazopatikana kwa kutumia zaidi mfumo huo.

Aidha, Bodi ya NACTE imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuwaondoa watumishi wasio na ujuzi na kuwapanga watendaji kulingana na sifa na ujuzi wao.

Profesa Ndalichako ameiagiza bodi hiyo kuanza kupitia na kujiridhisha kama vyuo vyote vilivyopewa hadhi ya kujitegemea vina sifa stahiki na endapo mchakato wake umefanyika kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu.

Kutokana na taarifa hiyo ya uchunguzi, serikali imeziagiza bodi na mabaraza ya vyuo vikuu, kuhakikisha kuwa malipo ya motisha wanayatoa kwa wafanyakazi wao yanazingatia vyanzo vya mapato kwa ajili hiyo na si kutumia fedha zilizotolewa kwa shughuli mahsusi ya taasisi/chuo.

Pia, wametakiwa kuzingatia miongozo na nyaraka zote za serikali kuhusu viwango vya posho vinavyoruhusiwa kwa watumishi wa umma. Pia, watendaji wakuu wa vyuo vikuu wametakiwa kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kwamba, atakayebainika kwa ubadhirifu hatavumiliwa.

No comments:

Post a Comment