Na Neeema Mwangomo, Dar es salaam
BALOZI wa China nchini, Dk. Lu Youqing, jana alijitokeza kuchangia damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kuwa na moyo wa kuchangia damu.
Kujitokeza kwa Balozi Lu kuchangia damu, pia ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wachangia damu duniani, ambayo huadhimishwa Juni 14, kila mwaka.
Balozi Lu amesema Watanzania hawana budy kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa upendo ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wa damu.
Alisisitiza azma ya serikali ya China kuendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kuisaidia sekta ya afya.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Makwaia Makani' alimshukuru balozi huyo wa China kwa kuwa wa kwanza kujitokeza kuchangia damu kwenye hospitali hiyo.
Alisema hatua hiyo imeonyesha ni jinsi gani anaguswa katika kuokoa maisha ya Watanzania.
“Timu ya wataalamu mbalimbali wa afya kutoka China, wamekuwa na ushirikiano mzuri na wa muda mrefu na hospitali hii katika kusaidia huduma za afya na tumekuwa tukifanya nao kazi tangu mwaka 1968,” alisema Makani.
Alisema kimsingi mahitaji ya damu ni makubwa kwani hospitali hiyo
inahitaji chupa za damu 100 hadi 150 kwa siku, lakini chupa zinazopatikana ni 60 na kwamba, upungufu ni asilimia 25.
Mkuu wa Idara ya Maabara wa MNH, Dk. Alex Magesa alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na hospitali katika kukusanya damu, zoezi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uchache wa vitanda vinavyotumika wakati wa kutoa damu.
Alizitaja changamoto zingine kuwa ni jokofu kubwa la kiibailojia kwa ajili ya kuhifadhia damu na usafiri wa kwenda kukusanya damu nje ya hospitali.
Katika kuadhimisha siku ya wachangia damu duniani, Hospitali ya Taifa Muhimbili imetembelea maeneo mbalimbali ya wazi, ikiwemo vyuoni kwa ajili ya kukusanya damu.
Maadhimisho hayo, ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Dodoma, yamebeba kauli mbiu isemayo ‘Damu inaunganisha kila mtu.’
No comments:
Post a Comment