Wednesday, 15 June 2016
TANESCO YAPIGWA MARUFUKU KUAGIZA TRANSFOMA KUTOKA NJE
Jonas Kamaleki-Maelezo -Dodoma
SERIKALI imeliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), kutoagiza transfoma nje ya nchi, badala yake litumie zinazotengenezwa hapa nchini na Kampuni ya Tanalec.
Agizo hilo lilitolewa bungeni mjini Dodoma, jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kusini (CCM), Daimu Iddi Mpakate.
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua ni lini serikali itatoa pesa kukamilisha miradi ya umeme ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Dk. Kalemani alisema uzalishaji wa transforma ni mkubwa, ikilinganishwa na mahitaji ya bidhaa hizo kwa mwezi, hivyo hakuna sababu ya kuagiza transforma hizo nje kwa bei kubwa wakati zinapatikana hapa nchini.
Akizungumzia utaratibu wa kugharamia nguzo za umeme katika
mpango wa REA, Dk. Kalemani alisema mteja hatakiwi kutozwa gharama yoyote zaidi ya sh. 27,000.
Dk. Kalemani alisema serikali inatekeleza mradi wa REA Awamu ya II katika wilaya ya Tunduru na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema kazi ya kupeleka umeme katika wilaya hiyo ni pamoja na ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33, yenye urefu wa kilomita 293. 2 na ujenzi wa njia nyingine yenye msongo wa kilovoti 0.4, yenye urefu wa kilomita 76.1 na ufungaji wa transfoma 38. pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 3,330
“Gharama ya mradi kwa mkoa wa Ruvuma, ikiwemo wilaya ya Tunduru ni shilingi bilioni 32.56,” alisema Dk. Kalemani na kuongeza kuwa, mkandarasi ameshalipwa sh. bilioni 27.22, sawa na asilimia 83.6 ya fedha.
Dk. Kalemani alisema katika wilaya ya Tunduru, vijiji vinne ndivyo ambavyo vimeunganishiwa miundombinu ya umeme na kufanyiwa majaribio kabla ya kuwashiwa umeme.
Kwa mujibu wa Dk. Kalemani, mkandarasi anaendelea kufunga transforma na mita za luku katika vijiji 34, vilivyosalia katika wilaya ya Tunduru ili viweze kupatiwa huduma ya umeme ifikapo Juni 30, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment