Wednesday, 15 June 2016

LUSINDE ADAI MBOWE ANAHATARISHA AMANI YA NCHI

MBUNGE wa Jimbo la Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, amesema Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe anataka kuhatarisha amani ya nchi kwa kutumia vibaya nafasi alizonazo kisiasa.

Lusinde alisema hayo bungeni jana, mjini hapa, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Mbunge huyo machachari alisema kutokana na vitendo vya Mbowe, ikiwemo kuwashinikiza wabunge wa UKAWA kususia vikao vya bunge, baadhi yao wameanza kumchoka na kuchukizwa naye.

Kwa mujibu wa Lusinde, amekuwa akizungumza na baadhi ya wabunge wa kambi hiyo, ambao wamekuwa wakimweleza wazi kwamba, Mbowe ni dikteta na amekuwa akitumia vibaya madaraka yake.

Alisema wabunge hao wamemweleza kuwa, uamuzi wa kususia bunge ulitokana na shinikizo la Mbowe na haikuwa dhamira yao kumkataa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

"Mheshimiwa Naibu Spika, nimetumwa na wabunge wa upinzani kuja humu ndani kuwasemea kuhusu udikteta wa Mbowe. Wanadai anawaburuza katika maamuzi. Wamesema wanakubali kutoka nje kwa shingo upande kuogopa adhabu, lakini hawaridhiki

"Mbowe ni mchochezi, anataka kuhatarisha amani ya nchi. Demokrasia isiyokuwa na mipaka, sio demokrasia. Leo hii amekwenda Kahama, anakwenda kufanya nini. Kwanini asiende jimboni kwake Hai?" Alihoji Lusinde.

Alisema Mbowe amekuwa na tabia ya kuwaita wabunge wa upinzani katika chai (kantini ya bunge) na kuwapa maelekezo yasiyokuwa na tija kwa ustawi wa nchi, hivyo wameamua kumuagiza (Lusinde) awasemee bungeni.

"Naamini wabunge wa upinzani tuliokuwa tunakunywa chai kantini wananipigia makofi kwa kuwa ujumbe wao nimeufikisha kama ulivyo.
Mbowe aache kuwahadaa wananchi, ana sababu zake za kumkataa Dk. Tulia,"alisema Lusinde.

Alisema mwenyekiti huyo wa CHADEMA anajali zaidi maslahi yake binafsi na hana nia njema ya kuwatumikia wananchi kwa nafasi yake ya mbunge wa Hai.

Lusinde alisema hatua ya Mbowe kwenda Kahama, Shinyanga kwa madai ya kuzungumza na wafuasi wa CHADEMA, ni uchochezi unaotakiwa kukomeshwa na serikali ili kuepuka uvunjifu wa amani.

Alisema Mbowe na wabunge wa upinzani wanatakiwa kuwasemea wananchi wa majimbo yao wakiwa ndani ya bunge na si kwenda mitaani kueneza siasa za chuki dhidi ya serikali ya awamu ya tano.

Mbunge huyo aliwataka wabunge wa upinzani kumpa nafasi Rais Dk. John Magufuli kutelekeza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema hatua ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016-2017, kutenga asilimia 40, katika miradi ya maendeleo, inaonyesha dhamira ya Rais Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Lusinde alimtaka Mbowe kumuacha Rais Magufuli na serikali yake kuwatumikia wananchi baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema hakuna sababu ya wabunge wa upinzani kupanda katika majukwaa kumsema vibaya Dk. Tulia au Rais Magufuli kwa kuwa uchaguzi umeshapita.

"Tumuache Rais afanyekazi, uchaguzi umepita, hata Mufti au Askofu wakishachaguliwa, wanaachwa wafanyekazi,"alisema Lusinde.

Lusinde alisema licha ya wabunge wa kambi ya upinzani kususia vikao vya bunge, wabunge wa CCM wataendelea kutetea maslahi ya majimbo yao kwa manufaa ya wananchi.

No comments:

Post a Comment