MANISPAA ya Kinondoni imesitisha posho za watumishi wake zaidi ya 8,000, kwa lengo la kununua madawati 18,743, kwa ajili ya shule zote za wilaya hiyo, yatakayogharimu sh. bilioni moja.
Posho hizo ni zile za muda wa ziada wa kila siku katika idara mbalimbali, isipokuwa madaktari walioko kwenye hospitali za wilaya hiyo.
Akizungumza Dar es Saalam, jana, wakati akikabidhiwa hundi ya mchango wa fedha za madawati kutoka Kanisa la Pool of Siloam, Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Ali Hapi, alisema wilaya yake itakwenda kwa kasi inayohitajika na kuhakikisha inamaliza tatizo hilo katika muda uliotolewa na Rais Dk. John Magufuli.
Hapi alisema changamoto kubwa ya uhaba wa madawati na ukosefu wa majengo, zinatokana na sera mpya ya elimu bure, ambayo imesaidia kuleta chachu ya elimu na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi.
"Manispaa yetu imejiongeza katika maarifa tuliyonayo na tumeona tujifunge mkanda katika kutekeleza agizo hili la serikali la kuhakikisha tunakuwa na madawati ya kutosha kwenye shule zetu,"alisema.
Hapi alisema baada ya kufikiwa kwa uamuzi huo wa kusitisha matumizi ya posho ya hizo za muda wa ziada, zimepatikana sh. bilioni moja na kwamba, ambazo zimewezesha kupatikana kwa madawati 12,091, kwa ajili ya shule ya msingi na viti 6,552 na meza 6,552 kwa ajili ya sekondari.
Wakati huo huo, Hapi amepokea sh.milioni 19, kutoka Kanisa la Pool of Siloam kwa ajili ya kutengenezea madawati.
Hapi alisema ni kwa mara ya kwanza kwa taasisi hiyo ya kidini kuchangia mchango wa madawati na kwamba, hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika sera ya elimu bure.
"Taasisi yenu imeonyesha mfano mzuri wa kuigwa kwani ni kila wajibu wa taasisi zote za dini kuwajibika kutatua changamoto za jamii yetu badala ya kuitegemea serikali pekee," alisema.
Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo, Elisha Elia Miaka Mia, alisema taasisi hiyo inaunga mkono sera ya elimu bure na kwamba, itaendelea kuichangia.
"Kanisa lina wajibu mkubwa wa kutatua matatizo na changamoto katika jamii inayotuzunguka, hii pesa ni michango na sadaka ya Watanzania wanyonge kwa ajili ya upendo wa serikali yetu," alisema.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob, alisema hatua zinazofanywa na manispaa hiyo ni kuhakikisha Agosti,mwaka huu, tatizo la uhaba wa madawati linamalizika.
No comments:
Post a Comment